RAY VANNY NI MSHINDI HATA ASIPOSHINDA TUZO

0
859

NA MWANDISHI WETU

SIWEZI kusema ni bahati, ila ni maandalizi, yanapofanyika kwa wakati ndiyo tunapata matokeo mazuri kama haya ya mwenendo mzima wa muziki wa msanii, Ray Vanny kutoka lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB).

Milango ya mafanikio kwake kwenye muziki imeendelea kufunguka kadri siku zinavyozidi kwenda. Kwa muda mfupi ambao amefanikiwa kutoa nyimbo zake chini ya lebo hiyo, Ray Vanny amefaulu kwa kiasi kikubwa kutumia vyema fursa pale zinapojitokeza.

Kama nilivyosema hapo awali kuwa, mafanikio aliyonayo kijana huyu ni maandalizi ambayo yalifanyika kwa wakati, ndiyo maana kwa muda mfupi ameweza kupata nafasi ya kushiriki kwenye msimu mpya wa Coke Studio huko Kenya.

Nafasi hiyo ilimpa wasaa wa kufanya kazi na staa wa muziki wa RnB Marekani, Jason Derulo, ambaye ametokea kuvutiwa na uwezo wa Ray Vanny kiasi kwamba ametoa mwaliko kwa msanii huyo kumtembelea nyumbani kwake ikiwezekana wafanye kazi.

Nadhani amekuwa akiutumia vizuri ushauri kutoka kwenye menejimenti yake. Hivi sasa amefanikiwa kuingia kwenye tuzo kubwa duniani zinazoandaliwa na kituo cha runinga cha Black Entertainment Television (BET), zinazotolewa kesho huko Los Angeles, Marekani.

Kabla ya kutolewa kwa tuzo hizo, leo hii amepata nafasi ya kutumbuiza kwenye sherehe za awali za tuzo hizo zinatazofanyika katika klabu ya usiku ya Sayers Club 1645 Wilcox, ambapo ataungana na wasanii wengine kama Stone Bway, Tekno Miles, Becca na Nasty C.

Mbali na kutumbuiza kwenye sherehe hiyo ya awali ya tuzo za BET, Ray Vanny ameingia kwenye tuzo hizo kama Viewer’s Choice: Best International Act. Watanzania tulikuwa na muda wa kutosha kuhakikisha kijana huyu anafanikiwa kutwaa tuzo hiyo kwa kumchagua kupitia kwenye kurasa za Instagram za @bet-Int na@bet-awards kwa kuandika #ipickrayvanny.

Katika tuzo hiyo anashindana na wasanii wengine kutoka kwenye mataifa kama Australia, Jamaica, Nigeria, Korea na Ghana. Huu ni mwanzo mzuri kwa Ray Vanny kufanikiwa kimuziki, ukifananisha muda alioingia kwenye muziki na mafanikio aliyoyapata yanaonyesha wazi nyota yake inavyozidi kung’aa.

Nimalize kwa kusema kuwa, katika mashindano kuna kushinda na kushindwa, hivyo hata kama Ray Vanny hatashinda tuzo hii, kwetu atakuwa mshindi kwa kuwa ni mwanzo na kwa Afrika Mashariki yeye ni msanii pekee kutajwa kwenye BET 2017.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here