23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

JPM kuzindua Hifadhi ya Burigi-Chato kesho

ELIYA MBONEA-KARAGWE

KESHO Rais Dk. John Magufuli anatarajiwa kufungua  Hifadhi ya Burigi-Chato yenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,702.

Akizungumza kwenye mahojiano na wanahabari waliotembelea hifadhi za Burigi-Chato, Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu, alisema watakaowekeza katika hifadhi hizo hawatajutia fursa hiyo.

“Wawekezaji wa Kitanzania katika sekta ya utalii changamkieni maeneo yaliyotengwa na kuyatumia kibiashara kabla wageni hawajayachangamkia.

 “Uwekezaji unaotakiwa kwenye maeneo hayo si wa maghorofa, ni huduma bora, ndiyo maana watalii hupendelea kulala kwenye mahema na kuona vitu wanavyovitaka,” alisema Kanyasu.

Alisema katika eneo ambalo Tanzania haijafanikiwa kulitumia hata kwa asilimia 30, ni eneo la biashara ya utalii, kwamba hadi sasa zinatumika asilimia 10 hadi 25 ya vivutio vilivyopo.

 “Tanzania ni ya kwanza Afrika kuwa na vivutio vingi, tungeweza kupokea watalii milioni 10 kwa mwaka. Lakini watalii hao wanatafutwa na nani?

“Kazi ya Serikali ni kuuza maeneo ya hifadhi, wafanyabiashara wa Kitanzania kwa ubia na wengine wana wajibu wa kutafuta wateja na kuwekeza kwenye sekta ya utalii ili wapate utajiri,” alisema.

Katika mahojiano hayo, Kanyasu alizitaja sababu za kupandisha hadhi yaliyokuwa mapori ya akiba na kuwa hifadhi za taifa kwanza ilikuwa ni kuyaongezea thamani.

“Tunaamini Tanapa wamekuwa na uzoefu na utaalamu wa kufanya biashara ya utalii kwa muda mrefu na wana uwezo wa kusimamia biashara ya utalii.

“Hifadhi ya taifa ni hatua ya juu kabisa ya uhifadhi ambapo tunaamini kutaongeza thamani na kuhamasisha wawekezaji kwenda maeneo hayo na kuyatumia kibiashara.

 “Utalii wa Kaskazini umeimarika si kwa bahati mbaya, kwa sababu mgeni akiteremkia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), anaweza kwenda Hifadhi ya Mkomazi, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tarangite na Ngorongoro na Serengeti.

“Hivyo uwapo wa Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato, Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe, Rubondo, Gombe na Katavi, kutafanya ukanda huo kuwa eneo kubwa, hivyo mtalii kuchagua aanzie wapi,” alisema Kanyasu.

Alisema kuanza kupokea watalii kwenye hifadhi hizo kutavuta idadi kubwa ya wawekezaji waliohofia kwenda kuwekeza kutokana na hofu ya kuwa na hifadhi moja ambayo ikipokea watalii 500 inakuwa imejaa.

“Kujengwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chato uliopo kilometa 180 kutoka Geita ni mkakati madhubuti wa kuunyanyua na kutangaza utalii kwenye ukanda huo.

“Uwanja ule una umuhimu, utaongeza thamani ya hifadhi na pili watalii watakwenda kwenye hifadhi zilizopo maeneo hayo kwa gharama nafuu,” alisema Kanyasu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles