25.2 C
Dar es Salaam
Monday, December 2, 2024

Contact us: [email protected]

JPM, Lungu waeleza manufaa kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Tunduma

Na ANDREW MSECHU

RAIS John Magufuli na Rais Edgar Lungu wa Zambia, wamezindua Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani cha Tunduma kwa upande wa Tanzania na Nakonde kwa upande wa Zambia, huku wakisema kitakuwa na manufa matatu makubwa ikiwamo kuongeza mapato na kupunguza usumbufu kwa wafanyabiashara.

Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hichi mjini Tunduma jana, Rais Magufuli alisema kitasaidia pia kushamiri kwa biashara kati ya nchi hizi mbili, ambazo zimekuwa na ushirikiano wa kihistoria.

Waasisi wa nchi hizo ni Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Kenneth Kaunda wa Zambia, ambao kwa pamoja waliimarisha ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi katika nchi zao, kisha kuanzisha harakati ya ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

Rais Magufuli alisema kituo hicho pia kitarahisisha upitaji wa watu na bidhaa na kurahisisha taratibu za utendaji kazi kwa pande zote mbili na kuboresha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

“Kituo hiki cha kisasa kabisa kilichogharimu Sh bilioni 14 ni muhimu kwa maenedeleo yetu, kwa sasa miundombinu ya mipakani nama hii ni kipaumbele chetu kwa kuwa tunataka kukuza biashara baina ya nchi zetu na biashara ya kikanda,” alisema.

Alisema ujenzi huo uliosaidiwa na Uingereza kupitia ufadhili wa Shirika la Trade Mark East Africa (TMAE) ni chachu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kibiashara wa Tanzania, Zambia na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Alisema kwa sasa, kituo hicho kitakuwa na manufaa yanayotarajiwa iwapo watendaji na maofisa wote watazingatia madhumuni ya kuanzishwa kwake, ili kuondoa urasimu na kuharakisha usafirishaji wa bidhaa na mizigo baina ya nchi hizo.

“Kwa watendaji na maofisa wote wa Zambia na Tanzania sasa waache kuwabughudhi wafanyabiashara na wasafirishaji, msisababishe urasimu usio wa lazima wala kujenga mazingira ya rushwa, mtambue kuwa macho ya Serikali zote mbili yanawatazama.

“Waacheni wafanye biashara wafanye biashara watajirike, hayo ndiyo matarajio yetu mimi na Rais wa Zambia (Edgar Lungu), yeye anaitwa Lungu na mimi ninaitwa pombe, na mnajua kazi ya rungu. Lakini pia mnajua matokeo ya pombe hasa ukinywa zile za jamii ya gongo,” alisema.

Alisema ili kufikia malengo tarajiwa ni lazima vikwazo vyote vya kibiashara viondolewe na anaamini kuundwa kwa kituo hicho, vikwazo hivyo vitakuwa historia.

Rais Magufuli aliwataka wananchi pia kuwa mstari wa mbele kuwafichua waharibifu wa miundombinu ya kituo hicho.

Alisema pamoja na kufanya biashara, ni lazima tuendelee kuimarisha undugu wa kweli baina ya watu wa nchi hizi mbili, ambao ni wa kihistoria.

“Nina uhakika hapa hata Lungu anafahamu, inawezekana kuna mtu yuko huku au ana mke kutoka huko upande wa pili au kuna mtu kutoka huko ana nyumba ndogo huku, au wa huku ana girlfriend yuko huko au wa huko ana mshkaji huku, na huo ndio undugu ninaouzungumzia,” alisema.

Aliongeza kuwa nchi zote mbili ni wanachama wa Sadc lazima kutangaza biashara miongoni mwa nchi hizo huku akitoa wito kwa wana-Tunduma kuhakikisha wanatumia fursa kikamilifu.

Rais Magufuli alisema pamoja na uwepo wa fursa hizo, wapo waliojenga kwenye eneo la ukingo wa mpaka baina ya Tanzania na Zambia, ambapo wengine chumba cha watoto kiko Zambia na cha wazazi kiko Tanzania.

Alisema tatizo hilo lilianza kushughulikiwa muda mrefu lakini bado utekelezaji unasuasua hivyo ni lazima eneo hilo la mpaka litambulike rasmi na liwekwe wazi, kwa wale waliojenga katika eneo hilo kuondoka kabla sheria haijachukua mkondo wake.

“Wale waliojenga na waliokuwa na mpango wa kujenga kwenye buffer zone (eneo la mpaka), niwambie tu bahati nzuri mimi kubomoa nimeshazoea, nimekuwa Wazir wa Miundombinu kwa karibu miaka 15, kwa hiyo hili si suala geni kwangu.

“Na katika kutekeleza hili, yeyote aliyeingia kwenye eneo hilo bila kujali chama, awe wa CCM au anatokea upinzani atashughulikiwa tu kwa sababu maendeleo hayana chama,” alisema.

Edgar Lungu

Kwa upande wake, Rais Lungu alisema kituo hicho ni kimoja kati ya vituo vyenye shughuli nyingi kwa ukanda wa Kusini mwa Afrika na kunakuwa na magari ya mizigo zaidi ya 600 kwa siku, hivyo kuhusisha biashara yenye thamani ya mamilioni ya dola za kimarekani katika ushoroba wa Dar es Salaam hadi Zambia.

Alisema baada ya kuboresha miundombinu, kutakuwa na uharakishaji wa mizigo na kuongeza kiwango cha biashara baina ya nchi hizi mbili.

“Kituo kimoja kimepunguza urasimu na muda wa watu kukaa mpakani kutoka siku nne awali hadi siku moja, hivyo kitasaidia kuoanisha taratibu za kutoa mizigo na kukuza mbinu za uratibu na kurahisisha zaidi utendaji kazi kwenye mpaka wetu.

“Ninashukuru Serikali zetu ambazo ni wazi kwamba hazitasaidia wafanyabiashara wakubwa tu, bali pia wafanyabiashara wadogo kupitia mkataba maalumu uliosainiwa mwaka 2017 na hii ni muhimu kwa kuwa watu wetu wengi wanafanya biashara ndogondogo,” alisema.

Alisema wafanyabiashara wakubwa wanakuja na kuondoka, lakini wadogo wapo pale wakati wote wakihitaji usaidizi wa Serikali, hivyo wanahitaji kuwasaidia sana.

Alisema kurahisishwa kwa mfumo wa pamoja kutasababisha kuwepo kwa dawati la pamoja la taarifa, ambalo litasaidia kukuza takwimu za wafanyabiashara wadogo wanaovuka mipaka na kutoa taarifa kuhusu namna ya kuboresha biashara kwenye mipaka.

“Ninaomba mamlaka zote mbili za hapa mpakani kusaidia wafanyabiashara wadogo kwa kuweka taratibu nzuri za kuwaisadia katika kuvuka mpaka na kusaidia kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma, hata kama tunatumia mfumo wa kielektroniki,” alisema.

Alimwambia Rais Magufuli kuwa yeye akiwa Rais wa Tanzania na (Lungu) ambaye ni Rais wa Zambia, ni lazima wahakikishe katika juhudi za kuleta maendeleo ya watu hakuna anayeachwa nyuma.

Alisema wakati mwingine nchini kwake kunakuwa na changamoto nyingi katika kufikia kituo hicho, moja ikiwa ni miundombinu isiyotosheleza, hivyo ni lazima waendelee kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha wanatatua changamoto zote zilizopo na zile zitakazotokea baadaye.

Rais Lungu alisema ili nchi hizo ziendelee kwa haraka, lazima wahakikishe maofisa kutoka pande zote mbili wana utaalamu unaohitajika ili kuhakikisha malengo ya kituo hiki yanafikiwa.

Alisema historia ya ushirikiano katika ya Tanzania na Zambia hauishii tu katika kusaini makubaliano kama hayo, bali inaanzia tangu waasisi wa mataifa hayo walipoamua kushirikiana katika kupigania uhuru, kujenga Reli ya Tazara na Bomba la Mafuta la Tazama.

“Kwa sababu hiyo ninapenda kueleza nia yangu ya dhati ya Serikali yangu kujitolea kuendelea ushirikiano na kusimamia ufanisi wa kituo hiki na katika mipango mingine.

“Ninaunga mkono wale waliojenga katika mpaka lazima waondolewe, kaka yangu (Rais Magufuli) yeye ni buldoza lakini na mimi pia huwa naonyesha mambo yangu, kwa hiyo lazima kuchukua hatua.

“Kwa wale Wazambia mliojenga mpakani mjadiliane na viongozi wenu muondoke kwenye maeneo hayo, kama hutaki kuchukua karoti utachukua fimbo, bila kujali kama uchaguzi utafanyika kesho,” alisema.

Alisisitiza kuwa kwa wale wasiotaka kuondoka mapema watachukua fimbo, tena fimbo kubwa, kwa kuwa hana woga katika kuwashuhulikia kwa mujibu wa sheria, maana wengi wao wanajua kuhusu waliowahi kushughulikiwa siku zilizopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles