23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ATOA ONYO KALI


Gabriel Mushi na Ramadhani Hassan - Dodoma    |   

RAIS Dk. John Magufuli, amesema kamwe Serikali haitomwonea huruma au aibu mtu yeyote kutoka ndani na nje ya nchi anayetaka kujaribu kuvuruga Muungano.

Ametoa kauli hiyo jana mjini hapa, alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza Uwanja wa Jamhuri kuadhimisha maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Tutashirikiana katika kuulinda na kamwe, narudia, kamwe hatutamwonea aibu au huruma mtu yeyote, awe wa hapa nchini au wa nje ya nchi, mwenye nia ya kuvuruga Muungano wetu.

“Pili, napenda kuwahimiza Watanzania wenzangu tuendelee kuitunza amani yetu, amani ni kitu muhimu, ni msingi wa maendeleo.

“Hivyo Watanzania tushirikiane katika kuulinda, msikubali kutumika na watu wachache wenye nia ya kuharibu amani yetu.

“Pia toeni ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama, kwani kwa upande wetu Serikali zote mbili tupo imara katika kulinda na kutunza amani hiyo,” alisema. 

MAFANIKIO YA MUUNGANO

Rais Magufuli alisema sio siri Tanzania imepata mafanikio makubwa kutokana na kudumisha Muungano ambao sasa umefikia miaka 54.

Alisema mafanikio hayo ni pamoja na kuimarisha Muungano na kuongeza idadi ya maeneo ya ushirikiano. Mwaka 1964 yalikuwa maeneo 11 ya ushiririkiano na sasa yamefikia 22 kwa mujibu wa sheria.

“Vilevile Muungano umeifanya nchi kuwa yenye sauti na nguvu, kuwa huru na kujiamulia mambo yetu, umeiwezesha nchi kutoa mchango mkubwa katika masuala mbalimbali ya kimataifa kwenye harakati za ukombozi na kusuluhisha migogoro.

“Umetuwezesha kupata mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Tanzania ya leo sio ile ya mwaka 1964 kwani tumeimarisha huduma za kijamii, taasisi za elimu na afya zimeongezeka maradufu,” alisema.

Aliwashukuru na kuwapongeza waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

“Nimefurahi kumwona mama mjane Fatuma Karume, ambaye ameweza kuhudhuria sherehe hizi, nawashukuru pia na mama Maria Nyerere.

“Natambua mchango wa marais wastaafu, Mwinyi, Mkapa, Kikwete, Salmin Amour, Amani Karume, Dk. Shein na makamu wa rais na viongozi wote wastaafu katika kuimarisha muungano wetu. Pia Watanzania wote kwa michango mbalimbali iliyowezesha mafanikio haya,” alisema. 

CHANGAMOTO ZA MUUNGANO

Rais Magufuli alisema hakuna jambo zuri lisilo na kasoro kwani Muungano una changamoto.

“Lakini kwa bahati nzuri pande mbili zimeweka utaratibu mzuri wa kushughulikia changamoto hizo.

“Nimpongeze mwenyekiti wa kamati ya kushughulikia masuala ya muungano, ambayo inashughulikia changamoto hizo, Mama Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, mawaziri na makatibu wakuu wa Serikali zote mbili, ambao ni wajumbe wa kamati hiyo.

“Ni matumaini yangu kuwa kamati hii itaweza kumaliza changamoto ndogondogo zilizobaki,” alisema.

Alisema kaulimbiu ya Muungano kwa mwaka huu inayosema “Miaka 54 ya Muungano wetu ni mfano wa kuigwa duniani, tuuenzi, tuulinde, tuumarishe na kudumisha kwa maendeleo ya taifa letu”, inaweza kutekeleza kwa vitendo dhamira ya waasisi wa Muungano.

“Kamwe pasitokee mtu yeyote wa kutamani kuvunja Muungano wetu. Aidha, tusikubali mtu au kundi au chama chochote kuchezea Muungano wetu, mimi na Dk. Shein tutaulinda Muungano kwa gharama zote.

“Naomba nichomekee machache pia kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa Muungano wetu ndio nguvu au silaha yetu kama taifa, hivyo kila mmoja wetu ana wajibu wa kulinda muungano huu.

“Wananchi mna wajibu wenu na Serikali ina wajibu wake, kwa upande wa Serikali niwahahakishie Serikali zote mbili ziko imara kulinda Muungano wetu,” alisema.

 DODOMA SASA JIJI

Rais Magufuli alitumia sherehe hizo za Muungano kuitangaza Manispaa ya Dodoma kuwa jiji kuanzia jana kwa mamlaka aliyonayo kikatiba.

“Niwahakikishie Watanzania kuwa azma ya Serikali kuhamia Dodoma iko palepale, hakuna kurudi nyuma na tayari watumishi 3,800 wameshahamia na mimi mwaka huu nahamia Dodoma. Ndio makao makuu.

“Tulizoea kuona Dar es Salaam kuwa makao makuu miaka ile na ikawa jiji vilevile, nikaona niangalie katika nchi yetu kuna majiji mangapi, manispaa ngapi, na mimi nina mamlaka gani katika kutengeneza majiji au manispaa, nikakuta Dar es Salaam ni jiji, Tanga, Mwanza, Arusha, Mbeya ni majiji, lakini cha ajabu nikaambiwa Dodoma ni manispaa.

“Nikasema hili haliwezekani, kwahiyo kuanzia leo kwa mamlaka mliyonipa Watanzania, Dodoma inakuwa jiji, kwa hiyo maandalizi yote ya jiji lazima yaanze, na huyu mkurugenzi wa manispaa kuanzia leo 26/4/2018 anakuwa mkurugenzi wa Jiji la Dodoma,” alisema.

Alisema Jiji la Dodoma litakuwa jiji la peke yake kwa sababu lipo katikati ya Tanzania.

WACHEKELEA JIJI, MUUNGANO

Viongozi na wanasiasa mbalimbali waliozungumza na MTANZANIA, walifurahia uamuzi wa Rais Magufuli kuifanya Dodoma kuwa jiji na kuahidi kutekeleza maagizo yake haraka.

Mmoja wa viongozi hao, Mkurugenzi wa jiji hilo, Edwin Kunambi, alishukuru kuteuliwa kuendelea kuongoza jiji hilo na kusema nafasi aliyopewa ni dhamana kubwa.

“Nafasi niliyopewa ni dhamana kubwa, kama kijana namwomba Mwenyezi Mungu anisaidie ili niweze kufanya kazi ya kuonekana mbele za watu na kuwatumikia walalahoi,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema wao kama manispaa waliishatimiza vigezo vya kuwa jiji muda mrefu.

“Dodoma ni tofauti na majiji mengine kwani hapa lazima mkumbuke ndio makao makuu ya nchi, lakini lazima nikiri nina changamoto ya kutimiza wajibu,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa mipango yao ni kuipitia ‘Master Plan’ ya mwaka 1976 ili jiji hilo liendane na kukidhi matakwa ya makao makuu. 

CHEYO

Akitoa maoni yake kuhusu hotuba ya Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic (UDP), John Cheyo, alisema alichokisema rais kuhusu amani, kila Mtanzania anatakiwa kuilinda.

Cheyo ambaye amewahi kuwa mbunge wa Bariadi Mashariki kupitia UDP, alisema amani ni tunu na kila mmoja anatakiwa kuilinda kwa nguvu zote.

“Kwa watu wa Dodoma, naamini leo ni siku ya furaha, lakini lazima wajishughulishe ili kuendana na hilo jina la jiji,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles