31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

DK. SLAA AZIDI KUFUNGUKA

 

Na ELIZABETH HOMBO


SIKU mbili baada ya gazeti la MTANZANIA kuripoti kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ameanza kufanya kazi katika duka kubwa (supermarket) huko nchini Canada, yeye mwenyewe amezidi kufunguka juu ya kazi yake hiyo mpya.

Dk. Slaa alimwambia mwandishi wa habari hizi juzi kuwa, analipwa Dola za Canada 10, ambazo ni sawa na Sh 17,684 kwa saa, kama mshauri wa mauzo wa Supermarket ya Costco ya nchini Canada, anakoishi hivi sasa.

Alisema mbali na kazi hiyo ya supermarket, anafanya kazi nyingine mbili tofauti, ambazo hakuweka bayana kiwango ambacho analipwa.

Jana MTANZANIA Jumapili liliwasiliana na Dk. Slaa kwa mara nyingine ili kufahamu kiwango anacholipwa katika kazi nyingine mbili za ushauri, mbali na ile ya supermarket, ambapo alikataa kuweka wazi.

“Nilikwambia nafanya consultancies (kazi za ushauri) mbalimbali, nadhani hukunielewa,” alisisitiza Dk. Slaa.

Alipoulizwa kama kazi yake ya supermarket na hizo nyingine za ushauri anazozifanya malipo yake yanazidi yale aliyokuwa akilipwa wakati akiwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa alisema pasipo kufafanua:

“Nadhani ukilinganisha mishahara ya Tanzania na Canada, unalinganisha Mlima Kilimanjaro na kichuguu”.

Akiielezea Supermarket ya Costco anakofanya kazi, Dk. Slaa alisema ni Kampuni ya Kimataifa inayomiliki msururu wa maduka makubwa (malls) ya Amerika ya Kaskazini.

“Wanaonunua kwenye malls zao ni wanachama tu, kwa mfano mimi ni executive member  na uanachama nalipia dola ya Canada 120 kwa mwaka (sawa na Sh  212,200),” alisema Dk. Slaa, ambaye alisisitiza kuwa, kazi anazozifanya zinamwezesha kumudu maisha ya Canada, ikiwa ni pamoja na kumiliki magari  ambayo kwa hapa nchini ni ya bei kali kama Jeep na Dodge.

Wakati Dk. Slaa akieleza hayo, kumbukumbu zinaonyesha kuwa, wakati anaondoka Chadema alikuwa akilipwa mshahara wa Sh milioni 13.8 kwa mwezi, kiwango ambacho kilitajwa kuwa ni kikubwa kuliko makatibu wakuu wa vyama vyote vya siasa katika nchi za Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa mchanganuo wa mshahara wake, ambao ulishawahi kunukuliwa kwenye vyombo vya habari miaka miwili nyuma, ni kwamba alikuwa analipwa na Chadema mshahara kwa mwezi wa Sh milioni 9.3, fedha ya usafiri Sh milioni mbili na fedha za matumizi ya ofisi Sh milioni 2.5.

Kama haitoshi, inadaiwa kwamba, Dk. Slaa alikuwa analipwa posho ya Sh milioni 1.5 katika kila kikao.

Ujira wa Dola ya Canada 10 (Sh 17,684.74) kwa saa anaolipwa sasa, endapo kazi hiyo ataifanya kwa saa nane kwa siku na kwa mwezi mzima, atakuwa anapokea Sh milioni 5.3.

Kiwango hicho kinaweza kuwa pungufu au kikubwa, hasa kutokana na ukweli kwamba, Dk. Slaa mwenyewe, licha ya kukiri kufanya kazi kwa mikono yake zaidi ya moja, lakini hakuweka wazi kiwango cha fedha anazolipwa kwenye kazi hizo nyingine.

Dk. Slaa, ambaye amepata kuwa Padri wa Kanisa Katoliki kabla ya kuingia kwenye siasa na kuwa mbunge, mgombea urais na katibu mkuu wa Chadema, aliliambia gazeti la MTANZANIA wiki hii kuwa, duka kubwa “supermarket” anayofanya kazi kwa sasa ina hadhi kama yalivyo maduka ya Nakumat, Shoppers na Imalaseko.

Katika maelezo yake kwa mwandishi wa habari hizi, Dk. Slaa alisema kuwa, kwa sasa anaishi kwa kazi ya mikono yake, kwani ili uweze kuishi Canada unahitaji kufanya kazi zaidi ya mbili hadi nne kwa siku.

“Niko ninafuatilia matukio Mutukula (ziara ta Rais Dk. Magufuli). Siku zote nimesema ninaishi kwa jasho na kazi ya mikono yangu. Canada ili uishi vizuri unahitaji kazi zaidi ya mbili au tatu mpaka nne. Hayo nimeweka wazi, sijui jambo jipya kama mtu alikuwa hafuatilii.

“Canada ni kazi, Profesa wa Chuo Kikuu anafanya kazi ya Uber (sijui kama Uber inafahamika Tanzania, dereva teksi kwa kutumia gari lake binafsi). Ofisa wa Serikali usiku anaosha vyombo hotelini.

“Ndiyo maana familia ina magari mawili au zaidi, TV, nyumba ya kisasa, chakula cha kisasa. Wanatekeleza sera ya Hapa Kazi Tu kwa matendo. Nadhani nimekupa taarifa za kutosha, ikiwa ni pamoja na kujibu propaganda kuwa nilihongwa mabilioni.”

Mapito ya Dk. Slaa

Dk. Slaa alizaliwa Oktoba 29, 1948, wilayani Mbulu na kusoma Shule ya Msingi Kwermusi na baadaye alijiunga na Shule ya Kati (Middle School) ya Karatu kati ya mwaka 1962-1965, ni msomi mzuri na mtaalamu wa theolojia.

Alijiunga na Seminari ya Dung’unyi mkoani Singida mwaka 1966-1969 na kusoma sekondari, kisha masomo ya juu ya sekondari katika Seminari ya Itaga, mkoani Tabora mwaka 1970 na 1971, ambako ndiko alihitimu kidato cha sita.

Baada ya hilo, alijiunga na Seminari ya Kibosho mwaka 1972-1973, ambako alipata stashahada ya Falsafa na baadaye kujiunga na Seminari Kuu ya Kipalapala, iliyoko Tabora, kati ya mwaka 1974 na 1977.

Dk. Slaa pia alipata Stashahada ya Theolojia katika Chuo Kikuu cha Makerere, nchini Uganda.

Alipata upadri mwaka 1977 na baadaye kujiunga na Chuo Kikuu cha Pontifical Urbaniana nchini Italia, akisomea udaktari wa Sheria za Kanisa, maarufu kama J.C.D. (Juris Canonici Doctor), ambayo ndiyo shahada ya juu katika masomo ya sheria ya kanisa kati ya mwaka 1979 na 1981.

Mbali na hilo, Dk. Slaa amewahi kuwa Msaidizi wa Askofu na Mkurugenzi wa Maendeleo katika Jimbo la Mbulu.

Pia alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kwa miaka tisa, lakini ilipofika mwaka 1991, Dk. Slaa alijitoa kwenye ubadri na kisha kumuoa Rose Kamili, kabla ya kuachana na baadaye kufunga pingu za maisha na Josephine Mushumbusi.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Dk. Slaa kuingia kwenye siasa, ambako kwa mara ya kwanza aliomba ridhaa ya kugombea ubunge kupitia tiketi ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.

Pamoja na madai ya kushinda wakati wa kura za maoni, vikao vya CCM vilipokutana Dodoma vilimuengua na kumuweka Patrick Qorro kugombea jimbo hilo la Karatu.

Hata hivyo, Dk. Slaa alikihama CCM na kujiunga na Chadema, ambako aligombea jimbo hilo na kushinda ubunge na huko alikuwa mbunge katika awamu tatu mfululizo.

Dk. Slaa anatajwa kuibua ufisadi na rushwa katika Bunge la miaka ya 2005– 2010.

Kutokana na namna alivyojituma ndani ya Chadema, chama hicho kilimsimamisha kugombea nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010.

Katika uchaguzi huo, Dk. Slaa aliibuka nafasi ya pili, akipata asilimia 27.05 ya kura zote, huku Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, akiongoza kwa kupata asilimia 62.83.

Dk. Slaa, ambaye ana stashahada tatu pamoja na Shahada ya Uzamivu (PhD), alijiengua ndani ya Chadema wakati kikielekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, baada ya chama hicho kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akitokea CCM.

Awali Dk. Slaa hakuonekana katika shughuli za chama hicho, ikiwamo ile ya Julai 28, mwaka 2015, ya kumpokea Lowassa, wakati wa kuchukua fomu za kugombea urais na Julai 30, siku ya kurudisha fomu hizo.

Kutokana na hilo, Agosti 3, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kuwa, Baraza Kuu la Chadema liliridhia aliyekuwa Katibu Mkuu huyo apumzike wakati chama hicho kikiendelea na mchakato wa Uchaguzi Mkuu, baada ya kutofautiana nao katika uamuzi huo wa kumkaribisha Lowassa kugombea urais.

Septemba, 2015, Dk. Slaa alizungumzia hilo na kuweka wazi kujiweka kando na siasa, kwa kile alichokieleza kutofautiana na viongozi wenzake ndani ya chama chake juu ya masharti ya kumpokea Lowassa.

Alisema sharti la kwanza ambalo alitaka Chadema izingatie ni kiongozi huyo wa zamani ndani ya Serikali ya CCM kujisafisha dhidi ya tuhuma ya kashfa ya sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond aliyohusishwa nayo akiwa Waziri Mkuu.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa, sharti hilo Lowassa alilitimiza katika vikao vya ndani vya Chadema, ambavyo Dk. Slaa mwenyewe alishiriki.

Watu wa karibu na familia ya Dk. Slaa walidai kuwa, mwanasiasa huyo alibadili msimamo baada ya kurudi nyumbani kwa mkewe, Josephine.

Inadaiwa Josephine hakupendezwa na uamuzi huo wa kumsimamisha Lowassa, kwa sababu aliona mumewe anapoteza nafasi ya kugombea urais na hata ndoto za yeye kuwa mke wa rais (First Lady).

Ingawa Josephine amekuwa akikataa jambo hilo kuwa sababu za msingi za yeye kumshawishi mumewe kukaa kando na siasa, mwaka huo huo waliondoka nchini na kukimbilia Canada, ambako wanaishi hadi sasa.

Taarifa zilidai kuwa, Dk. Slaa aliomba hifadhi ya kisiasa nchini humo, kwa sababu ya kuhofia usalama wa maisha yake hapa nchini, baada ya kuanza kutishwa na watu ambao hawajapata kujulikana, kutokana na uamuzi wake wa kujiondoa Chadema wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles