26.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Kamati ya Bunge yaonya miradi ya afya kutopelekewa fedha

Na ARODIA PETER

-Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, imeitaka Serikali kupeleka fedha zote zilizoainishwa na Bunge ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Akisoma maoni ya Kamati hiyo bungeni jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba alisema miradi yote ya maendeleo iliyokuwa imetengewa fedha kwa mwaka 2018/2019 na ambayo waliikagua haikupelekewa fedha zozote.

Mbali na hilo, kamati imeitaka Serikali kuangalia na kurekebisha upungufu wa watumishi wa afya hususan kwa hospitali za rufaa za mikoa ambazo zinakabiliwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa.

Serukamba alitolea mfano wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala akisema kuna haja ya hatua za haraka kuchukuliwa ili kupunguza adha hiyo.

“Pamoja na hiyo, changamoto nyingine ni uchakavu wa miundombinu inayohitaji ukarabati mkubwa, ukosefu wa nyumba za watumishi, ukosefu wa huduma za ufuaji na mlolongo mrefu wa manunuzi maalum katika Bohari ya Dawa (MSD) hasa kwenye vitendanishi vya maabara.

“Kamati imebaini changamoto ya malipo mbalimbali zikiwamo motisha ya posho ya nyumba, motisha ya saa za ziada kwa watumishi wa afya ni kubwa na inaweza kuathiri utendaji wao wa kazi, Kamati inashauri Serikali kulibeba suala hili kipekee na kulitafutia ufumbuzi wa haraka”alisema Serukamba.

Serukamba ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM) alisema Kamati inaishauri Serikali kukamilisha mchakato wa uletwaji wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote bungeni uweze kuwa sheria na kuanza utekelezaji kwa kuhakikisha kila mwananchi afya yake inalindwa kwa kuwa na bima ya afya ya uhakika.

“Aidha wakati mchakato huo unaendelea Serikali ianze kupanga mikakati ya namna gani watahamasisha jamii kwa ajili ya kuelewa umuhimu wa bima hiyo ili wakati wa utekelezaji kusiwepo changamoto ya kutokukubali licha ya kuwapo sheria.

Kwa upande wa kambi rasmi ya Upinzani bungeni, imehoji amri za wanasiasa wasiokuwa na mamlaka ya nidhamu kuwawajibisha madaktari bila kufuata utaratibu unaostahili kwa waajiriwa wa umma.

Akisoma hotuba ya bajeti ya Wizara Kivuli ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema), alisema katika Serikali ya awamu ya tano kumekuwapo na wimbi na mwendelezo wa matukio sit u yanayodhalilisha taaluma za watumishi wa sekta ya afya bali na kuishusha thamani.

Matiko alisema zipo hatua na taratibu za kinidhamu  kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma kwa madaktari wote waajiriwa.

Kwamba kwa mujibu wa sheria na kanuni, ni pamoja na Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) ama Baraza la Wauguzi ndiyo wenye mamlaka ya kutoa onyo na kuwasimamisha ama kuwafutia sifa udaktari ama wauguzi watakaopatikana na hatia baada ya malalamiko ya kutowajibika.

“Mwezi Machi 2017, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai alitangazwa na Jumuiya ya Madaktari Tanzania kuwa adui namba moja wa afya baada ya mkuu huyo kumuweka mbaroni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Dk Vitalis Katalyeba baada ya kusimamishwa kazi kwa kutuhumiwa kuchelewesha gari la wagonjwa na kusababisha kifo cha mgonjwa.

“Tukio jingine nila Mkuu wa Wilaya ya Singida, Rehema Nchimbi alipomuweka rumande Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida, Dk Erivk Bakuza pamoja na kwamba kulikuwa na upungufu wa kiutendaji bado taratibu za kiutendaji zilitakiwa kufuatwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles