28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Jumuiya ya Wazazi CCM yahimiza utunzaji mazingira

Mwandishi Wetu – Geita

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kupitia Jumuiya ya Wazazi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu UVCCM Tanzania Bara, Galila Wabanh’u amewataka Watanzania kuwa na utamaduni wa kutunza mazingira.

Hayo aliyasema jana wilayani Mbogwe mkoani Geita, alipokuwa akishiriki upandaji miti katika shamba la Jumuiya ya Wazazi ya CCM, lililopo Kata ya Nyasato ambako walipanda miche 500 ya miti.

“Kwa niaba ya Jumuiya ya Wazazi, niseme mazingira ni mali. Tupende kuwafunza watoto wetu umuhimu wa kuyatunza na kuyahifadhi ikiwemo upandaji miti. Sisi pia tujenge tabia ya kupanda miti kila tunaposherehekea kumbukizi muhimu za maisha yetu kama siku ya kuzaliwa. Niwaombe miti hii takribani 500 itunzwe ili ilete maana ya kile tulichokifanya leo (jana).

“Kwa sasa kasi ya ukataji miti ni kubwa, hali inayopelekea mabadiliko makubwa ya tabianchi ambayo huchochea ukame ambao hupelekea vyanzo vya maji kukauka na hata mvua kupotea hivyo kilimo na ufugaji kuwa katika tabu. “Niwaombe wana CCM na Watanzania wote msimu huu wa mvua tupande na kutunza miti angalau mitatu kila mmoja ili kukabiliana na mabadiliko haya ya tabianchi,” alisema Galila.

Katika hatua nyingine, Galila alipokea shukrani za wanafunzi, walimu, wazazi na walezi wa Shule ya Msingi Mlange kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, kwa Serikali yake kusaidia katika ujenzi wa madarasa na kuwafanya wanafunzi wao kutosomea nje.

Pamoja na shukrani hizo, waliomba kusaidiwa kukamilisha maboma matatu ya madarasa ili kukidhi uhitaji walionao kwa sasa.

Katika ziara hiyo, Galila aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi aliyepewa nafasi kwa niaba ya Jumuiya ya Wazazi kukabidhi vitabu takribani 1,500 vya masomo ya hisabati, kiingereza, kiswahili, maarifa ya jamii na sayansi kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Baada ya kukabidhi vitabu hivyo, aliwaasa wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii, kuvitumia vizuri vitabu hivyo, wamtangulize Mungu katika masomo yao, kuwa wenye heshima na utii kwa wazazi, walezi na walimu ili wafanikiwe kimasomo.

“Nawaomba msome kwa bidii, wasikilizeni wazazi, walezi na walimu wenu na kumtanguliza Mungu katika masomo yenu mtafanikiwa.

“Vitabu hivi tulivyowakabidhi leo (jana) ni ishara kwamba Rais Magufuli anathamini elimu na anawapenda, msimwangushe, vitumieni vizuri na mvitunze,” alisema Mkupasi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles