24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

KAMANDA MAMBOSASA VALIA NJUGA RUSHWA

JESHI la Polisi limekuwa likinyooshewa kidole kila kukicha kutokana na baadhi ya askari wake kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya upokeaji wa rushwa.

Vitendo hivyo vinaonekana kufanywa na askari wachache ambao wameamua kutumia nafasi zao kuwaumiza wananchi wa kawaida ambao masikini wa Mungu wamekuwa wakihangaika kujitafutia riziki.

Pamoja na kuwapo na shughuli za kila siku za jeshi hilo, lakini limekuwa likifanya kazi kwa karibu na wananchi  ambao wakati mwingine ndiyo msaada mkubwa kwao.

Leo tumelazimika kuanza kuyasema haya, baada ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro  Mambosasa kutoa karipio kali kwa baadhi ya askari  wanaojihusisha na rushwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya askari mmoja aliyejipachika jina la ‘Faru John’ kudaiwa amekuwa kinara wa kuomba rushwa ya Sh 20,000 kutoka kwa wananchi wa eneo la Mbagala, Dar es Salaam.

Baada ya kuwapo malalamiko hayo, Kamanda Mambosasa hakusita kuchukua hatua za kumwita askari huyo ili afikishwe ofisini kwake kwa ajili ya mahojiano.

Tunafurahi kusikia ‘Faru Jon’ amehojiwa na kamanda mwenyewe na uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini ukweli wa tuma hizi.

Tunaamini ahadi ya Kamanda Mambosasa ya kuwa askari huyo ataendelea kufuatiliwa mwenendo wake, tunaona ni hatua nzuri na ya msingi ambayo kwa kweli inaweza kusaidia kuibua askari wa aina hiyo.

Ni aibu kwa askari aliyepata mafunzo na kula kiapo cha kutumikia chombo hicho, kisha kujipachika jina la kipuuzi eti Faru John kwa nia ya kufanya uhalifu wa aina hii, tunasema jambo hili halikubaliki.

Hatua hii inaonyesha wazi mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa askari hawa ambao kwa maadili yao tu ni kulinda raia na mali za wananchi, hivyo wale wote watakaobainika kuomba au kupokea rushwa waondolewe.

Lakini mwenendo huu, tunaona wazi umeota mizizi na hatua kali zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kurejesha nidhamu kwa askari wachache wanaolipaka tope jeshi hilo.

Haiwezekani na haiingi akilini eti askari wengi wanadaiwa kuwa wamegeuka kuwa wajasiriamali wa kukusanya fedha za hongo kwa wananchi, badala ya kutimiza wajibu wao wa kila siku.

Kwa mfano, mkazi mmoja wa Mbagala amemwomba Kamanda Mambosasa kuwahamisha askari wote wa Kituo cha Maturubai kwa kutuhuma kuwa hawakamati wahalifu, bali wapo kwa ajili ya kupokea rushwa tu.

Jambo hili si dogo, kama wananchi wamefikia kuelezea  hadharani ni wazi kuna tatizo kubwa la msingi. Lakini jambo jingine la kusikitisha  ni jeshi hili kufunga vituo vyake mapema tofauti na zamani. Kitendo hiki kimekuwa kero kubwa kwa wananchi waonafika vituo kuhitaji huduma.

Sisi MTANZANIA, tunamshauri Kamanda Mambosasa kuchukua hatua za kinidhamu bila kumwonea askari, tunaamini kwa kufanya hivyo tuhuma hizi za rushwa zinaweza kufika sehemu zikapungua kuliko kuongezeka siku hadi siku.

Lakini pia kuwafukuza wale wote wenye tabia kama ya ‘Faru John’ ambaye inaonekana wazi amesaliti kiapo chake mbele ya mwajiri, amebweteka kiasi cha kuonekana yeye ni zaidi kuliko jeshi.

Tunamalizia kwa kusema siku zote polisi lazima wafanye kazi karibu na wananchi kwa sababu ndiyo jukumu walilokabidhiwa, sasa iweje  wageuke kuwa wakusanya mapato haramu?

Tunaamini kwa tukio hili la Mbagala litakuwa mfano kwa askari wote wa Kanda Maalumu ambao wanajiona wako juu ya jeshi hili. Ndiyo maana tunasema Kamanda Mambosasa  valia njuga rushwa hii kwenye kanda yako.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles