30.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 2, 2022

Contact us: [email protected]

JPM: Inakuja mitano ya ajira kwa vijana

 NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amesema asilimia 65 ya Watanzania ni vijana, hivyo ameahidi miaka mitano ijayo atashughulikia tatizo la ukosefu wa ajira kwa nguvu zote.

Akizungumza jana wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Kinyerezi, alisema ana mikakati mizuri ya kuendelea kuyanufaisha makundi maalumu kama ya wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu ili kuboresha maisha na kuwaletea maendeleo.

“Kama tumeweza kujenga ‘ma–fly over’, kununua ndege, meli, siwezi nikashindwa suala la ajira kwa vijana ambao ndio tegemeo la taifa la kesho.

“Sizungumzi kwa kufurahisha, nataka taifa hili lisihesabike kama taifa la uchumi wa kati tu, walione kama mataifa mengine yaliyoko Ulaya. Uwezo huo upo, madini, bahari, maziwa, mlima mrefu na mti mrefu uko Tanzania, kwahiyo, tunataka kwenda mbele.

“Mimi huwa naumia ninapoona kina mama, vijana na wazee wananyanyaswa, kina mama wanateseka kwenye mirathi… nitatembea na kina mama, ndiyo maana nimeamua kumchagua tena Samia anisaidie kushughulikia masuala ya kina mama,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema atafanya mambo matano katika Wilaya ya Ilala yenye majimbo ya Segerea, Ilala na Ukonga ili kuiwezesha kuwa na maendeleo zaidi.

Mambo hayo ni kuondoa ubovu wa barabara na miundombinu mingine, kero ya maji, umeme, mafuriko na mgogoro wa ardhi baina ya Hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi na kata kadhaa za wilaya hiyo. 

“Mwaka huu tumejipanga kufufua miradi mingi zaidi, tupo ‘serious’ kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi hii na kero nyingi zimo katika ilani ya uchaguzi, naomba mniamini Watanzania na wana Ilala,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema zaidi ya Sh bilioni 32 zimetengwa kujenga kingo za Mto Msimbazi ili kudhibiti mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Ilala.

Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, mkuu wa wilaya na katibu tawala kuhakikisha mradi wa maji unakamilika kwa wakati ili ifikapo Desemba mwaka huu wakazi wa Kinyerezi, Bonyokwa na Kifuru wawe wanapata maji.

“Kama kuna waziri wa maji na katibu mkuu wanisikilize, hiyo ni amri yangu, nataka Desemba Kinyerezi, Bonyokwa na Kifuru wawe wanakunywa maji, ndiyo maana nataka mniletee wabunge na madiwani ili niweze kuwauliza kama maji yameshaletwa,” alisema Dk. Magufuli.

Kuhusu umeme, alisema licha ya mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi I na Kinyerezi II kuwepo katika wilaya hiyo, lakini baadhi ya maeneo bado yana shida ya umeme.

“Kinyerezi I na Kinyerezi II umezalisha umeme zaidi ya megawati 425, haiwezekani watu wa karibu na eneo la Kinyerezi unakotoka hawana umeme. Msongola, Chanika, Zingiziwa, Buyuni na Pugu hayana umeme wa kutosha, tupeni tumalizie hii kazi kwa sababu tunaijua na pesa zipo za kutosha,” alisema Dk. Magufuli.

Pia aliahidi kushughulikia mgogoro wa ardhi ambao unahusisha Hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi na kata kadhaa za wilaya hiyo zikiwemo za Chanika na Zingiziwa.

Dk. Magufuli alisema ameishi Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 30, anazifahamu changamoto zake na kuwaomba wananchi wamwamini na kumchagua tena ili aweze kuzitatua.

“Dar es Salaam ninaijua, nimeishi miaka mingi, nimekuwa waziri kwa miaka 20, miaka yote nilikuwa Dar es Salaam, nilipokuwa nikisoma chuo kikuu kwa zaidi ya miaka sita au saba yote nilikuwa Dar es Salaam, miaka mitano ya urais nilikuwa Dar es Salaam kabla sijahamia Dodoma. Kwa hiyo ukijumlisha yote utakuta ni zaidi ya miaka 30, hivyo shida za wana Dar es Salaam nazifahamu.

“Kwenye DMDP (Mradi wa kuboresha miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam) zimetolewa Sh bilioni 660 kwa ajili ya Dar es Salaam peke yake, bado unaendelea, ndiyo maana tunaomba kura ili katika miaka mitano inayokuja tufanye maajabu katika majimbo haya,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema pia ataboresha mazingira ya kufanyia biashara na kwamba vitambulisho vya wajasiriamali vitaendelea kutolewa kwa gharama ya Sh 20,000 kwa mwaka huku akiwataka wawe huru kufanya shughuli zao popote wanapotaka.

“Nimewapa wafanyabiashara wadogo wadogo jeuri ya kuishi katika maeneo yao bila kubugudhiwa,” alisema Dk. Magufuli.

MIRADI YA MAENDELEO

Dk. Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa katika Wilaya ya Ilala ambayo inajumuisha pia ujenzi wa masoko ya kisasa maeneo ya Kisutu, Bombom, Kigilagila na Minazi Mirefu na kwamba ujenzi wa machinjio ya kisasa unaendelea Vingunguti ambao unagharimu Sh bilioni 12.5.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, machinjio hiyo itakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 1,000 na mbuzi 500 kwa siku.

Alisema Sh bilioni 2.2 zimetumika kufanya upanuzi katika Hospitali ya Rufaa ya Amana ambao unahusisha pia ujenzi wa wodi ya mama na mtoto.

Dk. Magufuli alisema vimejengwa vituo vya afya Buguruni na Gulukwalala na kwamba zaidi ya Sh bilioni 2.4 zimetolewa kununua vifaa tiba katika zahanati za Luhanga, Mbondole, Bangulo na Lubakaya.

Kwenye elimu, alisema Sh bilioni 13.6 zimetumika kutoa elimu bila malipo katika Wilaya ya Ilala, na kwamba yamejengwa pia madarasa 269 na kununua madawati 13,505 kwa shule za msingi wakati kwa upande wa sekondari yamejengwa madarasa 1,040 na kununua madawati 18,006.

JIMBO LA SEGEREA

Dk. Magufuli alisema baadhi ya majimbo likiwemo la Segerea maendeleo yalichelewa kwa sababu kata zote 13 zilichukuliwa na upinzani, hivyo kukosa ushirikiano wa kutosha.

“Nilipokuwa nikiomba urais ahadi nilizotoa, nikitoa nilikuwa nina imani nazo, kubadilisha Wilaya ya Ilala na Dar es Salaam yake yote, hayo ndiyo yalikuwa malengo yangu.

“Baada ya uchaguzi yapo maeneo mlichanganya, jimbo hili (Segerea) mlichanganya, hamkunipa uhuru kufanya kazi, nafahamu maisha ya wana Segerea yalivyokuwa. Leo mabadiliko yamepatikana, lakini kwa shida sana,” alisema Dk. Magufuli.

Aliwaomba Watanzania kuwachagua wagombea wa CCM ili abaki na deni la kuwaletea maendeleo kwani walioteuliwa walichujwa kwenye Kamati Kuu, NEC, mikoa na wilaya zao.

“Changamoto zinatakiwa kutatuliwa na sisi sote, naomba mniletee wabunge na madiwani ili nibaki na deni kwenu, nipitishieni ili dhamana yangu na upendo nilionao kwa wana Dar es Salaam niweze kutimiza vizuri bila vikwazo.

“Ninaomba katika miaka yangu mitano iliyobaki, mnipe kura za kutosha, kushinda kwa Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM lazima mkapige kura, nawaomba Watanzania wote, vyama vyote maendeleo hayana chama,” alisema Dk. Magufuli.

UMOJA WA KITAIFA

Katika mkutano huo, pia Dk. Magufuli alisema taifa limesimama kwa sababu ya misingi mizuri iliyoachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na waasisi wengine na kuwataka Watanzania kuendelea kushikamana pamoja na kuepuka mbinu zozote zenye lengo la kuwagawa.

Alisema alipoingia madarakani changamoto ya kwanza aliyoanza kupambana nayo ni kushughulikia vitendo vya uhalifu ili kuleta amani na utulivu, huku akitolea mfano wa baadhi ya matukio yaliyotokea Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kagera.

“Nawaomba sana tujenge umoja wetu, taifa hili wanalionea gere, miaka ya nyuma mataifa ya Afrika yaligawiwa kwa wazungu, sisi kuna wakati tulitawaliwa na Wajerumani, baadaye tukatawaliwa na Waingereza.

“Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliposhika madaraka mwaka 1961, alilijenga taifa la Tanzania, aliamua kuungana na Zanzibar ndipo Tanzania ikaundwa, lengo lilikuwa kuijenga Tanzania ili kila Mtanzania atambue yuko huru,” alisema Dk. Magufuli.

 CORONA

Dk. Magufuli alisema kipindi ambacho kilimpa ugumu katika utawala wake ni changamoto ya ugonjwa wa corona, lakini alisimama imara.

“Katika kipindi nilichopata ugumu ni hicho, nikaona nitumie ‘knowledge’, nikapima papai nikakuta lina corona, nikapima kwale nikakuta ana corona. Nikasema huu ni mchezo mchafu, nikasimama nikasema njia pekee ni kumtegema Mungu na akajibu kwa haraka sana.

“Nataka niwaambie sasa ndiyo mambo mazuri yanakuja, watatumia mbinu za kila aina, lakini mimi nina imani Watanzania tuko pamoja na Mungu wetu kwa ajili ya kuikomboa nchi yetu kiuchumi. Tusimame imara kama taifa, tusibaguane tuko kwenye vita ya uchumi na kulitengeneza taifa,” alisema Dk. Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,509FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles