27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Kailima ahimiza ushirikiano kati ya Mawakili wa Serikali na na polisi

Na Ashura Kazinja, Morogoro

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhan Kailima, amewataka Mawakili wa Serikali nchini kuendeleza ushirikiano na Jeshi la polisi ili kuimarisha utendaji kazi wao kwa kufuatilia, kushughulikia na kumaliza kesi kwa wakati.

Kailima ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya  makosa ya mtandao ya kuwajengea uwezo mawakili  wa serikali toka mikoa mbalimbali nchini, yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Alisema kuwa ushirikiano kati ya mawakili na jeshi la polisi ni nyenzo kuu ya kutatua changamoto ya ucheleweshaji wa kesi  na hivyo kuondoa malalamiko toka kwa wananchi yakiwemo malalamiko ya kuchelewa kupata dhamana na upelelezi kutokamilika kwa wakati.

“Naomba muendeleze ushirikiano na jeshi la polisi, kwa sababu jeshi la polisi ndio hatua zote za awali za uchakataji wa swala la mashtaka wanafanya wao wanaandika wanapeleka pale, nimekuwa nikifanya ziara kwenye vituo vya polisi, unamkuta mkuu wa kituo pale au mkuu wa upelelezi wa wilaya mkoa, nikimuuliza kwa nini hawa hawajapata dhamana, anajibu hawa makosa yao hawawezi kupata dhamana, kwa sababu gani, faili lipo kwa DDP, ndio wanaishia hapo,’’ amesema Kailima.

Aidha, amewasihi mawakili hao wa serikali kujitahidi kupambana na kumaliza kabisa changamoto ya ucheleweshaji wa kesi kutokana na upelelezi kuchukua muda mrefu, kwani wana mamlaka na nafasi kubwa ya kutatua changamoto hiyo na nyingine zinazofanana na hiyo.

“kuna changamoto ya upelelezi kuchukua muda mrefu, yapo malalamiko mengi tu kuhusu upelelezi kuchukua muda mrefu, mmepewa hati idhini na DDP ambayo mna mamlaka na nafasi kubwa ya kutatua changamoto hii kupitia utekelezaji wa majukumu yenu,’’ amesema.

Akizungumzia swala la rushwa Kailima alisema kuwa ni mbaya sana kwani inapunguza hadhi na heshima ya mtu, na kuwasisitiza mawakili hao kuepuka na kukemea vikali rushwa katika majukumu yao ya kila siku, kwani rushwa ina laana kubwa inayotafuna mtu mpaka kizazi chake na kuharibu baraka ya familia.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali Mkuu, Veronika Matikila, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya makosa ya mtandao Monica Mbogo, alisema kwamba mafunzo hayo yanalenga kuwajengea ufahamu mawakili hao wa namna bora ya kuratibu upelelezi wa makosa ya mtandao na yanayo fanana na hayo, pamoja na matumizi ya ushahidi wa kidijitali.

Alisema kuwa mawakili hao watajengewa uwezo kwenye maeneo mbalimbali muhimu ambayo kimsingi hutumika kama zana za kupambana na uhalifu wa kimtandao, na kwamba mojawapo ya maeneo hayo ni elimu juu ya utaifishaji mali ambazo ni mazao ya uhalifu wa makosa hayo, na namna bora ya kutumia mahusiano ya kitaifa kwenye ukusanyaji wa ushahidi uliovuka mipaka na urejeshwaji wa  wahalifu kwenye eneo walilotenda kosa.

Nae Mkurugeni Mkuu wa Mashtaka(DPP) Silvesta Mwakitalu alisema maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari inaleta mambo mazuri lakini ndani yake pia kuna uhalifu, kwa watu wachache kutumia maendeleo hayo vibaya, ambapo mabenki na taasisi zingine za kifedha zimekuwa zikikumbana na changamoto hiyo.

Hata hivyo amewaasa washiriki hao kutumia vyema mafunzo hayo kwa kubadilisha utendaji kazi wao, kwa kushirikiana na kuhamishia ujuzi huo kwa wenzao ili kuboresha kazi zao kwa maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles