22.7 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ARUHUSU KILIMO KANDOKANDO YA MITO

ASHURA HUSSEIN NaRENATHA KIPAKA-KARAGWE


RAIS Dk. John Magufuli, amepiga marufuku viongozi kuwazuia wananchi kulima mazao yao kandokando ya mito na kuwataka wawaunge mkono ili kupunguza migogoro isiyokuwa  ya  lazima.

Akipokea malalamiko kutoka kwa mkulima aliyejitambulisha kwa jina la Rosh Omary, kuhusu kufyekwa mazao yake aliyokuwa amelima kando kando ya Mto Nkenge eneo la Kyaka mkoani Kagera, Rais Magufuli aliuagiza uongozi wa Wilaya ya Misenyi kuhakikisha vijana wanalima bila kubughudhiwa na mtu yeyote hata kama ni katikati ya mto.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana Mjini Kayanga  wilayani  Karagwe mkoani Kagera  alipokuwa akizindua barabara ya  Kyaka-Bugene  yenye urefu wa kilometa 59.1 iliyogharimu  Sh bilioni 81.

Akiwasilisha malalamiko hayo kwa Rais, Omary alisema alikuwa anafanya shughuli zake za kujipatia kipato katika gereji ya magari lakini aliamua kuachana na shughuli hiyo na kwenda kuanzisha kilimo cha mahindi kandokando ya Mto Nkenge.

“Nimelima mazao yangu lakini yote yamefyekwa na viongozi wa Serikali wanadai ninaharibu chanzo cha maji na wakaamua kufyeka shamba langu,” alisema Omary.

Baada ya kumsikiliza kijana huyo, Rais Magufuli alimuagiza Omary na wananchi wengine wanaolima kandokando ya mito kuendelea na shughuli zao za kilimo na kuwataka viongozi wawaunge mkono ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima.

Mbali na Omary, Rais aliagiza wananchi 200 wanaoishi kwenye vyanzo vya maji wilayani Karagwe na kufukuzwa na uongozi wa wilaya hiyo, Serikali iwatafutie maeneo mengine ya  kuishi  na si kuwafukuza bila kuwatafutia sehemu mbadala wakati  makosa  mengine ni ya viongozi.

“Kama watu wanaanza kujenga kwenye vyanzo vya maji viongozi wapo wanaangalia na hawachukui hatua ni makosa ya  viongozi, kama wananchi hawapo karibu sana na chanzo cha maji msiwafukuze waacheni walime mazao yao kandokando ya mito wajipatie kipato.

“Tukisimamia sheria za mazingira kila mtu tutamfukuza lazima kila kiongozi  aangalie kama watu wanaharibu vyanzo vya maji ndani ya mita 60 iwe kwenye ziwa au bahari lakini mkitumia mita 60 hizo kila mto mtaendelea kuchochea  migogoro kwa wananchi bila sababu, kama nina mji wangu upo karibu na mto nisilime kweli,” alihoji Magufuli.

Rais Magufuli aliagiza wananchi waachwe walime kandokando ya mito wapate mazao na kipato kwa sababu mto umeletwa na Mwenyezi Mungu na haukuletwa na mkuu wa mkoa wala mkuu wa wilaya kwani maji yanatiririka kwenye mkondo wake.

Pia aliwaeleza wakazi wa Karagwe kuwa anafahamu na kuzitambua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwamo ukosefu wa maji, ambapo alisema kati ya miji 17 iliyoingizwa kwenye mpango wa mradi wa maji Tanzania, Karagwe ni miongoni mwa miji hiyo na watapata maji ya uhakika.

“Ili kutekeleza miradi hiyo tayari fedha zipo ambazo tumekopeshwa na serikali ya India Dola milioni 500, kati ya hizo Sh bilioni 70 zitapelekwa Karagwe kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji, najua mmeteseka muda mrefu na adha ya maji changamoto hiyo sasa itageuka kuwa historia,” alisema.

Awali Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bashungwa (CCM), alimwomba Rais Magufuli kumaliza kero ya maji iliyodumu kwa miaka mingi, huku akiutaja mradi wa maji wa wakajuju kwamba upo tangu serikali ya awamu ya tatu na haujawahi kuleta matunda yoyote kwa wananchi.

Pia mbunge huyo aliomba waongezewe vituo viwili vya afya kutokana na wilaya hiyo kuwa na kituo kimoja tu kinachohudumia wilaya nzima na kuwalazimu baadhi ya wakazi wa maeneo ya Nyakikika kutembea hadi kilomita 60 kufuata huduma za afya Kayanga.

Aidha katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliagiza barabara ya Kyaka-Bugene aliyoizindua jana kuendelea hadi wilayani Ngara mkoani humo kwakuwa kipande kilichobaki ni kidogo.

Naye Waziri wa Ujenzi,  Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema ujenzi wa barabara hiyo uliomalizika Juni mwaka huu umegharimu Sh bilioni 81.5 zilizotolewa na serikali na itaunganisha Tanzania na mipaka ya Mtukula (Uganda), Rusumo (Rwanda) na Kobero (Burundi).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles