AJALI YAUA WATANO KILIMANJARO

0
1253

Na Upendo Mosha- Hai

WATU watano wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali ya gari aina ya Noah baada ya gari la mizigo la Kampuni ya Bonite kuacha njia na kugongana nalo uso kwa uso.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah, alisema ajali hiyo imetokea jana saa tisa alasiri katika Barabara Kuu ya Moshi/Arusha eneo la Daraja la Mto Kikavu wilayani Hai mkoani hapa.

Alisema Noah yenye namba za usajili T 646 BVU iliyokuwa ikitokea Moshi Mjini kuelekea Sanyajuu wilayani Siha, iligongana uso kwa uso na gari ya mizigo yenye nambari za usajili T 835 CJR na tela enye namba za usajili T 979 BTA na kusababisha vifo vya watu watano papo hapo na majeruhi saba.

“Gari ya mizigo iliacha njia na kwenda kuligonga gari dogo la abiria ambalo lilikuwa linapanda mlima katika Daraja la Mto Kikavu wilayani Hai na baada ya kuligonga lilitumbukia mtaroni lakini gari hilo lililifuata katika mtaro na kulikandamiza na kusababisha vifo vya watu watano pamoja na majeruhi saba,” alisema.

Pia alisema Noah ilikuwa na abiria 10 na kati yao, watano wamefariki na watano ni majeruhi huku katika gari la mizigo waliojeruhiwa ni wawili na majina ya waliofariki na majeruhi bado hayajafahamika.

“Majina ya madereva, majeruhi na marehemu bado hayajafamika, lakini hadi sasa majeruhi wote wamewahishwa katika Hospitali ya KCMC na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here