22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

JPM aweka tena historia

Tanzania's President elect Magufuli addresses members of the ruling CCM at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam*Atangaza kusitishwa sherehe za Muungano April 26

*Asema bil 2/- zilizotengwa zitajenga barabara Mwanza

 

NA MWANDISHI WETU, CHATO

RAIS Dk. John Magufuli ameweka tena historia kwa kutangaza kufuta sherehe za maadhimisho ya mwaka huu ya Muungano ambayo hufanyika kila Aprili 26.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli ni wa pili kuufanya ambapo Novemba 23, mwaka jana alitangaza pia kusitisha sherehe za Uhuru ambapo aliagiza siku hiyo itumiwe kwa ajili ya kufanya usafi wa mazingira kutokana na nchi kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa pamoja na kufutwa kwa sherehe hizo, badala yake Rais Magufuli ameelekeza kuwa siku hiyo itakuwa ya mapumziko kama kawaida na Watanzania waiadhimishe wakiwa majumbani kwao ama katika shughuli zao binafsi.

“Kuahirishwa kwa shamrashamra hizo, Rais Magufuli ameelekeza kuwa fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya kugharamia vinywaji, vyakula, gwaride, halaiki, burudani mbalimbali na hafla ya usiku ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 2, zitumike kuanzisha upanuzi wa barabara ya Mwanza – Airport katika eneo linaloanzia Ghana Quarters hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

“Barabara hiyo inafanyiwa upanuzi ili kukabiliana na kero ya msongamano mkubwa wa magari ambao unaathiri shughuli za kila siku za wananchi,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Rais Magufuli kwa sasa yupo nyumbani kwake wilayani Chato kwa mapumziko.

Sherehe za Muungano zinafanyika Aprili 26 ya kila mwaka kukumbuka Tanganyika na Zanzibar zilivyoungana na kuwa nchi moja.

 

ALIVYOFUTA SHEREHE ZA UHURU

Novemba 23, mwaka jana, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali, Balozi Ombeni Sefue, alitangaza uamuzi wa Rais Magufuli wa kufuta sherehe za maadhimisho ya Uhuru, na badala yake kuwataka Watanzania kutumia siku hiyo kusafisha mazingira nchi nzima ili kuondokana na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu.

Mbali na hatua hiyo, Rais Magufuli pia aliagiza kiasi cha Sh bilioni 4 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hizo zinazofanyika Desemba 9 kila mwaka, zitumike kupanua barabara ya Bagamoyo jijini Dar es Salaam, kuanzia Mwenge hadi Morocco.

WACHAMBUZI WAZUNGUMZA

Kutokana na uamuzi huo wa Rais Magufuli kufuta sherehe za mwaka huu za maadhimisho ya Muungano, wanasiasa, wasomi na viongozi wa dini wametoa maoni yao.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya awamu ya tatu, Profesa Simon Mbilinyi, alisema kuwa anaungana na uamuzi wa Rais Magufuli na hauna athari yoyote inayoweza kujitokeza kwa kusitisha sherehe za Muungano.

“Uamuzi wa rais ni mzuri na Muungano ulikuwepo tangu siku nyingi, hivyo shamrashamra hazina athari zozote na badala yake kinachotakiwa ni kuuheshimu na kuutunza basi,” alisema Profesa Mbilinyi.

 

PROFESA SAFARI

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Profesa Abdallah Safari, alisema ni uamuzi mzuri uliofanywa na rais kwa kuwa watu walizoea kufanya sherehe hizo kama sehemu ya kujipatia fedha kwa masilahi binafsi.

Alisema sherehe zilikuwa ni nyingi, hivyo kusitishwa kwa sherehe za Muungano kutapunguza gharama zisizokuwa na ulazima.

“Mimi namuunga mkono Rais Magufuli kufuta sherehe hizo kwani zilikuwa nyingi na watu walizoea kuzitumia kupiga dili kwa masilahi binafsi,” alisema Profesa Safari.

 

BASHIRU ALLY

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema uamuzi huo wa Rais Magufuli unatoa ujumbe wa aina mbili; kiuchumi na kisiasa.

Alisema Rais Magufuli yupo sahihi kutoa uamuzi huo kwa sasa kwa kuwa hakuna maana kufanya maadhimisho hayo huku bado Taifa likiwa tegemezi.

“Ni sawa kwa sababu anajenga uwezo wa ndani kwa kuzielekeza fedha hizo kwenye shughuli za maendeleo, na naamini kwamba katika bajeti tutaelezwa baadae kwamba hatua ya kufuta haya maadhimisho na safari za nje imesaidiaje.

“Lakini Muungano una faida gani na uhuru uko wapi ikiwa kwa mfano hatuna vitanda na dawa za kutosha kwenye hospitali zetu. Hivyo hapa kuna ujumbe wa kiuchumi na kisiasa, kwamba lazima tuangalie mambo yetu jinsi tunavyoamua,” alisema.

Alisema hata hivyo kazi iliyopo sasa kwa Serikali mbali na kubana matumizi, ni kujitahidi kuongeza uzalishaji wenye tija kwa jamii.

“Wakati Serikali inajitahidi kubana matumizi, lazima iongeze uzalishaji wenye tija ili ipatikane ziada na igawiwe kwa usawa kusudi maendeleo yapatikane, maana kama haya hayatazingatiwa itafika mahali wananchi watayachoka haya,” alisema Ally.

 

ASKOFU MWAMBALANGA

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Madhehebu ya Dini Tanzania, Askofu William Mwamalanga, alisema kwamba uamuzi huo umeacha maswali mengi.

“Awali alifuta sherehe za Uhuru, kwa maana hiyo huu ni uamuzi wa pili, lakini sherehe ina umuhimu wake… ni kumbukumbu ya Taifa lolote duniani kwa sababu huleta watu pamoja kama Taifa,” alisema.

Alisema hata hivyo licha ya sherehe hiyo kuwa na umuhimu kwa watu wote ameshangaa kitendo cha Rais Magufuli kuzipeleka fedha zitakazookolewa kujenga barabara ya Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Askofu Mwamalanga alisema kuwa ni vema fedha za kila sherehe ziwe zinagawanywa kwa usawa katika miradi ya maendeleo

“Zimeokolewa Sh bilioni mbili lakini amezipeleka kujenga barabara ya mkoa mmoja, hii inaleta ubaguzi kwa sababu kuna mahali wana tatizo la njaa, barabara na kwingine hakuna madawati, hii si haki,” alisema
Askofu Mwamalanga.

Imeandaliwa na Koku David, Florian Masinde na Veronica Romward

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles