30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Tacaids yaonya maambukizi zaidi VVU kwa vijana

NA MWANDISHI WETU – Geita

MKURUGENZI Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk. Leonard Maboko, amesema maambukizi ya Virushi Vya Ukimwi (VVU) kwa Tanzania bado yako juu.

Amesema kila mwaka watu 72,000 hupata maambukizi mapya, huku vijana wakiwa waathirika zaidi.

Dk. Maboko alisema hayo katika hafla ya Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) kutoa msaada wa Sh milioni 50 kwa kituo cha kulelea yatima cha Moyo wa Huruma, Geita.

 “Takriban watu milioni 1.5 wameambukizwa VVU, kwa wastani wa hali ya maambukizi ni sawa na asilimia 4.7 kwa Tanzania bara,” alisema.

Alisema wakati maambukizi hayo yakipungua kwa ujumla wake kwa Watanzania, yamekuwa yakiongezeka kwa vijana kati ya miaka 15 hadi 24.

 “Makundi mengine yaliyoko kwenye mazingira hatarishi ni kama vile wasafirishaji wa masafa marefu, watu wanaotumia dawa za kulevya, wanaofanya mapenzi kinyume na maumbile, wanawake wanaofanya biashara ya ngono, wafanyakazi kwenye migodi, wavuvi na wafanyakazi kwenye mashamba makubwa,” alisema Dk. Maboko.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Adalbera Mukure, alisema tangu kifunguliwe mwaka 2006 kwa kuwezeshwa na GGM, kinahudumia watoto 137 ambao hutumia zaidi ya Sh milioni 200 kwa mwaka kwa matumizi ya chakula pekee.

“Kwa kutaja milioni 200 unaweza kuhisi ni fedha nyingi, ila tujaribu kutafakari kuwa watoto hawa 137 wanatakiwa kupata milo mitatu kwa siku 365, sawa na wewe watoto wako unavyowalisha nyumbani, kwa hiyo hili ni jukumu kubwa ambalo sisi peke yetu hatuwezi.  “Tunahitaji misaada kutoka kwa watu mbalimbali, na mashirika binafsi ili kuendesha kituo hiki ambacho sasa  kimeboresha maisha ya watoto mbalimbali,” alisema.

Alisema kituo kimesomesha watoto 18 wa chekechea, shule za msingi 70, sekondari 29, kidato cha tano na sita 8, vyuo vikuu wawili, mmoja chuo cha walimu na kwamba wawili wameajiriwa sekta binafsi na wawili bado hawajapata ajira.

 “Tunaomba michango yenu kuwezesha ujenzi wa shule ya English Medium ili kuwezesha watoto kusoma na hata watoto wa nje ya kituo kusoma na fedha zitakazopatikana kutumika kuendesha kituo,” alisema.

Makamu wa Rais wa GGM, Simon Shayo, alisema; “GGM tulianzisha Mfuko wa Kilimanjaro Challenge Against HIV & AIDS miaka 17 iliyopita, ambao sasa umekusanya zaidi ya Sh bilioni 13 ambazo zimenufaisha taasisi 50 zinazotoa huduma za VVU na Ukimwi na Mfuko wa Ukimwi (ATF),” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,195FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles