JPM, M7 WAISHUKIA ICC KUANZISHA UCHUNGUZI MGOGORO WA BURUNDI

0
730

Na MWANDISHI WETU-KAMPALA


RAIS Dk. John Magufuli, amesema uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) wa kumwagiza Mwendesha Mashtaka wake, Fatou Bensouda, kuanzisha uchunguzi dhidi ya mgogoro wa Burundi, unarudisha nyuma jitihada za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) za kuutatua mgogoro huo.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Magufuli alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati akiagana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ambaye naye alilaani uamuzi huo wa ICC kwa kusema kuwa unaingilia mambo ya ndani ya EAC.

Katika maelezo yake, Magufuli alisema ICC imechukua uamuzi huo wakati tayari EAC ikiwa imeanza jitihada za usuluhishi wa mgogoro huo kwa kuunda kamati maalumu ya kuushughulikia.

Alisema kamati ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi inaongozwa na Museveni na Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Pia alisema hali ya amani nchini Burundi si mbaya kama inavyotangazwa na tayari wakimbizi wengi wa nchi hiyo waliokuwa Tanzania wamerejea nchini kwao na wengine wanaendelea kurejea.

“Viongozi wanaosuluhisha mgogoro huo wamepanga kukutana Novemba 23, mwaka huu kwa lengo la kuendeleza mchakato wa kuutatua,” alisema.

Awali, kabla ya kumuaga Magufuli, Museveni alisema Majaji wa ICC wametoa uamuzi wa kumtaka Bensouda kuchunguza vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu vilivyotokea Burundi tangu ulipozuka mgogoro huo miaka miwili iliyopita.

Novemba 9, mwaka huu, ICC ilimwamrisha Bensouda kuanzisha uchunguzi kamili kuhusu madai ya uhalifu dhidi ya binadamu uliotokea Burundi.

Majaji walisema kwamba kuna sababu za kuchunguza uhalifu huo yakiwamo mauaji na mateso yaliyofanywa na Serikali pamoja na makundi yenye uhusiano na Serikali.

Wakati ICC ikifikia uamuzi huo, mwezi uliopita tayari Burundi imeshatangaza kujiondoa uanachama wake.

Serikali ya Burundi iliutaarifu Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu kufanya uamuzi huo tangu mwaka jana, ingawa ICC nayo iliweka bayana mpango wa kutathmini iwapo itachunguza ghasia za kisiasa zilizoibuka baada ya Rais Pierre Nkurunziza kusalia madarakani kwa awamu ya tatu licha ya kuwapo kwa kipindi cha mihula miwili kwa mujibu wa Katiba.

Inaelezwa kwamba, makundi ya haki za binadamu yanasema kuwa mamia ya watu waliuawa wakati wa ghasia zilizoibuka baada ya Nkurunziza kuamua kuwania muhula wa tatu mwaka juzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here