24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa dini watoa neno Uchaguzi Mkuu

 Na WAANDISHI WETU -DAR/MIKOANI

VIONGOZI wa dini kote nchini wamezungumzia umuhimu wa amani wakati wa Uchaguzi Mkuu wakitaka Watanzania kuilinda kwa kuwa ni tunu isiyohitaji kuchezewa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Thadeus Ruwa’ichi alisema ni vyema Watanzania wanapokwenda kupiga kura wahimizwe kushiriki kwa ukomavu, utulivu, kwa nidhamu na uzalendo wa hali ya juu.

“Niwaombe pia wale wanaohusika na vyombo vya dola wahakikishe mazingira yanayohitajika yanakuwepo kwa ajili ya kuwawezesha raia kupiga kura zao bila bughudha, usumbufu na bila uwoga wowote,” alisema Ruwa’ichi.

Pia aliwataka Watanzania kuungana kumwomba Mungu ili uchaguzi uende vizuri, viongozi wazuri wapatikane kwa ustawi wa maendeleo ya taifa.

Ruwa’ichi aliwataka waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali wawe watulivu ili matokeo yanapotolewa wayapokee katika mazingira ya amani na usalama. 

Alisema viongozi wote wa dini ni wadau wa amani na haki, hivyo aliwataka waendelee kuwahimiza raia watimize msimamo unaotetea haki na amani kwa kuwa ni vitu viwili ambavyo vinaenda pamoja.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima aliwataka Watanzania kuwa makini kufuata sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na mamlaka husika katika kipindi hiki cha uchaguzi.

“Vyombo vinavyohusika kuratibu na kusimamia Uchaguzi Mkuu, vina wajibu wa kuzingatia sheria, taratibu na maadili ya kazi zao ili kuwapa wapigakura na wapigiwa kura imani juu ya kazi zao,” alisema Padre Kitima. 

SINGIDA 

Viongozi wa dini mkoani Singida, wamesema hawapo tayari kuruhusu wala kuwa upande wa wanasiasa wenye nia ovu ya kuwagawa wana-Singida na taifa.

Pia wamewataka wakazi wa Mkoa wa Singida kuzingatia na kufuata kanuni, taratibu, maelekezo na sheria za uchaguzi zilizowekwa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza, ikiwemo kuligawa taifa sambamba na kuhatarisha ustawi wa amani iliyopo.

Akizungumza wakati wa Kongamano la Amani la Viongozi wa Dini lililofanyika mwishoni mwa wiki, Sheikh wa Bakwata mkoani hapa, Issa Nassor, alisema Nabii Abrahamu katika dua yake ya kwanza alimwomba Mungu aujalie mji wa Makka uwe na amani, utulivu na salama, na dua ya pili aliomba chakula na matunda, maana bila amani chakula na vingine vyote visingekuwa na maana.

Aliwasihi viongozi wenzake wa dini kuwa katika kipindi hiki ambacho taifa litapiga kura kesho kinachotakiwa ni kuelekeza jamii kushiriki uchaguzi katika hali ya salama na amani. 

“Ni jukumu la viongozi wa dini kuweka misingi ya amani kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

“Niwasihi viongozi wenzangu wa dini tusitumike kuvunja amani, tutafakari kwanza, ni kipindi kigumu. 

“Na Watanzania tutumie kadi zetu vizuri katika kuleta haki, usawa, amani na viongozi bora.

“Suala la vijana kuhakiki kura au kuendelea kukaa kwenye vituo vya kupigia kura hilo si jambo sahihi hata kidogo, litasababisha uvunjifu wa amani,” alisema Sheikh Nassor.

Askofu kutoka Kanisa la Tanzania Assemblies of God Singida (TAG), Gasper Mdimi aliwasihi viongozi wa dini kusimamia upande wa Mungu, huku akisisitiza kuna kila sababu ya kuilinda amani iliyopo kama ‘yai,’ lakini zaidi kuwa makini sana inapozungumziwa amani na hasa kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.

“Chanzo cha amani ni Mungu mwenyewe. Na ili amani iendelee kuwepo lazima haki izingatiwe, tukimwogopa na kumcha Mungu kamwe hatutatumbukia kwenye kutenda mabaya,” alisema Askofu Mdimi.

DODOMA 

Mkoani Dodoma, Kanisa la Uweza wa Bwana limefanya maombi maalumu ya kuombea Uchaguzi Mkuu, huku likiwaomba wagombea wa nafasi mbalimbali kukubali matokeo ambayo watayapata kwani kuna maisha baada ya uchaguzi. 

Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Amos Yusuphu alisema hakuna mbadala wa amani, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda amani iliyopo kwa vitendo.

“Tuendelee kuiombea nchi yetu, tuendelee kulinda amani iliyopo katika nchi yetu, tunawasihi Watanzania kuendelea kulinda amani iliyopo kwa nguvu zote, hasa kipindi hiki cha uchaguzi,” alisema Askofu Yusuphu.

Katibu wa Kanisa hilo, Boniface Kisinga alisema wagombea wote katika nafasi za ubunge, udiwani na urais wanatakiwa kukubali matokeo na wasiweke ubinafsi kwani kipaumbele ni kuendelea kuilinda amani ya nchi.

“Tunatoa rai kwa wagombea wote katika Uchaguzi Mkuu wakubali matokeo na kuondoa ubinafsi wa kukataa matokeo,” alisema Kisinga. 

Alisema kipaumbele cha kwanza ni amani, hivyo Watanzania wana wajibu wa kuilinda kwa nguvu zote wakati huu na kuwasihi kutokubali kushawishika kuivunja katika kipindi hiki cha uchaguzi.

“Shida yoyote ikitokea tutapata shida, kupoteza amani ni kujipoteza sisi wenyewe, kwahiyo tunatoa rai kwa Watanzania tusikubali kushawishiwa kwa namna yoyote ile ya kuonyesha viashiria vya uvunjifu wa amani.

“Kwa pamoja tuwakatae watu ambao hawaoni umuhimu wa amani, madhara ya kupoteza amani ni makubwa kwani chuki na vifo vitatawala kila mahali, kila Mtanzania anawajibika kulinda amani maana ndio mboni ya Watanzania. 

“Tunatoa rai kwa viongozi wa dini na misikiti na makanisa wawaambie waumini na kuwaonya wasiwe sehemu ya kupoteza amani bali tuhamasishe kushiriki kupiga kura,” alisema Kisinga. 

TANGA 

Viongozi wa dini mkoani Tanga wamekutana jana huku wakitoa maazimio matano, ikiwemo kupinga aina yoyote ya vurugu na maandamano, viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi huo.

Akisoma maazimio ya Baraza la Amani Mkoa wa Tanga, Askofu Mstaafu wa Kanisa la TAG, Dk. Jonson Mwakimwage wakati wa kikao cha baraza hilo, alisema wao kama viongozi wa dini hawatakubali kuona vurugu na maandamano yakitokea wakati wa uchaguzi huo.

Alisema badala yake watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha vitendo vya namna hiyo havitokei kwenye jamii ili Watanzania waweze kushiriki kwa amani uchaguzi huo.

“Leo tumekutana kwenye kikao hiki maalumu kuelekea kwenye uchaguzi mkuu lakini moja ya maazimio yetu ni kutaka uchaguzi kufanyika kwa amani na tunakataa maandamano ya vurugu ya aina yoytote,” alisema Askofu Mwakimage.

Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Juma Luwuchu alisema wao viongozi wa dini wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kuhimiza amani.

Alisema kwamba moto mkubwa chanzo chake ni cheche, hivyo Watanzania wasichezee cheche ya moto.

“Uchaguzi ni siku moja na maisha ni kila siku, hivyo Watanzania walitambue hilo na kufikiria.

“Ndugu zangu tusichezee cheche wakati wa uchaguzi kwani siku moja tukichezea tunaweza kufanya tusiwe na nyumba ya kuwaongoza watu misikitini wala makanisani,” alisema Sheikh Luwuchu.

Aliwataka viongozi wa dini wasigeuke kuwa wapambe wa wanasiasa badala yake wahakikishe wanatumia nafasi zao kuendelea kuihubiri amani na utulivu uliopo hapa nchini.

Habari hii imeandaliwa na ELIZABETH HOMBO (DAR), AMINA OMAR (TANGA), DOTTO MWAIBALE (SINGIDA) NA RAMADHAN HASSAN (DODOMA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles