27.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

Kama sikuwatuma watekaji, sitakubali wanizidi nguvu

Na ANDREW MSECHUKWA wiki kadhaa sasa nimekuwa nikifuatilia kwa karibu kuhusu utekwaji wa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji (Mo) na namna chombo kikuu kinachowajibika kuhakikisha wananchi na mali zao wanakuwa salama, Jeshi la Polisi lilivyoendelea kupambana kuhakikisha anapatikana na kuwanasa watekaji.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro ameonesha imani na weledi wa jeshi lake, akiwahakikishia Watanzania kwamba lazima Mo atapatikana akiwa mzima na wateka nyara waliomteka watapatikana, wakiwa hai au wamekufa.

Kaili inayotia matumaini, kwa mkuu wa chombo anachokiongoza, anachoamini katika weledi wake na kwamba kutokana na uimara wa watendaji wake, hahitaji kupata usaidizi kutoka vyombo vya nje ambavyo aidha vina uzoefu na weledi wa hali ya juu zaidi kutokana na kuwahi kukabiliana na matukio ya aina hiyo ambayo kwetu bado ni mapya kiasi.

Kiongozi wa Wizara inayosimamia Jeshi  linaloongozw ana IGP, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametoa maagizo kadhaa tangu kutekwa kwa Mo, lakini ufafanuzi wake wa mwisho ni pale alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Oktoba 28 akisema suala la utekaji wa raia halivumiliki.

Katika mazungumzo yake, Lugola alisema licha ya mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ kupatikana, bado polisi ina kazi kubwa ya kuwasaka watu wengine waliotekwa hadi mtu wa mwisho atakapopatikana.

Alisema kila Mtanzania ana thamani sawa na mwingine bila kujali haiba na mwonekano kwa jamii, hivyo akaomba wananchi kupunguza kulisema vibaya Jeshi la Polisi ili kulipa nafasi lifanye kazi yake.

Wakati Lugola akisema hivyo, siku hiyo hiyo Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe aligusia suala la usalama nchini katika mkutano wake na wanahabari huku akiwataka Watanzania kuendeleza  juhudi na mshikamano kama walivyofanya kwa Mo, aliyetekwa Oktoba 11 na kupatikana usiku wa kuamkia Oktoba 22.

Huku akitaka waliokwishapotea kusakwa na kupatikana wakiwa hai ama wamekufa, Zitto aliwataja baadhi ambao hadi sasa hawajapatikana kuwa ni kada wa Chadema, Ben Saanane; mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Mwananchi, Azory Gwanda na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Simon Kanguye.

Aliwataka Watanzania wasibweteke baada ya Mo kupatikana, waendelee kuweka presha na msisitizo kwa watawala ili wengine wapatikane, wasikae kimya, akiwasihi wananchi waendelee kushikamana.

Zitto pekee ndiye mtu asiyekuwamo ndani ya Serikali ambaye hata baada ya Mo kupatikana, ameendelea kuzungumzia matukio haya. Wengine ni Lugola na wenye jukumu la kuendelea kuzungumzia hilo wakati wote ni Polisi, ambao kwa sasa kauli yao ni moja, kuwa wanaendelea na operesheni hivyo wasiingiliwe.

Operesheni hii ya Polisi kuwasaka watekaji wa Mo, hasa ikizingatiwa kwamba ni karibu miaka mitatu tangu matukio ya utekaji na upoteaji wa watu katika mazingira ya kutatanisha bila kupata majibu ya uchunguzi, waliopotea kutopatikana na waliopotezwa kutojulikana waliko, kunatoa sababu ya Watanzania kutokaa kimya.

Katika kutafakari, nikarejea na kukumbuka hadithi ya kisa cha raia wa Israel waliotekwa katika ndege na kupelekwa Entebbe, Uganda katika ndege Juni 27,1976 mara tu ndege yao ilipoanza kuruka katika Uwanja wa Ndege wa Athens nchini Ugiriki ikielekea Tel-Aviv.

Juni 29, 1976, baada ya kuwa angani kwa muda wa siku mbili hatimaye ndege hiyo, Air France Flight 139 ilitua uwanja wa ndege wa Entebbe, Uganda zaidi ya umbali wa kilomita 4,000 kutoka Israel.

Hii ni hadithi ya operesheni ya uokozi kutoka kwa watekaji, iliyopewa jina la Oparesheni Entebbe/ Operesheni Thunderbolt (Operesheni radi) au kama mwandishi mmoja aliyoiita ‘Dakika 90 Entebbe’, yaani  operesheni ya lisaa limoja na nusu iliyowafikisha askari maalumu wa Israel Uganda, kuwachukua raia wao na kuondoka nao kwa gharama yoyote.

Operesheni hii iliandaliwa baada ya Waziri Mkuu wa Israel  (wakati huo), Yitzhak Rabin kukutana na kufanya kikao cha siri na Mkurugenzi Mkuu wa Ujasusi la Israel (MOSSAD), Meja Jenerali Yitzhak Hofi. Kikao hicho cha siri kilifanyika kwenye makao makuu ya MOSSAD jijini Tel Aviv, muda mfupi baada ya taarifa za kutekwa kwa ndege hiyo.

Hadithi hii ya kweli, pia iliwekwa katika kumbukumbu na mwandishi William Stevenson, katika kitabu chake cha ‘90 minutes in Entebbe’ kilieleza namna wateka nyara hao wakiwamo Wapalestina, mjerumani aliyekuwa mfuasi wa kikundi cha wanaharakati.

Katika utekaji huo, inasadikiwa kiongozi wa chama cha ukombozi wa Palestina cha Populist front for Liberation of Palestine (PFLP), Dk. Wadi Hadad ambaye alikuwa mwanaharakati alishiriki katika kupanga utekaji huo.

Ndege hiyo ya Ufaransa ‘Air France Flight 139’ ikiwa na abiria 248 ndani yake ilitekwa na magaidi  wanne. Ambao walikuwa Wapalestina wawili na Wajerumani wawili.

Lakini haitasahaulika kwamba katika mipango hiyo, mpiganaji wa kukodiwa aliyekuwa na ujuzi na uzoefu wa hali ya juu, Irlich Ramirez Sancez (Carlos – The Jackal) ambaye aliogopeka sana katika maeneo hayo kwa nyakati hizo alidaiwa kuhusishwa.

Simulizi inaeleza kuwa aliyekuwa kiongozi wa kijeshi wa Uganda aliyeingia madarakani kwa Mapinduzi wakati huo, Iddi Amin Dada ambaye hakuwa katika uhusiano mzuri na Israel wakati huo, aliunga mkono harakati za Palestina na kwa maana hiyo, aliruhusu ndege hiyo kuingia Entebbe ikitokea Tripoli, Libya ilipokuwa imeweka mafuta ikiwa ni kituo cha kwanza baada ya kutekwa.

Tukio hili, liliibua madai ya watekaji baada ya kufika Entebbe na kupokelewa na Amin mwenyewe, ambapo siku mbili baadaye walitaka kubadilishana mateka wao na wafuasi wa kikundi cha wanaharakati ambao walikuwa wakishikiliwa katika nchi za Ulaya na Afrika.

Kwa kuwa Israel ilijua vyema uwezo wa jeshi la Iddi Amin, kutokana na maafisa wengi wa jeshi la Amin kupata mafunzo kwao, Shirika la MOSSAD liliamua kumtumia jenerali wake mstaafu aliyeitwa Chain Bal Lev ambaye alikuwa rafiki wa Amin kuzungumza naye.

Operesheni Thunderbolt inatajwa kuwa ya kipekee, iliyokuwa si rahisi kusadikiwa lakini iliyokuwa na matokeo yaliyoushangaza ulimwengu, baada ya makomandoo kuwasili Entebbe majira ya saa sita usiku wakitokea Telviv, huku ndege waliyoitumia ikiwa imezimwa taa za ndani na za nje huku ikiwa na muungurumo hafifu.

Kutokana na umahiri na weledi uliotumiwa na Mossad katika operesheni hiyo, Waisrael walifika katika ndege mbili, moja ikiwa imebaki Nairobi, Kenya ikiwa na vifaa muhimu vya tiba wakati iliyokwenda Entebbe ilikuwa na gari mbili zilizotumiwa na makomandoo hao kufika kwenye jengo walimokuwamo mateka wao, ambao pamoja na waliowateka nyara, walikuwa wamekusanyika kwenye eneo la mapumziko la uwanja huo.

Julai 4, 1976, siku tisa tangu kutekwa kwa raia hao wa Israel, kwa operesheni ya dakka 90 kikosi cha makomandoo wa Israel kilifanikiwa kuondoka na raia wake 102 kati ya 106, raia wake mmoja akiuawa na watano kujeruhiwa, huku wakimpoteza komandoo wao mmoja baada ya kuuawa.

Simuzili hii inatupa picha namna ambavyo mataifa mengine yamekuwa yakipigania uhai na uhuru wa raia wao kwa gharama, likiwa ni tukio la zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Kwa Tanzania, tangu matukio ya utekaji nyara ya hivi karibuni yalipoanza kuripotiwa, suala la taarifa kuhusu kinachoendelea katika operesheni ni siri na hata baada ya muda kupita na kutokuwapo maendeleo yoyote, itaendeela kuwa siri.

Nikiwa na mamlaka ya juu katika vyombo vya ulinzi na usalama, hasa kama ilivyo kwa jeshi la Polisi, nitahakikisha ninatangaza ushindi kwa vitendo kwa wateka nyara wote, kwa kuwatia mikononi kwa operesheni za muda mfupi ili kuwaonesha uwezo wa jeshi langu.

Kwa kuwa kuna watu watakaokuwa wakitaka kuonesha kwamba jeshi langu halina uwezo, nitawahakikishia kwamba lina uwezo na weledi wa hali ya juu, kwamba hawatapata nafasi ya ‘kunyoosha midomo yao’ si kwa kuwatisha, bali kwa kuhakikisha hakuna anayetekwa na kabla yeyote hajatekwa, tunawanasa watekaji.

Nikiwa na mamlaka ya juu katika jeshi hili lililopewa dhamana ya ulinzi wa watu na mali zao, nitawafunga mdomo wanaodai kwamba watendaji wangu wanajua waliko waliopotea kwa kuwaletea uthibitisho wa kupatikana kwao, mabaki yao na vipimo vya vinasaba (DNA) na hakika, watatambua kwamba watendaji wangu wana weledi uliotukuka.

Nitafanya tofauti kwa kuwathibitishia wote wenye mashaka na weledi wa watendaji wangu na kudhani kwamba ni lazima tupate msaada kutoka nje, kwa kutumia mbinu za kisasa kuhakikisha hatusumbuliwi tena na hawa watekaji kama waliomteka Mo na kuja kumtelekeza jirani na ofisi zangu, siku moja baada ya kutoa amri ya kutaka aachiwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles