24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

JPM: Jecha apewe tuzo

Rais Dk. John Magufuli akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Gombani, Pemba jana.
Rais Dk. John Magufuli akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Gombani, Pemba jana.

* Amchokonoa Maalim Seif ndani ya ngome yake

* Amtaka Shein kuacha upole vinginevyo aombe amsaidie

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

RAIS John Magufuli amependekeza Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, apewe tuzo kwa kusimamia uchaguzi vizuri.

Kiongozi huyo ambaye yupo katika ziara visiwani Zanzibar ya kuwashukuru wananchi baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwezi uliopita, aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Gombani ya Kale mkoani Kaskazini Pemba.

“Nampongeza sana mheshimiwa Jecha kwa kusimamia uchaguzi na umeenda vizuri sana na kama kuna tuzo mheshimiwa Shein (Rais wa Zanzibar Dk. Mohammed Shein) utazitoa umpe Jecha,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa na umati wa wana-CCM waliokusanyika kumsikiliza.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli imekuja wakati kukiwa na vita baridi kati ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad na mgombea wa CCM, Dk. Shein.

Katika vita hiyo, Maalim Seif ameendelea na msimamo wake wa kutotambua uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 21 mwaka huu ambao ulimpa ushindi Dk. Shein huku CUF wakisusia uchaguzi huo.

Oktoba mwaka jana siku chache baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha aliufuta uchaguzi huo kwa madai ya kuwepo kasoro kubwa, hatua ambayo ilipingwa vikali na CUF huku Maalim Seif akidai kuwa alishinda kwa zaidi ya asilimia 52.

Uamuzi wa Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi huo ulipingwa na baadhi ya wasomi wa sheria waliodai kwamba si tu ulikuwa ukikiuka misingi ya demokrasia bali kitendo cha kuamrisha kurudiwa kwake uchaguzi kinavunja sheria za nchi.

Uamuzi huo ndio uliosababisha nchi wahisani zipatazo 12 kutangaza kuondoa msaada wao katika bajeti ya Serikali.

Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC), ndilo lililokuwa la kwanza kuchukua uamuzi wa aina hiyo likiondoa msaada wake wa zaidi ya shilingi trilioni moja.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli licha ya kuwahi kukaririwa akisema kuwa hana mamlaka ya kuingilia suala la Zanzibar zaidi ya kuhakikisha kunakuwa na amani, jana alizungumzia suala hilo la uchaguzi wa marudio akiusifia na zaidi akimpiga vijembe Maalim Seif pasipo kumtaja jina.

Katika msingi huo huo mbali na Jecha, Rais Magufuli pia alivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa uzalendo waliouonyesha wakati wa kipindi cha uchaguzi.

“Mlitanguliza masilahi ya Tanzania kwanza, nyinyi ni wazalendo wa kweli tembeeni kifua mbele mimi kama Amiri Jeshi Mkuu nitaendelea kuwalinda kwa nguvu zote,” alisema.

Akisisitiza alisema uchaguzi wa marudio wa Zanzibar ulifanyika kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ibara ya 11 inayoipa mamlaka ZEC kama  chombo huru kisichoweza kuingiliwa na mtu yeyote ndiyo maana hata yeye hakuingilia mchakato huo.

Alisema kwa sasa wananchi wanapaswa kujua kuwa uchaguzi umeshakwisha na hakuna kitakachobadilika mpaka 2020.

Alisema kama kuna mtu tofauti anategemea kupata urais katika kisiwa hicho kabla ya mwaka 2020 ajue anaota ndoto za mchana ambazo hazitatimia.

Bila kutaja jina lakini kauli hiyo ikionekana dhahiri kumlenga Maalim Seif, kiongozi huyo alisema kuna watu wanazunguka huku na huko wakiwadanganya wananchi  kuwa uchaguzi utarudiwa ili waweze kuongoza Zanzibar na hali wanajua haitawezekana.

“Wengine wanasema uchaguzi utarudiwa, sisi Wasukuma na Wanyamwezi huwa tuna msemo kwa kawaida ndoto huwa ni usiku unaweza ukaota usiku umeota mabawa, kama ni mwanaume utaota unacheza mpira, hizo ni ndoto za usiku, lakini ukimkuta mtu anaota mchana, huyo anatafuta ukichaa.”

Akisisitiza katika hilo, alisema ukimkuta mtu anazungumza uchaguzi utarudiwa ama atakuwa rais katika kipindi cha miaka hii ana matatizo.

“Uchaguzi umeshakwisha …ulale unaota, unatembea, unazunguka, ufuge ndevu, chana nywele lakini uchaguzi ni 2020 huo ndio ukweli na lazima nieleze kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu, watazunguka wee wataenda kwenye kumbi zisizo na watu watakuja kuwaeleza nani anashtakiwa nani ashtakiwe uchaguzi umeshakwisha,” alisema.

Akizungumzia watu aliodai wanaleta chokochoko zinazoashiria kuharibu amani, Magufuli alimtaka Dk. Shein kupitia vyombo vya dola kuhakikisha anawashughulikia.

“Dk. Shein inawezekana umekuwa mpole sana kidogo, hebu huo upole upole uweke pembeni, fanya kazi kwa niaba ya Watanzania, una sapoti yangu yote atakayekuchezea chezea ukiona unamshindwa niambie hata kwakuninong’oneza kwamba hapa bana jaribu kidogo hazitapita hata dakika tano,” alisema.

Aliwataka wakazi wa Pemba kuwaogopa watu wanaochokoza amani kuliko shetani na wawakemee ili waweze kutekeleza ahadi ya kudumisha Muungano.

“Nasema yale tuliyoahidi tutayasimamia yote na kwa maana hiyo nina uhakika hatajitokeza mtu awe kwa sababu ya moyo wake wala ametumwa na watu kutoka nje aje kuchezea amani atacheza yeye, atakapojaribu kuchezea amani nakuhakikishia rais atacheza yeye tena mchezo ambao hajawahi kucheza,” alisema.

Alisema ifike mahali Watanzania tuambizane ukweli kwakuwa watu wamechoka ghiliba za ovyo ovyo  na wanahitaji maendeleo ili waende mbele na si kuendekeza mambo ya vyama.

“Tumeumbwa na Mungu tuishi kwa raha ukimpenda wa CCM kaoe CUF nenda Chadema hapo hapo, ukiona soko la CCM kanunue, hayo ndiyo tunayoyataka  atakayejaribu kuchezea hii amani hiiiiiiii, wanaofanya chokochoko  tunawajua wengine na tunaogopa kuwataja, polisi, usalama wa taifa wafuatilieni, anzeni na wanaochoma choma na kukata kata vitu vya watu washughulikiwe wote  bila huruma,” alisema.

Aliwataka wananchi washiriki kuwataja wanaochezea amani kwakuwa  wakiendelea kukaa kimya nchi inaweza ikaingia katika machafuko huku akitolea mfano wa nchi za Libya, Somalia na nyingine ambazo zimewahi kuingia katika machafuko.

“Katika nchi za Afrika zilizokuwa na raha mojawapo ilikuwa Libya, wakajitokeza watu wachache wakatumiwa tumiwa na kuahidiwa ahadi za uongo leo hapakaliki wanakimbia kwenda kuzama katika Bahari ya Mediteranea hapakaliki kila siku wanamwaga damu unajua hata raha zinalevya, hao walichezea amani,” alisema Magufuli.

Akizungumzia uchumi, Rais Magufuli alisema kisiwa cha Zanzibar kina nafasi kubwa ya kukuza uchumi wake kwa sababu ya uwepo wa bahari ambayo ina rasilimali nyingi zisizotumika.

“Bahari yetu hatujaitumia vyakutosha…visiwa vya Shelisheli uchumi wake unategemea uvuvi, lakini sisi hapa hatuna kiwanda kikubwa cha kuprocess samaki, nawaomba Watanzania  wakiwemo wanaopenda kuhubiri kuvunjika kwa amani wawaite wale wawekezaji waje kujenga viwanda vya samaki hapa,” alisema Magufuli.

Alisema ujenzi wa viwanda vya samaki utachangia vijana wa Pemba kupata ajira pamoja na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kuwa wahusika watapata fursa ya kusafirisha vitoweo hivyo nje ya nchi ambapo zitapatikana fedha za kujenga miundombinu.

Alisema wananchi wa Pemba wanahitaji maendeleo na si masuala ya siasa kwakuwa hawawezi kula vyama vya siasa.

Akizungumzia mkakati wa kufufua uchumi wa viwanda, alisema upo pale pale  huku akisisitiza nchi lazima iwe na amani ili ipate wawekezaji.

Alisema hakuna mtu atakayeweza kuwekeza katika viwanda mahali ambapo kuna vurugu, wananchi hawasalimiani, hawana amani kwa sababu ya vyama.

“Wananchi hawana amani, baba CCM mtoto CUF hawaelewani, mke wako CCM mwanaume CUF hamuelewani sasa sijui usiku mtalalaje kwenye kitanda, haya mambo tuyapige vita kwa nguvu hayana faida.

“Mna bahati mna Rais mpole sana na hata sura yake nzuri tu na ni Rais aliyetoka Pemba, ni kitu gani kinatusumbua mnataka malaika aje atawale hapa, mmepewa rais mpole mwaminifu hana majivuno mpenda watu na anampenda mke wake, watoto na wananchi, mimi namfahamu mpeni ushirikiano,” alisema Magufuli.

Katika hilo aliwataka wananchi kutokubali kurubuniwa na maneno ya uongo kwakuwa hakuna watakachoweza kubadilisha.

“Msikubali kuhubiriwa na maneno matamu matamu, kuna mtu anaondoka hapa anaenda Dar es Salaam anajifungia, sisi wa kule tunamuona na anakuja hapa  anasema ametoka Ulaya wakati sisi wa Dar es Salaam tunamjua anasema nimezungumza nao mambo yatakuwa sawa msikubali kudanganywa, tumedanganywa sana tusikubali tumechelewa,” alisema Magufuli.

Wakati Rais Magufuli akisema hayo, Juni mwaka huu Maalim Seif alikwenda nchini Marekani kwa ajili ya kuuelezea ulimwengu kilichotokea Zanzibar na mwelekeo wa demokrasia.

Julai mwaka huu, Maalim Seif na timu yake alikwenda nchini Uholanzi ilipo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa ajili ya kuwashtaki viongozi aliodai wanaminya demokrasia visiwani Zanzibar.

Katika safari hiyo, Maalim Seif alipeleka vielelezo kadhaa ikiwamo uvunjaji wa haki za binadamu huku ikitarajiwa mawakili wa ICC kuendelea na utaratibu wa kimahakama.

Katika ziara yake hiyo ya jana mbali na kupuuza kile kinachoonekana kufanywa na wapinzani,  Rais Magufuli alielezea ndoto yao ya kutaka kuijenga nchi ndani ya kipindi kifupi.

“Tukijenga umoja tukashikamana katika kipindi kifupi Pemba itakuwa kama Ulaya, tunaiharibu sisi wenyewe na wanaoharibu Pemba ni watu wachache sana muachane nao,” alisema Magufuli.

Rais Magufuli ambaye aliwasili kisiwani Pemba  kwa ndege ya  Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) akiwa na mke wake Mama Janeth, kabla ya kufanya mkutano huo alizuru kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais Dk. Omar Alli Juma, lililopo  katika Kijiji cha Wawi Bigilini, Wilaya ya Chakechake, Pemba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles