27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Ya Vikindu yafumukia Lushoto

Mtz Saturdaynew.indd

NA OSCAR ASSENGA, TANGA

MAJAMBAZI zaidi ya 15 yamevamia Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (Sekomu) kilichopo Kata ya Magamba, Lushoto mkoani Tanga na kuua mlinzi mmoja, kumjeruhi mwingine baada ya kumpiga risasi begani, kuchoma mabweni na kuharibu mali za wanafunzi waliokuwepo chuoni hapo.

Tukio la majambazi hao kuvamia chuo hicho limetokea usiku wa kuamkia jana wakati hali ya taharuki ikiwa bado haijasahaulika kwa wakazi wa Vikindu wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani baada ya usiku wa kuamkia Ijumaa ya wiki iliyopita Kikosi Maalumu cha Jeshi la Polisi cha Kupambana na Uhalifu kupambana na genge la watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi au magaidi waliokuwa wakiishi katika nyumba iliyopo eneo hilo.

Wakati tukio la chuoni hapo nalo likiibua shaka, hofu na maswali baada ya majambazi hayo kutoiba chochote licha ya kutekeleza uhalifu huo, lile la Vikundi ambalo msingi wake ulikuwa ni operesheni ya kuwasaka majambazi waliowaua askari wanne wiki iliyopita waliokuwa wakibadilishana zamu ya kulinda Tawi la Benki ya CRDB lililoko Mbande wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, likiwa limegubikwa na utata na sintofahamu huku Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Uhalifu, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Thomas Muniko, akiuawa kwa kupigwa risasi.

Licha ya majambazi hayo kutekeleza tukio hilo baada ya kuvamia na kufunga milango kwa nje na kumwaga mafuta na kuchoma moto mabweni huku baadhi ya wanafunzi wakipiga kelele za kuomba msaada na wengine kufanikiwa kutoka kupitia madirisha ya vyoo, lakini Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, amesisitiza kuwa kilichotokea chuoni hapo ni ujambazi na si ugaidi.

Akizungumzia tukio hilo jana kwa waandishi wa habari akiwa chuoni hapo, Wakulyamba, alithibitisha kuwa lilihusisha majambazi kati ya 10 hadi 15 waliovamia chuoni hapo na kuchoma vyumba vya mabweni mawili tofauti ya wanafunzi.

“Tukio hilo ni la ujambazi na si ugaidi. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa itakaa kikao na kulijadili tukio hilo kisha tutatoa taarifa,” alisema.

Wakulyamba alisema katika tukio hilo mlinzi mmoja wa chuo hicho, Yohana Shemzigwa (34), aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito mgongoni na kichwani huku mlinzi mwenzake, Abuu Rajabu, naye amejeruhiwa na majambazi hayo baada ya kupigwa risasi begani.

Pia alisema kuwa majambazi hayo yaliteketeza kwa moto mabweni mawili na kusababisha magodoro, nguo na simu za viganjani za wanafunzi wa chuo hicho kuungua.

Wakulyamba alisema mmoja kati ya majambazi hayo alijeruhiwa vibaya wakati akitekeleza unyama huo baada ya walinzi wa chuo hicho kutaka kumkamata na amepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto chini ya ulinzi wa polisi huku akiwa mahututi.

Katika hatua nyingine, alitangaza msako wa kuwasaka majambazi hayo ili kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili kujibu tuhuma zinazowakabili.

“Niseme kuwa sisi kama Jeshi la Polisi tutawatafuta wahusika wa tukio hili popote walipo usiku na mchana, wawe mapangoni au nchi kavu lazima tutawakamata na kuwafikisha katika vyombo vya kisheria ili waweze kujibu tuhuma zinazowakabili,” alisema Wakulyamba.

WANAFUNZI WASIMULIA

Akisimulia tukio hilo jana mmoja kati ya wanafunzi wa chuo hicho, Elizabeth Thobias, alisema lilitokea saa tano usiku wakati wakiwa mabwenini huku wengine wakijiandaa kwenda kujisomea na kulazimika kutoroka ndani ya mabweni hayo kwa kupitia madirisha ya vyoo.

Elizabeth alisema majambazi hayo yalifika chuoni hapo saa nne usiku na kuanza kuondoa vifaa vya kupoozea moto na kufunga milango kwa nje jambo lililowapa wakati mgumu walipotaka kujiokoa.

“Majambazi hayo yalipofika chuoni kabla ya kuanza kutekeleza ujambazi wao walisikika wakijadiliana kwa kuambiana watuchinje kwanza au watuchome moto, mmoja kati yao alisikika akisema moto tu unawatosha. Baada ya kuanza kuchoma moto ndipo tukaanza kukimbilia na kujiokoa kupitia madirisha ya vyoo vya mabweni,” alisema Elizabeth.

Tanga imekumbwa na matukio kadhaa katika siku za nyuma likiwamo lililotokea Februari, mwaka huu baada ya vikosi vya polisi na vile vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupambana na majambazi yaliyojificha katika Mapango ya Amboni na tukio jingine lilitokea Mei, mwaka huu baada ya polisi kuwaua majambazi wanne walioweka kambi katika mapango hayo.

Pia wakazi wengine wanane wa jijini Tanga walichinjwa na watu wasiojulikana katika tukio lililotokea Juni, mwaka huu katika Kitongoji cha Kibatini kilichopo Kata ya Mzizima

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles