23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

MZEE WA UPAKO MATATANI DAR

*Adaiwa kumfanyia fujo jirani yake akiwa amelewa chakari


lusekeloHERIETH FAUSTINE Na FARAJA MASINDE – DAR ES SALAAM

 

MCHUNGAJI Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Dar es Salaam, Anthony Lusekelo, maarufu Mzee wa Upako, amekamatwa na polisi akituhumiwa kumfanyia fujo na kutishia kumuua jirani yake.

Tukio hilo lilitokea juzi maeneo ya Kawe wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, kuanzia saa 11 asubuhi hadi saa tatu alipochukuliwa na polisi wa Kituo cha Kawe.

Taarifa za mchungaji huyo kufanya vurugu, zilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, huku video aliyorekodiwa eneo la tukio, ikimuonyesha akiongea huku akionekana kama aliyelewa chakari.

Wakati wa tukio hilo, Mchungaji Lusekelo alikuwa ameegesha gari lake barabarani kiasi cha kusababisha usumbufu na foleni ya magari mengine.

Chanzo cha tukio hilo kinadaiwa ni kulipiza kisasi kwa jirani zake hao wanaoishi katika nyumba namba KAW/MZN/1348, ambao alidai wamekuwa wakimkebehi kuwa hafai kuwa mchungaji kwa sababu ya ulevi.

Licha ya baadhi ya watu kumsihi aondoke eneo hilo kutokana na hadhi yake, mchungaji huyo alikaidi, huku akiendelea kuongea kwa sauti iliyofanana na mtu mwenye kilevi.

Baadhi ya maneno yaliyosikika kwenye video hiyo tumeshindwa kuyaandika kutokana na maadili ya taaluma kwa kuwa si ya kawaida.

“Mjinga wewe, mimi ni zaidi ya askari na wewe ni mgambo, na si mgambo wewe ni raia tu.

“Umenitukana sana wewe mpaka leo nimeamua kuloana na mvua, usitoe gari hapo mshenzi sana wewe, na nikikuona mahali popote…, mshenzi kabisa, muangalie sana huyo,” alisikika Mchungaji Lusekelo akiongea kwa sauti.

Baada ya kuongea maneno hayo, ilisikika sauti ya mwanamke kutoka ndani ya uzio wa nyumba hiyo ikimjibu mchungaji huyo: “Huwezi, aniangalie kitu gani.”

Hata hivyo, hata watu mbalimbali walipomsihi aache kutoa lugha hizo za kejeli na aondoe gari lake lililokuwa limesababisha foleni, alikataa akisema hataliondoa hadi atakapokuja Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.

Baada ya purukushani hizo, polisi kutoka katika Kituo cha Kawe walifika eneo hilo saa tatu asubuhi, wakamchukua mchungaji huyo na kumpeleka kituoni.

Inadaiwa baada ya kufikishwa kituoni hapo, mchungaji huyo alipimwa kiwango cha ulevi na kukutwa 131, ambacho kinaelezwa kuwa ni kikubwa – ulevi wa kupindukia.

Ilipofika saa tano asubuhi, mchungaji huyo alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central), ambako huko nako inadaiwa alipimwa kilevi na kuonekana kushuka hadi kufikia 121.

MTANZANIA lilipomtafuta Kamishna Sirro ili kuzungumzia sakata la mchungaji huyo, alisema atalizungumzia leo katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Juni 5, mwaka huu, Rais Magufuli alikwenda kusali katika kanisa la Mchungaji Lusekelo na kuahidi kumjengea barabara inayoingia kanisani hapo.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi katika eneo hilo, walipinga uamuzi huo wa rais wakidai ni wa upendeleo.

 

KANISANI KWA LUSEKELO

MTANZANIA lilifika katika kanisa la Mchungaji Lusekelo lililopo Ubungo Riverside jana na kukuta kukiwa katika hali ya ukimya tofauti na siku nyingine.

Sehemu ya maulizo ambayo siku zote inakuwa wazi kwa ajili ya wageni ilikuwa imefungwa.

Mmoja wa walinzi ambaye alikuwa amevalia sare za bluu, alisema siku kama ya jana (Alhamisi) si ya ibada isipokuwa huwa na huduma ya ushauri alasiri.

“Siku ya leo (jana) huwa hakuna ibada ya maombezi kama siku zote, huduma inayopatikana ni ya ushauri tu,” alisema mlinzi huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles