23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mambo Yanayoweza kugusa moyo wa mwanamke – 3

Usiri ni dalili ya kutokuwa mwaminifu, mwanamke hupenda kujua mambo muhimu anayofanya mwenzi wake.
Usiri ni dalili ya kutokuwa mwaminifu, mwanamke hupenda kujua mambo muhimu anayofanya mwenzi wake.

Na Christian Bwaya,

KWA wiki mbili sasa tumekuwa tukijadili mahitaji muhimu ya kisaikolojia kwa mwanamke. Tumeona kuwa mwanamke anahitaji kusikia lugha ya mapenzi kwa mwenzi wake. Kadhalika, tuliona mwanamke anatamani kuwa na uhakika wa nafasi ya kwanza kwa mwenzi wake.

Pia tumefahamu kuwa mwanamke anatamani kuwa na mtu anayeweza kuelewa hisia zake kwa usahihi. Na ili kuelewa hisia zake unahitaji kuwa msikivu zaidi ya kufafanua kile anachojaribu kukieleza kwako.

Mwanamke anapokutana na changamoto kazini kwa mfano, anapoudhiwa na watu wengine, anapohitafiana na majirani, anatamani mwenzi wake awe mtu wa kwanza kusimama upande wake na kuonesha kumwelewa. Ukiweza kuwa msikivu wa hisia za mwanamke unamfanya akuamini kwa alama nyingi kwa sababu umemwongezea hali ya kujiamini kuwa anaye mtu wa karibu anayemwelewa.

Hapa tunajadili mahitaji mengine mawili ya mwanamke unayohitaji kujifunza kuyaelewa na kuyafanyia kazi kama kweli unayo nia ya kugusa moyo wa mwenzi wako.

Uwazi wa mambo na kuambiwa ukweli

Tofauti nyingine ya mwanamke na mwanamume ni namna wawili hawa wanavyouchukulia uwazi. Tulishaona kuwa mwanamume anapenda faragha na usiri. Mara nyingi usiri huwa ni njia ya kulinda hadhi yake. Kwamba kutokutabirika wala kujulikana anafanya nini hasa ni namna ya kujihakikishia mamlaka yasiyohojiwa na mwanamke.

Lakini katika macho ya mwanamke, usiri na faragha ni dalili ya kutokuwa mwaminifu. Sababu ni kuwa mwanamke anatamani zisiwepo siri zozote asizozijua katika kila kila kona ya maisha ya mume wake. Kujua mambo ya muhimu anayoyafanya mume wake kunamhakikisha kuwa ni kweli mume wake amempa nafasi ya kwanza.

Ikiwa unataka kuugusa moyo wa mke wako jitahidi kuaminika kwa kufanya mambo yako kwa uwazi kadiri unavyoweza. Mwambie unakokwenda, mwambie uliko, mshirikishe mipango yako, mshirikishe siri zako usizoweza kumwambia mtu mwingine. Ukifanya hivyo atakuamini na hatakuwa na sababu ya kukupeleleza.

Sambamba na uwazi kuwa mkweli. Jenga mazoea ya kusema mambo yalivyo bila kulazimika kutumia uongo kuficha yale usiyopenda yafahamike. Mwanamke anapogundua kuwa unayo tabia ya kusema uongo, ujumbe anaoupata ni kuwa wewe si mwaminifu. Mwanamke asipokuamini hawezi kukuheshimu kama unavyotamani.

Najua wanaume wengi hujitetea kuwa uwazi na ukweli kwa mwanamke ni jambo lisilowezekana. Sababu wanayoitoa ni kuwa wanawake wenyewe hawaaminiki. Ingawa upo ukweli kuwa wapo wanawake wanaoweka wenyewe mazingira ya kufichwa mambo ya muhimu na wenzi wao, hiyo haiondoi ukweli mwingine kuwa mahusiano ya karibu kama ya ndoa, hayawezi kukamilika bila kuheshimiwa kwa misingi ya ukweli na uwazi.

Kusifiwa kwa ‘uanamke’ wake

Yapo masuala ambayo kwa mwanamke yanabeba wajihi (utambulisho) wake. Kwa wengi ‘uanamke’ ni pamoja na vile anavyovutia kimwonekano na kimaumbile, namna anavyotekeleza majukumu ya ndani  kama mwanamke na haiba yake kwa ujumla. Mwanamume anayetaka kugusa moyo wa mke wake ana wajibu wa kutambua na kuyasifia maeneo hayo.

Kwa mfano, mwanamke hutumia muda mwingi kujiweka katika mwonekano unaovutia. Anakwenda saluni kwa masaa kadhaa tofauti na mwanamume. Mara nyingi anapojipamba lengo ni kumvutia mume wake hivyo msifie.

Jitahidi kugundua mabadiliko anayoyafanya katika mwonekano wake na msifie kwa dhati. Unapofanya hivyo, unaongeza hali ya kujiamini kwake na anapojiamini atakuwa na nguvu ya kukupa heshima unayoihitaji kutoka kwake.

Itaendelea…

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com

0754 870 815

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles