24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Angela  Merkel wa Ujerumani  aamua kuipa mgongo siasa

*Ataendele kuwa Kansela hadi 2021

Na  OTHMAN MIRAJI, UJERUMANIENZI ya Angela Merkel hapa Ujerumani inamalizika. Desemba mwaka huu ataacha kuwa kiongozi wa chama tawala cha Christian Democratic (CDU). Lakini atabaki bado kuwa Kansela (mkuu wa Serikali) hadi mwaka 2021. Baada ya hapo hatawania tena wadhifa huo. Nani watakaokamata nafasi zake hizo ni jambo linalowashughulisha si tu Wajerumani wenyewe lakini pia watu wa nchi za nje.

Oktoba 29, mwaka huu kwa namna fulani, ilikuwa ni siku ya kihistoria kwa Ujerumani, pale Kansela Angela Merkel aliporipua bomu la kisiasa. Na yote ilitokana na hasara kubwa ya kupoteza kuungwa mkono na wapigaji kura ilichopata chama chake cha CDU na pia Serikali ya Mseto ya Shirikisho anayoiongoza ya vyama vya CDU (Christian Democratic), CSU (Christian Social) na SPD (Social Democratic). Siku ya pili baada ya kujulikana kwamba CDU ilipoteza asilimia 11.3 ya kura katika uchaguzi wa Mkoa wa Hesse na pia SPD ilipoteza asilimia 10.9, Merkel alibwaga manyanga na kuchukua uamuzi uliokuwa kinyume na alivyopanga hapo awali. Alitangaza kwamba hatapigania kuwa tena kiongozi wa CDU katika Mkutano Mkuu wa chama hicho hapo Desemba mwaka huu.

Katika mkutano na waandishi wa habari Merkeli alisema kwamba, hata hivyo, atabakia kuwa Kansela katika kipindi chote kilichobaki cha Bunge la sasa hadi mwaka 2021. Baada ya hapo ataacha shughuli zote za siasa. Aliendelea kusema kwamba japokuwa yeye maisha alihisi kwamba vyeo vya kiongozi wa chama na ukansela vinafaa vikamatwe na mtu mmoja, yaani ni uzuri mtu mmoja avae kofia hizo mbili, lakini hivi sasa, baada ya kuzingatia faida na hasara za jambo hilo, amefikia uamuzi kwamba kuzitenga kofia hizo mbili ni jambo linalokubalika.

Angela Merkel alikiri, lakini bila ya kujimwagia sifa mwenyewe, kwamba ilikuwa fahari kwa yeye kukiongoza chama cha CDU kwa miaka 18 na hivi sasa anahisi na anaamini kwamba umewadia wakati wa  kufungua ukurasa mpya wa kitabu. Haijahitaji kuwa mwanasiasa mzoefu na mahiri kama Merkel (amekuwa Kansela kwa miaka 13 sasa) kuzitambua na kuzisoma waziwazi herufi zilizoandikwa ukutani, ikiwa siku moja baada ya wapigaji kura wa Mkoa wa Hesse kutoa kauli yao. Kura za CDU zilipungua mno. Pia wiki mbili kabla chama ndugu cha CSU katika uchaguzi wa Bunge la mMkoa wa Kusini wa Bayern kilipoteza zaidi ya asilimia kumi ya kura.  Zaidi ya hayo, uchunguzi wa maoni ya wananchi unaonesha kwamba pindi uchaguzi mkuu wa Ujerumani nzima utafanywa sasa, basi CDU ya Angela Merkel itaambulia si zaidi ya asilimia 24 ya kura. Chama kingine kikubwa, SPD, nacho hakitasalimika kupoteza kura nyingi.

Mwenyewe Kansela Merkel anatambua kwanini chama chake kimefikia katika hali hiyo ya kusikitisha na ya kuvunja moyo. Sura ya Serikali ya Mseto anayoiongoza si nzuri hata kidogo mbele ya wananchi. Aliungama kwamba hali hiyo haikubaliki na sababu si tu mabishano miongoni mwa mawaziri wa serikali yake, lakini pia utamaduni wa kutekeleza kazi ndani ya serikali yenyewe. Yaonesha Serikali ya Merkle inashindwa kuyaelewa matakwa ya wananchi, sembuse tena kuyatekeleza kivitendo matarajio yao.

Tangu kuundwa Serikali ya Mseto ya Shirikisho Machi, mwaka huu Ujerumani imejionea mabishano kadhaa baina ya vyama ndugu vya CDU na CSU pamoja na kutofautiana baina ya viongozi wa vyama hivyo, Kansela Merkel na Waziri wa Mambo ya Ndani, Horst Seehofer. Pia chama shirika serikalini, SPD, kinapoteza umaarufu miongoni mwa wanachama wake ambao kila siku zikienda wanadhani hakuna faida kwa chama hicho kubakia serikalini. Ikumbukwe kwamba ilichukuwa muda mrefu-tangu Uchaguzi Mkuu wa Septemba mwaka jana hadi Machi mwaka huu- kuweza kuundwa Serikali ya Mseto hapa Ujerumani baina ya CDU, CSU na SPD.

Nchi shirika na Ujerumani zilishangazwa na uamuzi wa Merkel, lakini ziliuheshimu, japokuwa Serikali ya Marekani ambayo wakati wa karibuni imekuwa na uhusiano usiokuwa mchangamfu sana na Ujerumani ilisema kung’atuka kwa Merkel ni suala la mwenyewe Kansela na Wajerumani.

Kuna nchi za Ulaya zitakazopumua kuondoka Merkel kutoka ulingo wa kisiasa. Miongoni mwa hizo ni nchi kama Ugiriki zilizoshuhudia ukaidi wa Ujerumani chini ya Merkel pale Berlin iliposhikilia kuwekwa masharti magumu ya kupatiwa mikopo nchi hizo zilipokabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha. Nchi hizo zimeiona Ujerumani chini ya Merkel ikitumia misuli yake ya kiuchumi kuzibana nchi nyingine ndogo za Ulaya. Lakini Ujerumani hiyohiyo chini ya Merkel imesifiwa kuwa mbele katika kupigania usafi wa mazingira duniani na kutaka migogoro ya kimataifa itanzuliwe kwa njia za amani. Mchango wa Ujerumani katika kuutanzua mzozo wa kifedha barani Ulaya mwanzoni mwa mwongo huu ulikuwa mkubwa.

Atakapoondoka kabisa Merkel kutoka ukumbi wa kisiasa basi nusu ya kipande cha historia ya Ujerumani kwa vijana walio sasa umri wa miaka 20 kitamalizika. Vijana hao wanaujua tu ukansela wa Angela Merkel kama wale waliokuwa na umri wa miaka 40 wanavyomkumbuka Helmut Kohl. Katika mkutano wake wa kwanza wa kilele wa dunia Angela Merkel alizungukwa mezani na watu mashuhuri, kama kina George Bush (Marekani), Jacques Chirac (Ufaransa) na Tony Blair (Uingereza). Katika miaka iliyofuata walikuwapo  wakuu wengi wengine na ilionesha hadi karibuni kana kwamba hao wote wengine watapita isipokuwa Merkel.

Tangu uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2017 hapa Ujerumani mambo yalianza kumbadilikia Merkel. Punde baada ya kuanza kumiminika wakimbizi wa kigeni mwaka 2015 siasa za Kansela huyo zilianza kushambuliwa, tena kwa sauti kali, hata ndani ya chama chake. Mabishano ndani ya serikali yake na pia chama chake kupoteza kura katika chaguzi za mabunge ya mikoa ni mambo yaliyomtikisa kisiasa. Nyota yake ilizidi kupungua kung’ara kila siku zikienda.

Suali linaloulizwa sasa ni: nani atachukua nafasi za Merkel? Kuna nafasi mbili. Desemba mwaka huu kuna nafasi itakayokuwa wazi ya mkuu wa Chama cha CDU. Majina yanayotajwa na ambayo moja huenda likaijaza nafasi hiyo ni Annegret Kramp-Karrebauer (56) ambaye ni Katibu Mkuu wa sasa wa CDU na anayezungumzwa kwamba ni rafiki mkubwa wa kisiasa na msiri wa Kansela. Pia kuna Waziri wa Afya, Jens Spahn (38) anayeelemea siasa za kiasilia. Asisahauliwe pia Friedrich Merz (62) aliyewahi kuwa mkuu wa wabunge wa CDU, lakini akaacha siasa baada ya kutofautiana na Merkel na kujishughulisha na biashara. Uamuzi wake wa kurejea katika siasa unatafsiriwa ni kulipizia kisasi kushindwa kwake hapo kabla na Angela Merkel katika kuwania uongozi wa CDU. Nafasi ya kuwa kiongozi wa CDU huenda pia ikaenda kwa Spika wa sasa, Wolfganga Schäuble (76), aliyewahi kuwa waziri wa fedha. Lakini huyu, kutokana na umri wake, huenda akawa mtu wa kujishikiza tu.

Kipindi cha mwaka mmoja uliopita kimekuwa kigumu kwa Angela Merkel. Mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu uliopita ndipo alipotangaza atawania tena nafasi ya ukansela. Wakati huo alisema kwamba ilikuwa si rahisi kwake kufikia uamuzi huo. Huenda alitaka aachane na siasa. Lakini huo pia ulikuwa wakati ambapo Donald Trump punde alishinda uchaguzi nchini Marekani na utabiri ulionesha kwamba mambo huenda yasiwe mazuri huko mbele. Chama cha CDU kilitikisika katika suala la Ujerumani kuwapokea malaki ya wakimbizi wa kigeni, nayo Uingereza ilishaanza kufanya mashauriano ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya. Licha ya hayo, Merkel aliamua kuendelea kubeba dhamana na kuikabili kwa ujasiri mitihani iliyoko mbele ya nchi yake.

Pale uchaguzi mkuu ulipofika wafuasi wa vyama vya Pegida na AfD vya siasa kali za mrengo wa kulia na za kibaguzi walichomoza kila upande wakimtaka Kansela aachie ngazi. Vyama vya CDU na CSU vilijaribu kutafuta suluhisho kuhusu suala la wakimbizi, lakini ilikuwa si rahisi, mara kadhaa vilibishana na pale mapatano yalifikiwa basi yalishindwa kutekelezwa. Ilionesha kana kwamba kiongozi wa CSU, Horst Seehofer, alikuwa anamwandama kisiasa Angela Merkel.

Mwaka jana vyama ndugu vya CDU/CSU vilishinda uchaguzi mkuu, lakini vilipoteza asilimia tisa ya kura ukilinganisha na uchaguzi wa mwaka 2013. Chama cha kiliberali cha Free Democratic (FDP) kilichoalikwa na Merkel kuungana naye katika Serikali ya Mseto kilijitoa katika mazungumzo na kumuacha Merkel awe hana chaguo jingine isipokuwa kuunda Serikali ya Mseto na SPD. Ilimlazimu pia akubali chama chake kisalimu amri, kiache kushikilia wizara muhimu zilizokwenda kwa SPD. Alifanya hivyo ili angalau nchi ibakie kuwa na umoja na pia kuwa na serikali  imara.

Japokuwa Merkel amesema hatavaa tena kofia ya mkuu wa CDU baada ya Desemba mwaka huu, lakini ataendeela kuwa Kansela hadi 2021, uzoefu wa siasa nchini Ujerumani umeonesha kwamba ni busara kofia hizo mbili kuvaliwa na mtu mmoja. Kuwa kiongozi wa chama kunamuongezea madaraka Kansela. Kunaweza kukatokea mikwaruzano baina ya mkuu wa chama na Kansela na hivyo kuidhoofisha serikali na pia chama tawala. Lakini bado kuna watu, japokuwa ni wachache, wanaodhani kwamba Merkel anaweza akashawishiwa au kulazimika kuufikiria upya uamuzi wake huu aliouchukua sasa. Kauli ya mwisho kabisa kabisa bado haijatamkwa. Bado kuna muda hadi Desemba na katika siasa hata siku moja ni muda mrefu.

Umaarufu wa Merkel wakati fulani uliwahi kufika juu kabisa kileleni, lakini baadaye uliteremka chini. Wapiga kura wengi wa CDU wamekimbilia Chama cha Kijani na kile kinachopinga Ujerumani kumiminikiwa na raia wa kigeni, AfD. Na licha ya chama kingine kikubwa, SPD, kupoteza kura, CDU hakijafaidika. Yote hayo hayajasababishwa tu na Merkel, lakini pia na uchokozi wa kila wakati kutoka chama ndugu cha CSU. Kwa vyovyote vile, Merkel akiwa nahodha wa meli, hawezi kukwepa kubeba dhamana ya hayo yaliotokea.

Angela Merkel ameweka historia, si tu kama Kansela wa kwanza wa kike nchini Ujerumani, si tu kama mwanamke aliyekuwa na nguvu kubwa kabisa za kisiasa duniani, si tu kama Kansela aliyekuwa madarakani kwa muda mrefu kama vile Helmut Kohl, lakini anaacha madaraka bila ya kulazimishwa, bila ya kushindwa katika uchaguzi mkuu, tena kwa hiyari yake na kwa heshima, bila ya kusukumwa na bila ya kufanya kashfa. Yeye anaamini kwamba kuondoka kwake kutoka jukwaa la kisiasa kunatoa nafasi zaidi kuliko kuwa hatari kwa nchi yake, Serikali ya Shirikisho na pia chama chake.

Sasa CDU ina wakati, kwa utulivu, kutafuta nani atakuwa Kansela mpya baada ya 2021, pindi nacho Chama cha SPD, licha ya umaarufu wake kwenda chini hivi sasa, hakitaamua kujitoa serikalini na kusababisha kuitishwa uchaguzi mkuu mpya wa mapema. Na pindi wana CDU wataendelea kubishana tu wenyewe kwa wenyewe katika kumtafuta Kansela mpya, basi wasijutie na wala wasitarajie kwamba Merkel atarejea na kuwaokoa.

Yaonesha Merkel huyo ameamua kweli kutaka kuyafaidi maisha yake yajayo ya kustaafu. Ametosheka. Hahitaji zaidi ya yale aliyokwisha yafikia maishani mwake, nayo ni makubwa mno. Kama binti wa mchungaji, nahisi Angela Merkel amejifunza vilivyo tabia ya kukinai. Bahati mbaya ni kwamba tabia hiyo iliyotukuka inakosekana miongoni mwa wanasiasa wengi.

Somo lingine kwa wanasiasa. Merkel kila wakati amekuwa karibu na wananchi, akiusikiliza kila wakati namna moyo wa wananchi na wapiga kura unavyopiga. Kweli matokeo ya chaguzi kila wakati yalimpa darasa, lakini hajasubiri  matokeo ya chaguzi yampe somo nini wananchi wanataka na nini hawataki. Hata bila ya kungoja uchaguzi mkuu yaonesha alishapata ujumbe na akachukua uamuzi anaouamini kuwa ni sahihi kwa vile alikuwa kila wakati karibu na wananchi hao.

Kwake yeye madaraka yalimaanisha kuwatumikia watu na nchi yake, na pia wananchi waliomchagua waridhie yale anayoyatenda. Bila ya hivyo, kwake yeye kofia za ukansela na kiongozi wa chama juu ya kichwa chake hazina  maana yeyote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles