25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

KAIMU JAJI MKUU TUONDOLEE HOFU HII 

1-64WIKI iliyopita Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande alimaliza muda wake wa kuongoza mahakama.

Rais Dk. John Magufuli amemteua Jaji Prof. Juma kushika nafasi hiyo kwa kukaimu. Pamoja na kukaimishwa kazi hiyo tunapenda kumpa hongera na pongezi kwani hii ni fursa kubwa na njema.

Tutajua kazi hiyo ni kubwa na ya heshima  kwa Taifa kwani ni ya kuusimamia mmoja wa mhimili mikuu mitatu ya dola yaani Mahakama, Bunge na Serikali.

Pia tunapenda kumpongeza Jaji mkuu aliyemaliza muda wake  kwa kuhitimisha kazi yake vyema.Tunajua yapo mambo mengi aliyoyafanya katika kuhakikisha haki zinapatikana. Mfano alisimamia masuala ya utawala wa mahakama kwa weledi mkubwa  hasa suala la uharakishwaji wa kesi na kupunguzwa kwa mrundikano wa kesi.

Tunaposema kuwa mahakama ni mhimili wa dola kuna wakati suala hili halieleweki sana kwani pale watu wanapoona Rais akimteua Jaji Mkuu wanadhani ndiye msimamizi wa mahakama na kuwa ana uwezo wa kutoa maelekezo kwa mahakama.

Lakini pia Rais huapishwa na Jaji Mkuu bila Jaji Mkuu kuwa ndiye msimamizi wa Rais. Rais pia huteua baadhi ya wabunge lakini akishawateua wao huwa katika  mhimili wa Bunge na huapishwa kwa taratibu za Bunge na hata kuondoka kwake mbunge huwa ni kwa taratibu za Bunge kama zilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ya Mwaka 1977 na hususani ibara ya  67.

Tunapompongeza Kaimu Jaji Mkuu mpya tukiwa na matazamio kwake kama ambavyo kiongozi mpya yeyote afikapo huwa kuna yale yanayotarajiwa na si kwa kuwa aliyekuwapo hakufanya ila ni katika uendelevu na matarajio ya pale yalipofikiwa wakati wa uongozi wa awali.

Tunaamini kuwa kama tulivyomsikia mwenyewe  Jaji Profesa  Juma akijieleza  baada ya kuapishwa  suala la upatikanaji wa haki ndio kipaumbele. Mahakama  ndicho chombo cha upatikanaji haki kama ilivyo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 107 (A) ambayo inaeleza kuwa  “Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamuhuri  ya Muungano itakuwa ni Mahakama”.

Maana ya kifungu hiki ni kuwa panapokuwa na tatizo lolote la upatikanaji wa haki mahali pa kutafuta haki ni mahakamani. Kila mtu anapaswa kujua kuwa mahakama zipo na kazi yake ni kutoa haki.

Mahakama yenyewe kupitia mahakimu na majaji nao wanafahamu hivi na pia kama tulivyomwona Kaimu Jaji Mkuu akitoa kiapo chake mbele ya Rais, mahakama ina wajibu mkubwa wa kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria na kufuata kanuni zilizoainishwa kikatiba katika ibara 107(A) (2) vifungu vidogo (a) hadi  (e) .

Katika Ibara 107 (B) suala la Uhuru wa Mahakama limeelezwa vizuri sana kuwa mahakama zote zitakuwa huru na zitazingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi.

Maneno haya ya Katiba ni muhimu sana kwa mahakama zetu kwani watu wamekuwa wakipata wasiwasi sana wanapoona Jaji anateuliwa na Rais na hivyo kudhani kuwa Jaji kama huyu ataweza kweli kuwa huru mbele ya Rais pale ambapo  anapobidi kutoa haki upande mmoja akiwamo au yakiwamo maslahi ya Rais au Serikali yake?

Lakini tuna ushahidi kuwa mahakama ina uwezo na mamlaka ya kufanya haki kwa kusimamia uhuru uliopo kikatiba na tunaamini kuwa hata Jaji Mkuu mpya huyu anafahamu hivyo kwa sababu amekuwapo mahakamani kwa muda sasa na amekuwa akifanya hivyo.

Tunachojiangaliza ni ule msemo usemao haki inabidi si itendeke tu bali ionekane kuwa imetendeka. Kuna wakati ambapo mahakama huweza kufanya uamuzi wake na ikaona imesimamia haki lakini kunaweza kuwa na viashiria vinavyoweza kuonyesha shaka iwapo kweli haki imetendeka.

Mfano ni pale mahakama zinavyoweza kufuata zaidi taratibu za kisheria na kuacha kabisa kuangalia haki ya msingi aliyonayo mtu. Mfano mzuri ni pale shauri la mtu ambaye amedhulumiwa mali yake linapotupwa kwa vile sahihi imewekwa sehemu ambapo haikustahili au jina la Jaji limekosewa au madai yamepelekwa kwa kutumia karatasi isiyokubalika.

Ni kweli kabisa kukosea jina la Jaji ni tatizo lakini haki ya mtu ikikosekana kwa kosa hilo ambalo huweza kurekebishwa hapo haki haiwezi kusemekana imetendeka na ikaonekana kuwa kweli imetendeka.

Tunajua kuwa Jaji Profesa anachanganya kazi ya ujaji na taaluma ya sheria kwani yeye pia amekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu akifundisha sheria. Ipo mifano mizuri sana ya majaji hasa wa Mahakama Kuu walioweza kuondokana na vifungo vya taratibu za kisheria ili kuhakikisha haki kwa mtu aliyefika mbele yao inatimizwa. Tuna mifano kama Hayati Jaji Mwalusanya na Lugakingira kwa kuwataja kwa uchache.

Hivi karibuni nimeulizwa maswali mengi sana kuhusu yanayoendelea mahakamani kwa baadhi ya kesi zinazowagusa viongozi wa vyama vya siasa na hususani vya upinzani.

Sijaweza kuwa na majibu kwani sijapata hukumu au hata mienendo ya kesi hizo. Lakini pia wengi wa hao wanaoulizwa wana mawakili na hivyo nikidhani kuwa uwepo wa mawakili mahakamani wakiwa ni maafisa wa mahakama na wenye uwezo wa kushauri Majaji na mahakimu basi kila jambo litaenda sawa.

Lakini baada ya kuulizwa maswali hayo imebidi nami nijifikirishe bila kuingilia uhuru wa mahakama na kudhani hata mahakama za juu na hasa Jaji Mkuu naye huwa na nafasi ya kuweza kushughulikia masuala yanayoonekana kuwa na hali ya utata au sintofahamu.

Watu wengi wameniuliza ni kwanini Gobless Lema Mbunge wa Arusha Mjini  yuko rumande kwa muda mrefu hivyo wakati kosa analoshtakiwa nalo lina dhamana? Wengine wamehoji iwapo kosa hilo kweli ni uchochezi na maana ya uchochezi ni nini?

Watu waliokuwa wanauliza ni wale ambao si wanasheria na hawaelewi kabisa inakuwaje hivyo? Pia nimehojiana na baadhi ya wanasheria na hasa wale wanaopata nafasi ya kusimamia kesi mahakamani kama mawakili, hadi sasa sijawa na jibu la uhakika.

Na iwapo kitu kinachosababisha  kukosewa dhamana kwa Mheshimiwa huyu ni  mabishano ya kisheria, nadhani haki aliyonayo ya dhamana ni kubwa kuliko mabishano ya kisheria .

Kesi nyingine ni ile ya watu wajulikanao kama wana Uamsho kutoka huko Zanzibar, hapa pia nilipata maswali ya aina hiyo hiyo, Na hivi karibuni suala la Mbunge wa Kilombero ambaye naye amefungwa miezi sita kwa kosa ambalo lilikuwa na uwezekano wa kupewa faini.

Wanaohoji nao walitaka kujua kwa mtu ambaye ana wajibu mkubwa kama huu pamoja na kuwa hayuko juu ya sheria lakini pale ambapo sheria yenyewe imeweka huo mwanya iweje apewe adhabu itakayomtoa kabisa katika wajibu na jukumu lake hilo.

Hapa napo sikuwa na jibu kwa vile pia sikuwa na hiyo nakala ya kuhukumu na hata mwenendo wa kesi. Ila kusikiliza maswali haya ya watu wasio wanasheria yanagusa zaidi haki kuliko sheria na tujuavyo haki ndio hubeba sheria.

Tunategemea Kaimu Jaji Mkuu ataweza kuwa na wakati wa kuangalia mambo mbalimbali yanayoonekana kutokutenda haki au kutoonekana kutenda haki na kuyawekea misimamo kwa kuitazama haki. Kwa jinsi Katiba ilivyoipa mahakama uhuru sidhani kabisa kuwa masuala kama haya yanayotafsiriwa kuwa ya kisiasa yataionyesha mahakama kuwa inaongozwa na siasa bali inasimamia Katiba na sheria.

Tunamtakia Jaji Mkuu Profesa Juma kila la heri katika kazi yake hii kuu.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles