27.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

JPM, Kenyatta wakubaliana maeneo manne ya biashara

Mwandishi Wetu – DAR ES SALAAM

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amemaliza ziara binafsi ya siku mbili nchini, ambapo kabla ya kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Chato mkoani Geita, walifanya mazungumzo mwenyeji wake Dk John Magufuli, ambapo pamoja na mambo mengine wamezungumzia ushirikiano wa kiuchimi.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, ilisema viongozi hao wametaka biashara baina ya nchi hizo ikuzwe zaidi na kujenga uwiano wa kibiashara wenye maslahi kwa pande zote.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli alisema kwa kuwa Kenya imefanya uwekezaji mkubwa Tanzania ikilinganishwa wa Tanzania nchini Kenya, wamekubaliana kuwa kampuni za Kenya zijielekeza kuongeza thamani ya bidhaa kwa kuanzisha viwanda vitakavyosindika mazao na kuchakata bidhaa mbalimbali hapahapa badala ya kusafirisha malighafi kwenda Kenya.

Taarifa hiyo ilisema viongozi hao wamekubaliana kuwa, Kenya itanunua gesi ya Tanzania badala ya kuagiza kutoka nje ya Bara la Afrika kwa kuwa Tanzania imejaaliwa gesi nyingi, na kwamba wameagiza mawaziri wa Tanzania na Kenya kukutana na kujadili namna Kenya itavyonunua gesi hiyo.

Kuhusu ziwa Victoria ambalo kwa asilimia 51 lipo Tanzania na kwa asilimia 5 lipo Kenya, taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli alisema wamekubaliana kuwa mawaziri wa nchi hizo wahakikishe meli za Tanzania na Kenya zinaimarishwa na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha meli hizo kufanya kazi ya kukuza biashara katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ambazo zinazunguka ziwa hilo.

Taarifa hiyo ilisema kwa upande wake Rais Kenyatta, alisema pamoja na kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Kenya, wamekubaliana kuhakikisha nchi hizo zinakuwa na amani na kuheshimu mkataba wa kukabiliana na uhalifu.

Alisema Mtanzania atakayekamatwa kwa uhalifu nchini Kenya atashughulikiwa sheria za Kenya na Mkenya atakayekamatwa kwa uhalifu Tanzania, atashughulikiwa kwa sheria za Tanzania.

Ilisema Kenyatta alisisitiza kuwa Wakenya na Watanzania hawana sababu ya kupoteza muda kwa mambo yasiyo ya msingi bali kuhakikisha uchumi unakua, biashara inaongezeka na uhusiano na ushirikiano katika maeneo mbalimbali unaimarika zaidi.

Akiwa nyumbani kwa Rais Magufuli katika Kijiji cha Mlimani Wilayani Chato, Kenyatta ameweka shada la maua katika makaburi ya familia ya Rais Magufuli na kumtembelea mama wa Rais, Suzana Magufuli ambaye baada ya kupatiwa matibabu ya kiharusi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam anaendelea kupata matibabu hayo akiwa nyumbani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles