28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

CHADEMA, ACT WAZALENDO WAKACHA MUUNGANO


Gabriel Mushi na Ramadhan Hassan -Dodoma     |   

MAELFU ya wakazi wa Jiji la Dodoma, jana wamejitokeza kwenye sherehe za Muungano katika Uwanja wa Jamhuri, huku viongozi na wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT- Wazalendo wakikacha.

Viongozi wa upinzani waliojitokeza katika sherehe hizo ni Mwenyekiti wa Chama cha ADA-TADEA na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic (UDP), John Cheyo.

MKAPA AWAKILISHA MARAIS WALIOPITA

Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na viongozi wa Serikali, balozi za nchi mbalimbali, taasisi na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali, zilihudhuriwa pia na Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete hawakuhudhuria sherehe hizo.

Viongozi wengine waliohudhuria ni mke wa hayati Abeid Amani Karume, mama Fatma Karume, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ally Maulid na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. John Kijazi.

Wengine ni waziri pekee aliyesalia duniani katika Baraza la kwanza la Mawaziri wa Serikali ya awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere, Balozi Job Lusinde, mabalozi wa nchi mbalimbali zikiwamo za uarabuni, mawazi, manaibu waziri na wabunge.

Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Akinumwi Adesina akiwa na mwenyeji wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philp Mpango.

RAIS NA GARI LA WAZI

Licha ya wananchi kuzoea kumwona Rais Dk. John Magufuli akiwa katika gari la wazi pindi ahudhuriapo sherehe kama hizo, jana ilikuwa tofauti.

Rais Magufuli aliingia uwanjani hapo saa 3:18 asubuhi akiwa ndani ya gari, huku akipungia wananchi mkono kupitia dirishani na kisha kuanza kukagua gwaride.

Mara baada ya kukagua, uliimbwa wimbo wa taifa sambamba na kupigiwa mizinga 21 na kisha akaanza kuangalia maonyesho mbalimbali yaliyokuwa yameandaliwa.

WATOTO KIVUTIO

Katika sherehe hizo, watoto waliokuwa wakiigiza kama makomando waligeuka kivutio kutokana na kuruka vizuizi mbalimbali ikiwamo vya kukanyaga moto.

Watoto hao zaidi ya 2,000 kutoka shule 10 za Manispaa ya Dodoma, ambao baadhi walikuwa wamevalia sare za Jeshi la Wananchi, pia walipita mbele ya Rais Magufuli kwa mwendo wa kikakamavu na kuwafanya wananchi waliohudhuria kuwashangilia.

ULINZI WAIMARISHWA

Katika Uwanja wa Jamhuri pamoja na barabara za kuingilia uwanjani hapo, kulikuwa na ulinzi wa hali ya juu, huku kila aliyekuwa akiingia alikuwa akikaguliwa kwa kutumia mashine maalumu za ukaguzi.

Barabara ya kwenda Singida ilifungwa ili kuwaruhusu watembea kwa miguu kupita kiurahisi na kuweza kuingia uwanjani.

WANANCHI WAWAHI

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wakazi wa Manispaa ya Dodoma walijitokeza kwa wingi na hadi kufika saa 1 asubuhi tayari uwanja ulikuwa umejaa.

Lakini waandaaji waliandaa runinga kubwa nje ya Uwanja wa Jamhuri ambayo wale ambao hawakuingia uwanjani waliitumia kuangalia matukio yaliyokuwa yakifanyika ndani ya uwanja.

PAPII KOCHA AKUMBUKIA GEREZANI

Naye msanii wa muziki wa dansi nchini, Johnson Nguza, maarufu kwa jina la Papii Kocha ambaye alikuwapo uwanjani hapo na baba yake, Nguza Viking maarufu kwa jina la Babu Seya, alisema onyesho la askari Magereza wakiwazuia wafungwa wasilete fujo, limemkumbusha mbali.

Msanii huyo na baba yake, ambao mwaka jana walitolewa gerezani kwa msamaha wa Rais Magufuli, alisema machozi yalikaribia kumtoka mara baada ya kuwaona wafungwa wakiwa na mnyampara.

“Nimekumbuka mbali sana, hasa kipindi ambacho nilikuwa gerezani, hakika itabaki historia katika maisha yangu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,307FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles