Grace Semfuko-Dar es Salaam
SERIKALI imeanza mchakato wa ununuzi wa vichwa 22 vya treni, mabehewa 1,430 ya mizigo na 60 ya abiria vitakavyotumika katika uendeshaji reli ya kisasa ya SGR ambayo ujenzi wake unaendelea.
Kampuni ya Yapi Merkez inajenga reli ya SGR awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 56 na awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora Dodoma, umefikia asilimia 52, vipande vyote vikiwa na kilomita 722 na kugharimu Sh trilioni 7.2.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe wakati akizindua safari ya kwanza ya treni ya majaribio kwenye reli hiyo ya kisasa katika eneo la Soga Kibaha mkoani Pwani.
Kamwelwe alisema mpango wa sasa wa Serikali ni kuwa na seti tano za treni za SGR zitakazokuwa na behewa nane za abiria, mpango ambao unalenga kuimarisha sekta ya usafirishaji wa reli.
“Tumezindua majaribio ya njia ya reli yetu, hii ina maana kwamba tupo katika mipango ya kuhakikisha reli inakamilika kwa wakati, tumetembea kilomita 20 za majaribio, reli ni salama kabisa, haina kikwazo, sasa tumeanza mchakato wa kununua vichwa vya treni 22 na mabehewa yake 60 ya abiria na 1,430 ya mizigo,” alisema Kamwelwe.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, alisema majaribio ya awali ya treni ya wahandisi ni hatua muhimu ya kuhakikisha reli hiyo inapitika bila kikwazo kwani inakagua na kuimarisha miundombinu ya reli hiyo.
Alisema zoezi hilo la awali limekuja kufuatia kukamilika kwa baadhi ya maeneo ya kupita treni kuanzia Soga, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani kuelekea Morogoro na kuongeza kuwa treni rasmi itawasili hivi karibuni.
Majaribio ya uendeshaji wa reli ya kihandisi yalishuhudiwa na Kamwelwe, maofisa wa TRC na waandishi wa habari ambao walitembea na treni hiyo kwa kilomita 20.