KAMA KWELI TUNA DHAMIRA, TUFUFUE VIWANDA VIKUBWA

0
650

SERIKALI ya Awamu ya Tano, pamoja na mambo mengine, imejipambanua kwa kaulimbiu yake ya Tanzania ya Viwanda.

Pengine kama kuna jambo ambalo si tu Rais Dk. John Magufuli anatamani, bali ni Watanzania wote, ni siku moja tupunguze kuagiza, tutengeneze kila kitu hapa hapa nchini.

Hata hivyo, ukiwasikiliza baadhi ya wachumi, wanasiasa na baadhi ya watu, kila anayezungumza anasema hilo bado halijawezekana.

Wanaosema hivyo ni wale wenye mtazamo kuwa uchumi wa viwanda tunaoutamani haufungamanishi sekta nyingine za kilimo na uzalishaji wa malighafi.

Kumbukumbu ambazo zimewahi kuripotiwa kwenye vyombo vya habari, zinaonyesha kuwa, ripoti ya sensa ya viwanda ya mwaka 2013, Tanzana ilikuwa na viwanda 49,243, kati yake asilimia 85.13 ni viwanda vidogo sana, asilimia 14.02 ni viwanda vidogo, asilimia 0.35 ni viwanda vya kati na asilimia 0.5 ni viwanda vikubwa.

Takwimu za Wizara ya Viwanda zilizoandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuendeleza Viwanda (Unido) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, zinaonyesha asilimia 99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo sana.

Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, yaani 2016-21, Sekta ya Viwanda inachangia asilimia 5.2 ya Pato la Taifa.

Ili kufikia malengo, kwa mujibu wa Kambi ya Upinzani bungeni, itailazimu sekta hiyo kila mwaka ikue kwa asilimia 4.35.

Kimsingi Serikali inatambua hilo, ndiyo maana kila taasisi, ikiwamo mifuko ya hifadhi ya jamii, leo hii nayo imelazimika ama imelazimishwa kuzungumza lugha hiyo ya kuanzisha na kufufua viwanda vilivyokufa.

Pamoja na hayo, sisi tunaona ipo haja ya Serikali kupeleka nguvu nyingi katika viwanda vikubwa ambavyo leo hii ama viko katika hali mbaya, au vimefikia mwisho mbaya.

Mifano michache ya viwanda tunavyovizungumza hapa ni Kiwanda cha Nguo cha Urafiki na kile cha General Tyre, ambacho historia yake ya kuwa kiwanda pekee barani Afrika leo hii inaweza kuwa chungu kutokana na kuwa katika hali mbaya.

Tunadhani pamoja na kazi nzuri inayofanywa ya kuanzisha viwanda vidogo, lakini sifa kubwa na pekee ambayo itatufanya tujivune ni kuwa na viwanda vikubwa.

Pengine kwa sababu ya hali yetu au kutoamua, fedha ambayo tumekuwa tukiielekeza kwenye viwanda kama cha General Tyre ni sawa na tone la maji jangwani, kwa kuwa hazitoshi hata kununua mtambo mmoja.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, katika hotuba ya bajeti ya Wizara na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/17, serikali iliahidi kufufua kiwanda hicho.

Katika bajeti hiyo zilitengwa Sh milioni  150 kwa ajili ya kuboresha ekari 510 za mashamba ya mipira ambayo mpira wake uliopandwa miaka ya 70 umezeeka, huku zaidi ya hekta 1,500 hazijapandwa.

Katika mwaka wa fedha wa 2017/18, Wizara ilieleza imetenga Sh bilioni 1.85 kwa ajili ya kufufua kiwanda hicho na mradi wa Lake Natron/Engaruka Soda Ash, ikiwa ni asilimia tano ya bajeti ya maendeleo ya Sh bil 40.

Kiwango hicho kinaelezwa kuwa ni wastani wa Sh milioni 925 kwa kila eneo, kiasi ambacho tunathubutu kusema ni kidogo na kinazima ndoto ya kufufua viwanda.

Tunadhani ifike mahali kama tumedhamiria kwa dhati kuwa na Tanzania yenye viwanda, Serikali iamue kufunga mkanda kama ilivyofanya katika maeneo mengine, kufufua viwanda ambavyo si tu vilitujengea heshima, bali ambavyo vitatuletea tija katika uchumi wa nchi yetu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here