24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

NEC yaijibu Chadema karatasi za kura

 MWANDISHI WETU – DODOMA

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imejibu madai yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu mchakato wa zabuni ya kuchapisha karatasi za kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Majibu ya NEC yamekuja siku tatu baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuwaambia waandishi wa habari kuwa tume hiyo imekiuka utaratibu wa kupata mzabuni wa kuchapisha karatasi hizo.

Mnyika aliitaka tume kuweka wazi mambo matatu, ilikochapisha karatasi za kupigia kura, pili kutoa daftari la kudumu la wapigakura lenye majina na picha na tatu kuwaruhusu kukagua mfumo wa kuhesabu kura. 

“Kuna jambo ambalo waandishi na umma wa Watanzania hawalifahamu, tarehe 8 Oktoba NEC iliitisha kikao cha kwanza cha Kamati ya Taifa ya Manunuzi na Logistics.

“Tafsiri yake toka mchakato uanze NEC imekuwa ikifanya taratibu za manunuzi bila kuhusisha vyama vya siasa hadi tarehe 8 Oktoba ilipoitisha kikao ambacho kimsingi ilikuwa kuvieleza vyama kama tume imefanya manunuzi,” alisema Mnyika.

Katika hilo, Mnyika alihoji mchakato ambao tume imeutumia pasipo kuvishirikisha tangu mwanzo vyama vya siasa katika manunuzi ya karatasi za kupigia kura.

MAJIBU YA NEC

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk. Charles Mahela jana, ilisema tume imebaini kuwepo taarifa ya upotoshaji kuhusu mchakato wa zabuni ya uchapishaji wa karatasi za kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na jina la mzabuni aliyeshinda zabuni hiyo. 

“Kwa mujibu wa Ibara ya 74(6)(b) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, NEC imepewa mamlaka ya kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa upande wa Tanzania bara. 

“Ili iweze kutekeleza jukumu hilo, tume imeweka mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba vifaa vya uchaguzi vinapatikana mapema, vinahifadhiwa vizuri, vinafungashwa kulingana na uhitaji na vinasafirishwa katika hali ya usalama hadi kwenye vituo vya kupigia kura,” ilisema taarifa ya NEC. 

Ilisema kufanikisha azma hiyo, tume iliandaa mpango wa manunuzi wa vifaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa mujibu wa kifungu cha 49 (2) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410, ikisomwa kwa pamoja na kanuni kwenye GN 446 ya mwaka 2013. 

Taarifa hiyo ilisema tangazo la fursa za zabuni la ujumla (General Procurement Notice) liliwekwa kwenye tovuti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Julai 2, mwaka jana na kurudiwa tena Desemba 13, mwaka huo huo, likiwa katika mfumo wa Taneps. 

Kwamba pia tume ilitangaza kwenye Gazeti la Serikali la Daily News la Julai 8, mwaka jana kwa ajili ya kuufahamisha umma kuhusu fursa za zabuni zitakazotangazwa baadae na tume. 

“Umma uliofahamishwa ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa wakiweno wale wa Chadema,” ilisema taarifa hiyo. 

Ilisema katika mpango huo wa manunuzi, zabuni 47 ziliorodheshwa ikiwemo Na. IE/018/2019-20/HQ/G/GE/13 iliyohusu uchapishaji wa karatasi za kupigia kura. 

“Njia ya kumpata mshindi iliyotangazwa ni ya ushindani wa wazi wa kimataifa (International Competetive tender). Hivyo, zabuni hiyo ilitangazwa na PPRA Machi 9, mwaka huu kwenye mtandao wa Taneps, ikarudiwa kutangazwa na tume kwenye gazeti la Daily News la Machi 10, mwaka huu, baadae gazeti la kimataifa la The East African la Machi 14, mwaka huu. 

“Ufunguzi wa zabuni hiyo ulifanyika Aprili 8, mwaka huu, jumla ya makampuni yaliyoshiriki yalikuwa ni matatu, yote yalitoka nje ya nchi. 

“Makampuni hayo ni M/s Ren-Form CC ya Afrika Kusini, M/s Ellams Products Limited ya Kenya na M/s Al Ghurair Printing and Publishing LLC ya Dubai,” ilisema taarifa hiyo. 

Ilisema baada zabuni kufunguliwa na kufanyiwa uchambuzi, M/s Ren-Form CC wa Afrika Kusini ilitangazwa na mamlaka husika (PPRA) kuwa mshindi. 

“Hivyo, mzabuni aliyetajwa kwenye taarifa za uzushi kwa jina la Jamana Printers hakuhusika popote kwenye mchakato huo,” ilisema taarifa hiyo. 

Ilisema kuwa wajibu na mamlaka ya kutangaza washindi wa zabuni za umma kwa mujibu wa Kanuni ya 235 na 236 za GN 446 ya mwaka 2013 iliyoandaliwa chini ya Sheria ya Manunuzi ya Umma, Sura ya 410, ni wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), ambayo huyaweka matokeo yote wazi ya washindi wa zabuni kwenye Tender portal inayopatikana kwenye tovuti yake www.ppra.go.tz na jarida lake (Tanzania Procurement Journal). 

 “PPRA ilifanya hivyo, na mshindi wa zabuni hiyo alitangazwa kwenye Tender portal na jarida hilo ambalo lipo wazi wakati wote kwa umma,” ilisema taarifa hiyo. 

Ilipiga vikali taarifa kuwa tume haikuishirikisha Kamati ya Kitaifa ya Manunuzi na Lojistiksi ambayo inajumuisha wajumbe kutoka vyama vya siasa katika hatua zote za manunuzi ya vifaa vya uchaguzi. “Tume inapenda umma ufahamu kwamba michakato ya manunuzi ya umma inasimamiwa na Sheria ya Manunuzi ya Umma, Sura ya 410, ambayo haitoi nafasi kabisa kwa kamati nyingine yoyote zaidi ya Bodi ya Zabuni ya Tume kusimamia michakato ya manunuzi kuanzia kuitisha zabuni, kupokea zabuni na kuzifungua, kufanya uchambuzi na kuidhinisha mshindi.

“Hivyo kamati ya manunuzi na lojistiksi ya kitaifa inahusishwa tu chini ya dhana ya uwazi na ushirikishwaji ambapo inaweza pale inapobidi kutoa maoni na ushauri kwa tume,” ilisema taarifa hiyo. 

Ilisema pamoja na nia njema ya tume kuvishirikisha vyama vya siasa kwenye eneo la upatikanaji wa vifaa vya uchaguzi kwa ajili ya kupokea ushauri wao, vyama vingi kikiwemo Chadema havikuteua majina ya wajumbe wa kuunda Kamati ya Kitaifa ya Manunuzi na Lojistiksi, licha ya vyama kuandikiwa barua na tume ya Juni 30, mwaka huu.

Kwamba kikao cha kwanza cha kamati hiyo kilichofanyika Oktoba 8, mwaka huu Chadema na baadhi ya vyama vingine vilikuwa havijateua na kuwasilisha kwenye tume majina ya wawakilishi wa kuunda kamati hiyo ya kitaifa. 

 “Mwenendo huu wa vyama vya siasa umesababisha kuchelewa kuanza kwa wakati shughuli za kamati hii,” ilisema taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,867FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles