28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Lugola akaliwa kooni bungeni

Ramadhan Hassan – Dodoma

IKIWA ni siku chache tangu Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, baadhi ya wabunge wameonekana kumkalia kooni mbunge huyo wa Mwibara.

Lugola juzi alikaliwa kooni kutokana na kauli zake alizotoa bungeni wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alipokuwa akijibu hoja za Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu mkataba tata wa ununuzi wa sare za polisi.

Wakati huo, alidai kwamba atavua nguo iwapo itaonekana kwamba hakuna sare za Jeshi la Polisi zilizonunuliwa kama ambavyo ripoti ya CAG iliainisha.

Juzi jioni wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) Nagwenjwa Kaboyoka akihitimisha kwa kujibu hoja mbalimbali za wabunge mara baada ya asubuhi kuwasilisha taarifa ya kamati hiyo kwa mwaka 2019, ndipo alipoibua suala la Lugola.  

 “Tunataka kumtoa Mheshimiwa Rais asionekane ana ‘Double Standard’. Mimi nilikuwa nimesafiri, nilikuwa South Africa, nikapata taarifa kwamba wenzangu wameteuliwa Mambo ya Nje pamoja na Ulinzi na Usalama na wachache wa kamati yangu kwenda kuangalia zile sare za polisi (zilizoainishwa kwenye ripoti ya CAG).

“Wakati huo Mheshimiwa Zungu (Musa) ndio alikuwa Mwenyekiti wa Kamati hii (Ulinzi na Usalama), nikamwambia Zungu naenda kama nani na nikamwambia mimi kama naenda kukagua na kamati yangu ina maana tumekaa na CAG tumepitia zile nyaraka zote zilizotakiwa.

“Maana suala la CAG halikuwa tukazione ‘uniform’ (sare) kwa macho, ilikuwa tunaangalia namna ‘uniform’ zile zilivyonunuliwa. Je, huyo aliyepewa tenda alipatikanaje? ‘Uniform’ zililetwa kutoka wapi? Kiasi cha fedha ni ngapi? Baada ya hapo ndio CAG aende stoo akaangalie kuna nini.

“Kutokana na zile ripoti, aone ‘uniform’ ziliagizwa 100 je, zimekuja 100, viatu viliagizwa 10 je, vimekuja 10, kinyume cha hapo CAG hawezi kutoka akaangalie kitu ambacho hajui anaangalia nini.

“Kwa hiyo kulikuwa na ‘disconcertion’ ambayo mheshimiwa Kangi Lugola ‘ali-mislead’ Bunge kusema atavua nguo kama ‘uniform’ hazipo, ina maana hasomi hata taratibu,” alisema Kaboyoka.

Wakati Kaboyoka akiendelea kuzungumza, Naibu Spika Tulia Ackson aliyekuwa akiongoza kikao hicho, alimkatiza na kumweleza kuwa ‘ngoja tuongozane vizuri.’

“Wewe hapo sasa hivi unapozungumza ni kana kwamba nawe ni mchangiaji, wewe ni mtu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ambaye umekasimiwa madaraka ili uje ujibu hoja za wabunge na humpi mtu mwingine hoja, na baada ya kuzungumza wewe maazimio uliyotuletea, Bunge litahojiwa.

“Kama unatupeleka kwenye hoja nyingine wakati wewe ndio ulieleta taarifa hapa ndani, utakuwa unaliongoza Bunge sehemu ambayo sio, kwa sababu wewe unapaswa kuzijibu hoja za wabunge na sio kuuliza, hakuna mtu wa kukujibu, Serikali katika hoja hii wao ni wachangiaji kama wachangiaji wengine.

“Sasa ukija na wewe unauliza maswali, sasa nani ambaye atakujibu hayo maswali na wewe ndio hoja yako wewe, kwahiyo hoja zote zilizoletwa na wabunge wewe ndio unajibu,” alisema Dk. Tulia.

Baada ya maelezo hayo, Kaboyoka alijibu; “sawa sawa mheshimiwa.”

 Dk. Tulia aliendelea kusema; “Kama kuna hoja kwenye kamati hujazimaliza, hilo ni la kwako na Serikali haiwezi kulijibu hilo, hata maswali unayouliza nilikuwa nakuangalia unaelekea wapi, yote ni ya kwako utujibu kama Bunge.”

Kaboyoka alijibu; “Nakushukuru sana kwa mwongozo wako na hapo ndio nilipokuwa nafikia, hili nitalitaja huko kwamba nitalifanyia kazi huko, umenieleza vizuri na nimekuelewa.”

Dk. Tulia aliendelea; “Mwenyekiti nisikilize kwenye maazimio ya kwenye kitabu chako, hayo unayotaka kuyaleta mimi sina hapa mezani, waheshimiwa wabunge tufuate kanuni zetu ili kama unataka kuleta mabadiliko kwenye maazimio lazima niwe nayo hapa mezani.”

Kaboyoka alijibu: “Sawa nakuelewa sana, nilitaka nitoe tu ili kwamba Rais asionekane ana ‘double standard’ ambayo inawezekana hakupewa.”

Wakati mabishano hayo yakiendelea, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliomba mwongozo kwa Naibu Spika lakini alimkatalia.

“Hakuna mwongozo akiwa mtu anazungumza, wewe unajua kanuni na nitakuruhusu uusome, umesema mwongozo, hakuna mwongozo mtu akiwa anazungumza, naomba ukae,” alisema Dk. Tulia.

Mdee aliendelea; “Kuhusu utaratibu Mheshimiwa Naibu Spika.” Lakini pia Dk. Tulia alimkatalia.

Mara baada ya mvutano huo mfupi, Kaboyoka aliendelea kujibu baadhi ya hoja za wabunge na baada ya kutoa hoja na Naibu Spika kuwauliza wabunge ambao waliipitisha, Mdee alisimama tena na kumwomba Naibu Spika akitaka iundwe kamati teule ya kushughulikia ufisadi katika sare za Polisi.

Kabla ya Mdee kutoa hoja yake, alitakiwa kueleza kanuni anayotumia na alitaja kanuni ya 120 (1) (2).

Mdee alisema; “katika taarifa ya PAC imeonyesha ni namna gani kuna mgawanyiko kwenye hoja zinazohusiana na masuala ya kifisadi, mfano Jeshi la Polisi pale ambapo kamati inatoa taarifa uchunguzi ufanyike Serikali wamekuwa ni wazito kufanya uchunguzi.

“Hili limethibitishwa wakati Mwenyekiti wa PAC anaelezea mkataba wa E-Passport (paspoti za kielektroniki) na mradi wa ‘uniform’ za polisi, usanii uliofanywa na wizara, lakini ameonekana anazuiwa kuendelea wakati hoja ilizungumzwa kwa upana na Msigwa (Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa).

“Sasa kwa kuwa Bunge lina mamlaka ya kuunda kamati teule pale kunapokuwa na utata na kwa kuwa Kamati ya Bunge imeonyesha kuna shida, ninaomba nitoe taarifa hii ili nifanye ombi la kuomba niandike ombi hili kimaandishi ili Bunge liunde kamati teule kisha tufukunyue huu ufisadi unaofichwa, Mheshimiwa Naibu Spika nadhani umenielewa.”

Akijimjibu Mdee, Naibu Spika alisema hawezi kuruhusu kuundwa kamati teule kwa sababu ni lazima jambo hilo liwe limefika kwa utaratibu unaotakiwa.

“Kilichotokea ni cha ajabu, Mwenyekiti anaanzisha hoja nyingine wakati wa kuhitimisha hoja yake wakati yeye ndio kazi yake kujibu, sio kuja kutuanzishia hoja, lakini anakuwa kama anashtaki.

“Ili kamati teule iundwe, ni lazima hilo jambo liwe limefika kwa utaratibu unaotakiwa, kwa namna hiyo maelezo ya Mheshimiwa Halima yametoka kwenye yale niliyokuwa nikimrekebisha Mwenyekiti wa Kamati.

“Nadhani tumeelewana vizuri, kwa namna hiyo, hiyo hoja tuelewane vizuri, kwa kuwa hoja haijaja hapa, hiyo hoja haiwezi kutumika hapa,” alisema Dk. Tulia.

Januari 23 mwaka huu, wakati Rais Dk. John Magufuli akizindua nyumba za makazi ya askari Magereza, Ukonga, Dar es Salaam, alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola.

Rais Magufuli alieleza sababu za kumng’oa Lugola kuwa ni viongozi wa wizara yake walitia saini makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Euro milioni 408.5 (sawa na zaidi ya Sh trilioni 1) kutoka kampuni moja ya nje bila kufuata sheria.

“Kazi ya uongozi saa nyingine ni ngumu sana, ni ngumu, tuna changamoto nyingi. Kama kuna wizara inanitesa ni Wizara ya Mambo ya Ndani, nataka muelewe inanitesa sana.

“Tangu tumeingia madarakani, kuna tume nyingi zimeundwa kuchunguza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa miradi ya ovyo iliyokuwa ikifanyika, na mimi nilitegemea watu watakuwa wanajifunza.

“Kulikuwa na mkataba wa ovyo unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya Euro milioni 408.

“Umetayarishwa na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa Zimamoto, haujapangwa kwenye bajeti, haujapitishwa na Bunge.

“Wakati wa vikao na kampuni moja ya Romania, wahusika wa Tanzania walipokuwa wanakwenda kwenye majadiliano wanalipwa ‘seating allowance’ (posho ya vikao) ya Dola 800 (Sh 1,832,170) na hata tiketi za ndege walilipiwa.

“Yanayokwenda kununuliwa kule kwenye mkataba ni ya ovyo, ni ya ajabu, ukitaka kuuvunja, yale ambayo yameshaanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa,” alisema Rais Magufuli.

Pia alisema maofisa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliohusika kupitisha makubaliano hayo wajitafakari.

Maofisa hao wanadaiwa kupitisha makubaliano hayo wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Andelardus Kilangi alipofiwa na mkewe.

“Lugola nampenda sana, ni mwanafunzi wangu nimemfundisha Sengerema Sekondari, lakini kwenye hili hapana. Nilitegemea hata hapa sitamkuta.

“Nakueleza Lugola, Kamishna Jenerali (Thobias Andengenye) ninawashangaa kuona mko hapa, sitaki kuwa mnafiki, trilioni moja na zaidi mnasaini wakati sheria zote zinajulikana.

“Kwa hiyo mwanafunzi wangu Lugola nasema kwa dhati nakupenda sana, lakini kwenye hili hapana.

“Umenisifia sana hapa nakushukuru, lakini kwenye hili hapana, ni lazima niwe mkweli,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wapo wanaohusika kwenye wizara hiyo, hasa kitengo cha Zimamoto, hivyo akawataka wasaidizi wa Andengenye wajitathmini.

“Andengenye nampenda sana ni mchapakazi, umejenga nyumba mpaka Chato, lakini kwenye hili hapana, nilitegemea asiwepo hapa.

“Unakwenda Ulaya unasaini mradi ambao haujapitishwa hata na Bunge… ‘no’, nitaendelea kuwapenda, lakini kwenye ‘position’ hii ‘no’.

“Katibu Mkuu Mambo ya Ndani nampongeza sana kwa kuwajibika na hii imempa heshima, inawezekana hakuyafanya yeye, ninampongeza.

“Yule atakayekuwa anajikwaa iwe kwa makusudi au bahati mbaya, sasa ukianguka nenda ukajipange vizuri.

“Urafiki, upendo uko palepale lakini katika suala la kazi no way…that’s me, utawala wangu hapana nataka watu wafaidi kwelikweli,” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles