23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TPDC yatangaza kuanza kufanya biashara ya mafuta

Na FARAJA MASINDE -DAR ES SALAAM

CHANGAMOTO ya baadhi ya wafanyabiashara kuficha mafuta na kusababisha bidhaa hiyo kukosekana katika baadhi ya nyakati, huenda ikabaki historia baada ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutangaza kuingia katika biashara hiyo kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano TPDC, Marie Msellemu, alisema katika kipindi cha miaka mitano, wamejipanga kujenga vituo 100 vya mafuta ambavyo vitalenga kutoa huduma ya mafuta kwa wananchi.

“Tutajenga vituo hivi kwa kushirikiana na halmashauri na sekta binafsi. 

“TPDC haikuwa na majukumu ya kufanya biashara, jukumu letu kubwa ilikuwa ni udhibiti wa mafuta na gesi. 

“Sasa sheria ya mafuta ya mwaka 2015 iliipa TPDC majukumu ya kujiendesha kibiashara kutoa huduma kwa wananchi, huku shughuli za udhibiti sasa kufanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu (PURA),” alisema Marie.

Alisema hawataingia kushindana na kampuni za mafuta, bali dhamira yao ni kuhakikisha changamoto ya kukosekana kwa mafuta katika nyakati fulani inakoma.

Marie alisema vituo vya mafuta vilivyopo nchini ndivyo watakavyovitumia kuwapa wananchi huduma hiyo.

Alisema ili TPDC iendane na majukumu yake, wamekusudia kubadili nembo, hivyo wamewaalika wabunifu mbalimbali kuwasilisha kazi zao ili zishindanishwe.

“Safari ya mwonekano mpya inaanza leo mpaka tutakapohitimisha, hivyo TPDC inakusudia kuwaalika vijana, wajasiriamali na wote wenye vipaji walete kazi zao zenye nembo mpya watakayoibuni ya TPDC.

“Tunategemea kuanzia sasa mpaka Septemba 8 mshindi atakuwa amepatikana na zawadi kutolewa Novemba 12,” alisema Marie.

HUJUMA ZA WAFANYABIASHARA

Juni mwaka huu, Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo, alisema wamevifutia leseni za uuzaji wa mafuta vituo vitano, kwa makosa ya kuficha, kutouza na kuuza mafuta juu ya bei elekezi.

Alisema uamuzi huo umechukuliwa baada ya tathmini ya kina iliyowawezesha kubaini sababu za makusudi kwa wauzaji hao kuhujumu uuzaji wa mafuta.

Kaguo alisema katika uchunguzi wa awali uliofanywa na Ewura, kuna dalili za wafanyabiashara kufanya hujuma kwa kuwanyima wananchi mafuta kwa makusudi na kutoa onyo kwa wauzaji wote kutofanya hujuma ambazo zitawaingiza katika uhujumu uchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles