23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AWAONYA WANAOJIPITISHA URAIS 2020

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli.

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli, amewageukia mawaziri ambao kwa sasa wanajipitisha kutaka urais mwaka 2020.

Amesema watu hao hivi sasa wameanza kujipitisha kutaka kumrithi Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kabla ya muda na kwa hatua hiyo huenda wakapoteza sifa.

Kauli hiyo aliitoa juzi Ikulu Dar es Salaam, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).

Kwa mujibu wa chanzo chetu, Dk. Magufuli aliwaonya makada hao wanaoanza kujipitisha kutaka urais wa Zanzibar kabla ya muda, huku akitaka Dk. Shein aachwe afanye kazi.

“Rais Magufuli alikuwa mkali sana, hasa ilipoletwa ajenda ya hali ya kisiasa Zanzibar, ambayo ilikuwa ikiangazia uchaguzi wa marudio na wana CCM waliosaliti chama.

“Alisema hivi sasa wapo mawaziri ndani ya CCM wameanza kujipitisha kutaka kumrithi Dk. Shein kabla ya wakati wake na akawaonya kuwa wamuache afanye kazi muda wake,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kilisema kutokana na hali hiyo, Dk. Magufuli alisema kuwa ili mtu awe rais ni lazima apitie taratibu zinazokubalika na chama na si vinginevyo.

Mawaziri na vigogo kadhaa wanatajwa na wana CCM kwamba huenda wakajitosa katika kinyang’anyiro cha urais wa Zanzibar mwaka 2020 wakiwamo Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni na Waziri wa Miundombinu wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume.

Nahodha alikuwa mmoja wa vigogo waliojitosa mwaka 2010 kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais, lakini alikuwa mshindi wa tatu akipata kura 33, nyuma ya Dk. Mohamed Gharib Bilal aliyepata kura 54 na Dk. Shein aliyeibuka mshindi kwa kura 117.

 

MATOKEO UCHAGUZI PEMBA

Mbali na hilo, pia katika ajenda hiyo ya hali ya kisiasa Zanzibar, iliwasilishwa taarifa ya namna chama hicho tawala kinavyoteswa na matokeo ya uchaguzi wa wabunge na wawakilishi kwa majimbo ya Pemba.

Kutokana na hali hiyo, juzi NEC iliagiza kuundwa kamati maalumu ya kufanya tathimini ya kina kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar kwa ujumla na masuala yanayohusu uchaguzi wa 2015.

Wakati hayo yakiendelea, leo Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar, Dk. Shein, anatarajiwa kuongoza kikao cha Kamati Maalumu ya NEC.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar – Idara ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakar Jabu, ilisema kikao hicho cha kawaida cha siku moja kitafanyika Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Alisema kikao pamoja na mambo mengine, kitapokea na kujadili mapendekezo ya wanachama wa CCM, wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani.

“Kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya NEC, ambacho kimefanyika leo (jana) chini ya Mwenyekiti wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, kwa lengo la kuandaa agenda za kikao hicho,” alisema Waride katika taarifa yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles