20.5 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

JPM: Kapigeni kura kwa utashi wenu

Na NORA DAMIAN -DODOMA

RAIS Dk. John Magufuli amewataka Watanzania kutumia utashi wao kuchagua viongozi wanaowafaa, watakapokwenda kwenye vituo vya kupigia kura kesho.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa msikiti uliojengwa katika Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma, aliwataka Watanzania kuhamasishana kwenda kupiga kura kisha kurudi nyumbani.

“Tarehe 28 tuitumie kujenga mazuri, tuitumie katika kujenga umoja wa Tanzania, tukapige kura kulingana na utashi wa mioyo yetu.

“Naomba muhamasishane wote kapigeni kura, ukimaliza nenda nyumbani, fujo hazijengi nchi, Tanzania ni ya amani, pakiwa na fujo huwezi ukafanya biashara, huwezi ukaenda hata msikitini, kanisani. 

“Tunataka amani ikatawale baada ya uchaguzi kwa sababu kuna maisha baada ya uchaguzi,” alisema Dk. Magufuli.

Aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha umoja na mshikamano, na kamwe wasikubali kuvivuruga kwa misingi ya dini, kabila, rangi au itikadi za kisiasa kwani ni tunu ambayo waasisi wameiacha.

“Sifa kubwa inayoitofautisha Tanzania na mataifa mengine ni umoja na mshikamano uliopo nchini, zipo baadhi ya nchi zimeingia kwenye vita sababu ya dini, makabila, rangi, lakini Tanzania imejaliwa kuwa na umoja na wananchi hawabaguani.

“Unaweza kwenda kwenye familia utakuta mume Mchaga, mke Mgogo au wazazi Waislamu, mtoto ni Mkristu na wanaishi kwa upendo. 

“Sifa hii tuliyonayo haikutokea bahati mbaya, ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na waasisi wa taifa hili, hayati Mwalimu Nyerere na (Abeid Amani) Karume kwa kujenga taifa lenye umoja na mshikamano, ambalo leo tunafurahia matunda yake,” alisema Dk. Magufuli.

Kuhusu msikiti huo uliopewa jina la Sheikh Abubakar Zubeir Ally, alisema kwa lengo la kuwaenzi waasisi wa taifa, aliamua kuendesha harambee ya ujenzi wake, baada ya kuona uliokuwepo awali ulikuwa mdogo na umechakaa.

Dk. Magufuli aliendesha harambee hiyo Agosti 23 wakati wa uzinduzi wa ukarabati wa Kanisa Katoliki Chamwino, Parokia ya Mama Bikira Maria Imaculata.

Alisema pia atakapochaguliwa tena ataendeleza utaratibu huo ili kuhakikisha madhehebu yote yanakuwa na sehemu ya kuabudia, huku akiahidi kuwa Sh milioni 1.1 zilizobaki zitachanganywa katika harambee nyingine kwa ujenzi wa Kanisa la Wasabato.

“Huwezi kuwa na Ikulu halafu pakakosa nyumba ya kuabudia, nitafurahi kama itazungukwa na misikiti, makanisa, hizo fedha zilizobaki tutaendesha harambee kwa ajili ya wale wanaosali Jumamosi (Wasabato) ili madhehebu yote yawe na mahali pa kuabudia Chamwino,” alisema Dk. Magufuli.

Alilipongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kujenga msikiti huo na kuagiza waliojenga waajiriwe na wengine wapandishwe vyeo.

AMSHUKURU ROSTAM

Dk. Magufuli pia alimshukuru mfanyabiashara Rostam Azizi kwa kujitoa kuchangia ujenzi wa msikiti huo pamoja na ukarabati wa Kanisa Katoliki Chamwino. 

“Waumini wengi waliokuwepo kanisani walitoa michango yao kwa ajili ya kujenga msikiti, baadaye watu walijitokeza kutuongezea nguvu, zikapatikana milioni 319.3.

“Nimefurahi kumuona rafiki yangu Rostam, wakati nachangisha Kanisa la Katoliki alichangia milioni 20, nilipoanza kuchangisha tena hapa akaniletea milioni 20. Kwa yeyote aliyechangia msikiti huu asijione kwamba amepoteza, amefanya jambo zuri sana ambalo lina ujira mkubwa kwa Mwenyezi Mungu,” alisema Dk. Magufuli.

MUFTI

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir, alimshukuru Dk. Magufuli kwa ukarimu mkubwa aliowafanyia Waislamu kwa kushawishi kujengwa kwa msikiti huo pamoja na ule wa kimataifa uliojengwa Kinondoni, Dar es Salaam.

“Nakupongeza kwa ujasiri mkubwa ulioufanya na ukarimu wako uliowafanyia Waislamu, haya yote umeyafanya kwa sababu Mungu amekupa kipaji cha kuwapenda viongozi wa dini na kuwapa heshima stahiki.

“Na umekuwa ukimtanguliza Mwenyezi Mungu mbele, umekuwa ukijinyenyekeza na kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi na kuwajali wanyonge.

“Tunashukuru wadau wote ambao wamemuunga mkono rais. Miongoni mwa waliochangia ni Rostam. Kanisa pia limechangia na hakuna ubaya, Mtume alipokea zawadi kwa wasiokuwa Waislamu,” alisema Mufti Zubeir.

JKT

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Charles Mbuge, alisema ujenzi wa msikiti huo ulianza Agosti 28 na hadi sasa umekamilika kwa asilimia 100 huku ukiwa umegharimu zaidi ya Sh milioni 319.2 na fedha zilizobaki ni Sh milioni 1.1.

Alisema msikiti huo utakuwa na uwezo wa kuchukua waumini 500 tofauti na ule wa awali uliokuwa na uwezo wa waumini 150.

KAMPENI KONDOA, CHEMBA

Akiwa njiani kutoka mkoani Manyara kwenda jijini Dodoma, Dk. Magufuli alisimama maeneo tofauti ya majimbo ya Kondoa na Chemba na kuzungumza na wananchi waliokuwa wamesimama pembezoni mwa barabara na kuahidi kuteua mawaziri watakaokuwa na macho ya ziada ya kutatua kero za wananchi.

“Ninataka nitakayemteua kuwa waziri wa maji katika kipindi cha miaka mitano mingine, awe ni waziri ambaye atakuwa anaangalia nje ya boksi, kwa sababu hapa Chemba madaraja makubwa na makaravati tuliyoyajenga yanapitisha maji, sasa swali la kujiuliza haya maji yanayopita yanakwenda wapi?

“Hatuwezi kushindwa kutengeneza mabwawa ili wafugaji, wakulima na wananchi wafaidike, hatuwezi tukawa na wilaya jirani na makao makuu halafu hakuna maji,” alisema Dk. Magufuli.

Aliahidi pia kutatua kero za wananchi wa maeneo hayo zikiwemo za kuongezewa vituo vya afya, ujenzi wa kituo cha polisi Wilaya ya Chemba, shule ya sekondari, nyumba za walimu na madarasa na ujenzi wa barabara hasa katika maeneo yanayopitika kwa shida wakati wa mvua.

Dk. Magufuli ambaye hadi sasa amefanya kampeni katika mikoa 19, leo anatarajiwa kuhitimisha kwa kuongea na wazee katika Jiji la Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles