25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kadi za kieletroniki kurahisha maendeleo kwa jamii

Profesa Faustine Kamuzora
Profesa Faustine Kamuzora

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

KATIKA miaka ya karibuni, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kukaribisha na kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika shughuli za sekta ya fedha nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Faustine Kamuzora, anasema serikali imechukua uamuzi huo baada ya kuonekana kwa mafanikio makubwa katika matumizi ya teknolojia katika kufanikisha upatikanaji wa huduma mbalimbali.

Profesa Kamuzora ameeleza mtazamo huo wa Serikali wakati wa maonyesho ya benki na taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta ya fedha, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, hivi karibuni.

Wito huo wa Profesa Kamuzora umekuja wakati muafaka kwa kuwa sasa dunia inakwenda kasi katika masuala ya sayansi na teknolojia, huku mataifa yaliyoendelea yakiona asilimia kubwa ya wananchi wake wakitumia njia wezeshi za teknolojia ili kupata huduma za kifedha mahali popote, wakati wote na hivyo kutohitajika kutembea na fedha mifukoni.

Miongoni mwa kampuni zilizoshiriki maonyesho hayo ni DataVision International, ambayo imebuni mfumo wa kutengeneza kadi papo hapo na hivyo kuziwezesha taasisi kutoa kadi za aina tofauti zikiwemo za kielektroniki zinazomwezesha mteja kutoa fedha katika mashine za kutolea fedha (ATM), vitambulisho na kadi za huduma mbalimbali zikiwamo za manunuzi.

DataVision International wanazishauri taasisi hizo kutumia mfumo wa KadiPap kwani ni rahisi na salama katika kutengeneza kadi. Kwa kutumia mfumo huu taasisi mbalimbali zikiwamo za fedha zinakuwa na uwezo wa kumfungulia mteja akaunti na kumtengenezea kadi yake papo hapo hivyo kuondoa usumbufu kwa wateja.

“Itakumbukwa huko nyuma baada ya kujiunga na huduma ya benki mteja alilazimika kusubiri kwa zaidi ya siku saba kupata kadi ya ATM; lakini mfumo huu unaondoa kabisa usumbufu kwani unawezesha kadi kutengenezwa wakati huo huo na kuwa tayari kwa matumizi,” anasema Meneja Bidhaa wa DataVision International, MacLean Mwaijonga.

Mwaijonga anaamini kuwa itafika siku Watanzania watatembea bila fedha taslimu mifukoni; hata hivyo ili kufikia hali hii ni lazima kuwapo na kasi ya kutengeneza mifumo ya kuwezesha utumiaji wa kadi za kulipia huduma mbalimbali.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukitengeneza kadi mbalimbali zikiwamo za vitambulisho, kufungulia milango au mageti pamoja na zile zinazotumika kuwezesha huduma za kifedha.

“Mfumo wa KadiPap unaweza kutumika na benki, vikundi vya kuweka na kukopa (Saccos) na taasisi zingine za kifedha ambazo zinawapa wateja au wanachama wao kadi. Mfumo huu unaweza kutumika kwenye taasisi mbalimbali pia kama za kielimu, kiafya, mifuko ya bima na kadhalika,” anasema.

DataVision International imetengeneza mfumo unaotumia kadi za kielektoniki ili kuweza kusimamia na kuwatambua wafanyakazi wa Kampuni ya madini ya Acacia kwa ajili ya kupata huduma ya chakula.

“Kabla ya mfumo wetu ambao unaitwa ‘Canteen Information Management System’, Acacia walikuwa wakitumia mfumo wa kutoa karatasi ambazo wakati mwingine ulikuwa unatumika vibaya na wafanyakazi wasio waaminifu na hivyo kuiingiza hasara kampuni kwa kutoa huduma ya chakula hata kwa watu wasiohusika.

“Baada ya kuanza kutumia mfumo unaotumia kadi Acacia imeweza kuondokana na changamoto za kuwatambua wafanyakazi, kufahamu wamekula nini na kutunza kumbumkumbu sahihi za malipo kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi wanaotoa huduma ya chakula migodini,” anasema.

Pamoja na ubunifu ambao kampuni ya DataVision International imekuwa inaufanya katika kuleta ufanisi wa upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa kutumia kadi za kieletroniki.

Mwaijonga anasema bado kasi ya ukuaji wa matumizi ya kadi nchini ni ndogo ikilinganishwa na nchi zilizoendelea na hali hii inachangiwa na kukosekana kwa uelewa wa huduma hizo; hivyo elimu zaidi inahitajika kutolewa kwa wananchi.

Huduma za kadi kwa ajili ya malipo zina manufaa mengi kwa watumiaji pamoja na taasisi ikiwamo kupunguza muda wa kutoa/kupata huduma, usalama kwa kuwezesha kufanya utambuzi,  kupunguza gharama za kutoa huduma kwani kwa njia ya kadi na endapo ikiunganishwa na mawasiliano ya simu mhusika anaweza kutoa/kupata huduma wakati wowote.

Pamoja na kwamba bado Watanzania wengi wana mazoea ya kutumia fedha taslimu katika kulipia huduma hali inayowalazimu kutembea na fedha nyingi, changamoto za usalama zinaweza kusaidia kuwafanya waanze kugeukia matumizi ya mifumo ya kieletroniki.

“Ni kweli mabadiliko yanachukua muda na hasa yale yanayohusu fedha. Hata mimi wakati mfumo wa kutumia simu za mkononi kutuma na kupokea fedha ulipoingia nchini nilikuwa nina hofu. Hata hivyo, kadiri siku zilivyokwenda nikaanza kuzoea na kuona namna ilivyo rahisi na salama.

“Hivyo nawaasa Watanzania wenzangu kuwa sehemu ya mabadiliko haya, mtu akijaribu ataona utofauti.  Kwa sababu mtu anayebeba fedha nyingi daima ana wasiwasi. Lakini mtu anaweza kubeba kadi yenye zaidi ya Sh milioni 100 bila mtu wa jirani kujua, na kadi hiyo inamwezesha kufanya huduma yoyote kwa kugusisha tu kwenye mashine,”anasema

Naye Meneja Masoko na Uhusiano wa DataVision International, Teddy Qirtu, anatoa wito kwa vikundi vya Vicoba, Saccos na taasisi zingine za fedha kujiunga katika mfumo wa kadi ya kieletroniki uliotengenezwa na kampuni yake ili kuepuka madhara yatakayotokea wakati wa kutembea na fedha nyingi kwa wakati mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles