24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ATOBOA SIRI YA KUVUNJA BODI TRA

john-magufuliNA GUSTAPHU HAULE, Kibaha


 

RAIS   Dkt. John Magufuli ameeleza  sababu  za kuvunja Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  kuwa ni pamoja na kubaini  ubadhirifu wa Sh  bilioni  26.

Alitoa kauli hiyo jana katika  mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)  yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Rais pia alitaja Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima  kuwa ni taasisi nyingine  ambayo imekuwa na tabia ya kuchukua fedha za miradi na kuweka katika akaunti ya muda mrefu(Fixed account)  ili  waweze kugawana.

Alisema  fedha hizo katika akaunti ya TRA zilikuwa zimetolewa lakini baadaye zikachukuliwa tena jambo ambalo alilitilia shaka.

Dk. Magufuli  alisema hali hiyo ilionyesha kutokuwapo    uaminifu ndiyo maana aliamua kuchukua uamuzi wa haraka wa kuvunja bodi hiyo ili uchunguzi zaidi ufanyike.

Alisema zipo taasisi nyingi za umma ambazo zinapewa fedha za miradi na matokeo yake zinapelekwa katika akaunti za muda mrefu.

Rais alisema Mamlaka ya Elimu ya Watu Wazima ndiyo vinara wa jambo hilo na ameitaka taasisi hiyo na nyingine kuacha tabia hiyo mara moja.

Alisisitiza kuwa    fedha zinazotolewa zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Rais  pia alimtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuhakikisha wastaafu wote wa Chuo Kikuu Huria wanalipwa mafao yao  haraka.

Alisema  ingekuwa vizuri kama wangeweza kulipwa  ndani ya wiki mbili.

‘”Waziri wa Elimu naomba mshirikiane na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.  Phillip Mpango kuhakikisha wastaafu hao wawe wamelipwa mafao yao ndani ya wiki mbili  kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima  nchini,” alisema .

Rais  alisema   wakati anaendelea na jitihada  mbalimbali  za kuimarisha utawala bora nchini amekumbana na changamoto nyingi  ambazo zimekuwa  zikitokana na baadhi ya watendaji wa Serikali wasio waaminifu.

Hata hivyo aliahidi kuzimaliza changamoto hizo katika muda mfupi ujao.

Alizitaja  baadhi ya changamoto hizo   kuwa ni pamoja  vikwazo vya  utekelezaji wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, watumishi hewa,wanafunzi hewa na kuwapo kwa kaya masikini  ambazo zimeorodheshwa kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) huku zikiwa hazina vigezo.

Kuhusu sera ya elimu bure, alisema  kwa kipindi cha mwaka jana baada ya Serikali kuanzisha mpango huo,   wanafunzi milioni moja waliandikishwa.

Alisema idadi hiyo  imekuwa ikiongezeka   na hadi kufikia mwaka huu wanakaribia kufikia wanafunzi milioni mbili.

“Baada ya ongezeko hilo tulipofanya utafiti tulibaini kuwapo   majina ya wanafunzi hewa  zaidi  ya 65,000  ambao Serikali ilikuwa ikiwalipia gharama zote    kila mwezi wakati hawapo.

“Sasa unaweza kuona kuwa kweli watu walikuwa wanapiga dili jambo ambalo halipaswi kufumbiwa macho,”alisema.

Alisema   awali bajeti ya Serikali ilikuwa ni  Sh bilioni 340 na iliongezeka hadi kufikia Sh bilioni.473  huku idadi ya wanafunzi ikiongezeka kutoka 98,000 hadi kufikia  124,389.

Alisema baada ya ongezeko hilo la wanafunzi wa elimu ya juu,  ulipofanyika uhakiki ilibainika  kuna mikopo hewa   ya Sh bilioni 3.5.

Rais alisema  hadi sasa Sh  trilioni tatu  zilizokopwa na wanafunzi wa elimu ya juu   hazijarejeshwa.

“Wapo watu na viongozi fulani  walizoea maisha ya dili, walikuwa wanajichotea fedha kwa mipango ya udanyanyifu ndiyo maana leo wengi wanasema Serikali imebana fedha.

“Sasa ukimuuliza mshahara hupati, anasema anapata, lakini jiulize kama mshahara anapokea huo ugumu wa maisha unatokana na nini? “alisema.

Alisema   katika kuhakikisha anasafisha uozo huo ataendelea kutumbua majipu yaliyosalia bila ya kumwonea  mtu haya wala aibu ili  rasilimali za nchi ziwanufaishe wananchi wote .

Naye  Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Elifaz Bisanda alisema   chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo ukosefu wa majengo  jambo ambalo limekuwa likizorotesha ufanisi katika utendaji wa kazi

Alisema   ingawa chuo kinatoa mchango  mkubwa  kwa taifa kwa kutoa wasomi wengi ambao ni tegemeo la taifa,   hakijapata ruzuku kutoka Seriakalini jambo linalokilazimu   kujiendesha kupitia ada za wanafunzi.

“Hatujapata ruzuku kutoka Serikalini na ada haiwezi kukidhi gharama za kuendesha chuo maana tangu chuo hiki kianzishwe ada haijawahi kupandishwa.  Bado gharama ni zile zile hivyo tunakuomba  liangalie hili,” alisema.

Akizungumza kwenye hafla hiyo,  Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako alisema   ataendelea kusimamia misingi na sera ya elimu nchini ili  Serikali iweze  kupata wasomi bora watakaolitumikia taifa kwa ukamilifu  na kuhakikisha mfumo wa utoaji wa elimu unazingatia vigezo vinavyohitajika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles