24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

JPM aongoza wateule 16 kuwania urais

 RAMADHAN HASSAN -DODOMA

MGOMBEA urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli jana amewaongoza wagombea wengine wa kiti cha urais kurejesha fomu katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jijini Dodoma, na kupitishwa kugombea awamu ya pili.

Urejeshaji fomu jana ulisimamiwa kwa ukaribu na kuhakikiwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, ambapo kila mgombea aliporejesha alimsisitiza kufuata ratiba ya uchaguzi inayotaka kuanza kampeni leo hadi Oktoba 27.

Uchukuaji wa fomu za kuomba kuteuliwa na NEC kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulianza Agosti 5, mwaka huu jijini hapa ambapo Seif Maalim Seif wa Chama cha Wakulima (AAFP), alikuwa wa kwanza kuchukua akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Rashid Rai na baadhi ya wanachama wa chama hicho.

Katika tukio la jana, Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, aliongozana na mgombea mwenza wake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na baadhi ya viongozi wa chama hicho wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Bashiru Ally.

Rais Magufuli alikuwa wa kwanza kurejesha fomu ambapo alifika ofisi za NEC saa 2.35 asubuhi.

Akizungumza wakati wa urejeshaji wa fomu hizo, Rais Magufuli alisema ametii na kufuata taratibu za tume kama walivyoelekeza.

 “Tumetafuta wadhamini mikoa 10 kama tulivyoelekezwa na NEC, tuna ziada ya wadhamini wengine mikoa mitano, na hivyo kuwa 15, tumeweka ziada,” alisema Rais Magufuli.

NEC YAMPITISHA

Mkurugenzi wa NEC, Dk. Charles Mahera alisema wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais kupitia CCM, Dk. Magufuli na Samia Suluhu, wametimiza masharti ya uteuzi kwa kuzingatia vigezo vyote.

Alisema fomu za uteuzi zimejazwa kwa ukamilifu na wadhamini wamepatikana kwa idadi iliyotakiwa na ziada.

Dk. Mahera alisema wagombea wametoa tamko kwamba wanazo sifa za kugombea.

“Katibu Mkuu wa CCM, ametoa uthibitisho wa kuwateua wagombea, wagombea wamedhaminiwa na wapigakura kutoka mikoa 10 iliyokuwa inatakiwa na mitano mingine ya ziada, mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema Dk. Mahera.

Pamoja na hayo, alitaja vigezo vingine walivyonavyo wagombea wa CCM kuwa wasimamizi wa uchaguzi wamethibitisha majina ya wadhamini.

Alisema wagombea wametoa tamko mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu kuthibitisha wanazo sifa za kuteuliwa.

“Wagombea wamewasilisha stakabadhi ya malipo ya shilingi milioni moja ya dhamana, huku wakiwasilisha nakala nne za picha,” alisema Dk. Mahera.

 Alisema wagombea wametoa tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi kwa mwaka 2020 katika fomu namba 10. 

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi baada ya kujiridhisha kuwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais waliopendekezwa na CCM wametimiza masharti ya ibara 41(2), 39(1)(a)-(e), na ibara ya 47(4)(a)-(e) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa 

 pamoja na vifungu vya 30, 32, 33, 34 vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura 343 ya Sheria za Tanzania. 

“Kwa mamlaka iliyopewa chini ya kanuni 37(6) ya kanuni ya Uchaguzi wa Rais na Wabunge mwaka 2020, tume imewateua Dk. John Magufuli kuwa mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa kiti cha Makamu Rais.

“Kwa niaba ya tume tuwapongeze wagombea kupitia CCM, hatua inayofuata nitawakabidhi wagombea seti moja ya uteuzi fomu namba 8A, pamoja na nakala moja ya fomu namba 10 na nakala ya picha za wagombea,” alisema Dk. Mahera.

WENGINE WALIOPITISHWA

Wagombea wengine waliorejesha fomu na kupitishwa ni pamoja na Leopard Lukas wa Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), John Shibuda (Ada Tadea), Matamwega Mgaiwa (Sauti ya Umma – SAU), Cesilia Mwanga (Demokrasia Makini), 

Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Bernard Membe (ACT Wazalendo), Hashimu Rungwe (Chaumma), Yeremia Maganja (NCCR Mageuzi), Twalib Kadega (UPDP), Philip Fumbo (DP), Queen Sendiga (ADC), Seif Maalum Seif (AAFP), Khalfan Mohamed (UMD) na Tundu Lissu (Chadema).

PROFESA LIPUMBA

Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Profesa Lipumba alisema anaenda katika uchaguzi akiamini ameshinda kwani Watanzania wanahitaji mabadiliko. 

“Watanzania wanahitaji mabadiliko, wanatia huruma na vijana wanasema vyuma vimekaza, wanahitaji mabadiliko, tunahitaji kuwekeza kwenye afya, elimu na kuwekeza fedha za kutosha pamoja na kuweka mazingira kwa kufanya biashara kwani si mazuri, hivyo tunahitaji kuyarekebisha.

“Nchi yetu hatuna mfumo mzuri wa katiba ya vyama vya siasa na ikiwa tutashinda tutaweka katiba inayokubalika kwa pande zote mbili za muungano… Kukosolewa kunajenga na Serikali ya CUF itakubali kukosolewa

“Woga ni adui wa haki Watanzania tujitokeze kwa wingi, wote tuunge mkono kampeni zetu, wajue nchi yetu inaweza kujiendesha na tuweze kuipata Tanzania yenye furaha na haki siku zote.

“CCM si chama cha siasa, ni chama cha dola, watu wamekuwa waoga, hasa ndani ya CCM, hawajitokezi kujenga hoja, rai kwa Magufuli kama anahitaji uchaguzi kuwa huru na wa haki, basi asimame katika maneno yake, nchi yetu sote tujenge misingi bora na ya kidemokrasia,” alisema Lipumba.

PHILIPO FUMBO 

Mgombea wa Chama cha Democratic (DP), Philipo Fumbo alisema watadumisha mila za kitanzania kwani chama chao ni chuo cha siasa. 

“Chama chetu kinatetea walalahoi, pia kinadumisha mila na demokrasia, watu wamezoea kuona wagombea uraia wakivaa suti, wanasiasa wote wamepita, hiki ndicho chuo cha wanasiasa,” alisema Fumbo. 

MEMBE 

Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Membe aliishukuru tume kwa kufanya kazi vizuri, huku akidai umefika sasa wakati wa mabadiliko. 

“Mchakato huu ni mchakato ambao lazima ufanywe kwa makini, nimeona yaliyotendeka nchi hii kwa baadhi ya waombaji kutofanikisha azma yao ya kugombea.

“Nimeona umwagaji wa damu katika bara la Afrika, nimeona fujo ambazo zitafuta kabisa uchaguzi huu. 

“Uteuzi ni haki ya wananchi na hii ni zamu yao kuchagua wanayemtaka si kuchaguliwa na watawala, nafasi hii ni ya wananchi si nafasi ya utawala kuwapa maelekezo watu wanaokuja kuchukua fomu. Dhambi hii itatutafuna na tutakuja kujuta siku moja,” alisema Membe.

Alisema uzinduzi wa kampeni za ACT Wazalendo unatarajiwa kufanyika mkoani Lindi.

LISSU 

Mgombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu alifika ofisi za NEC, akitumia gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe.

Lissu alishuka na kupokewa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na mgombea mwenza wake, Salum Mwalim, kisha kuwasalimia waandishi.

Aliingia saa 6 mchana ofisi za tume ambapo alikaa muda mrefu ndani bila waandishi wa habari kuelezwa sababu ni nini.

Saa 1.43 usiku, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Kaijage alimtangaza kuthibitishwa kuwa mgombea urais baada ya kupitia na kuhakiki fomu zake. 

“Tume ya Uchaguzi imehakiki na inawathibitisha kuwa wagombea katika Uchaguzi Mkuu ujao na mtatakiwa kupewa na kujaza fomu za kuheshimu maadili ya uchaguzi,” alisema Jaji Kaijage.

CCK, NLD WAONDOLEWA

Wagombea wa vyama vya CCK na NLD wameondolewa katika kinyang’anyiro cha urais kutokana na kushindwa kukidhi vigezo.

Akizungumza baada ya kupokea fomu kutoka Chama Cha Kijamii (CCK), Jaji Kaijage alisema wamekiondoa kutokana na wagombea wake wa nafasi ya urais, Mwaijojele Daud na makamu wake, Ally Said Ally kutotimiza masharti ikiwemo kutokujaza baadhi ya fomu.

“Wagombea wa CCK hawakutimiza masharti yote ya kikatiba. Kwa mamlaka iliyopewa, tume haijawateua ndugu Mwaijojele Daud kuwa mgombea wa nafasi ya urais na ndugu Ally Said Juma katika nafasi ya Makamu wa Rais. Tume haina budi kuwapongeza,” alisema Jaji Kaijage. 

MAJALIWA APITA BILA KUPINGWA 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana ametangazwa na NEC kupitia msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kupita bila kupingwa nafasi ya ubunge wa Jimbo la Ruangwa.

Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Frank Chonya alisema mgombea wa CCM, Majaliwa ndiye pekee aliyekidhi vigezo vilivyowekwa na tume na kumfanya apite bila kupingwa.

Akizungumza baada ya kutangazwa, Majaliwa aliwashukuru wana CCM, viongozi na wanachama wa vyama rafiki na wana Ruangwa kwa ujumla kwa heshima waliyompatia na kumwezesha kupita bila kupingwa.

“Wana Ruangwa wote bila kujali siasa zetu, tunajua tulikotoka na wilaya hii tunajua changamoto tulizonazo, tunajua hatua tuliyoifikia sasa hivi na kauli zenu zilikuwa zinaangalia tunakokwenda na uwezekano wa kutatua changamoto huko mbele,” alisema Majaliwa.

 KAMPENI KUANZA LEO

Katika hatua nyingine, kampeni za urais, ubunge na udiwani zinazinduliwa rasmi leo, baada ya wagombea kukamilisha urejeshaji w a fomu jana.

Mkurugenzi wa NEC, Dk. Mahera alisema kuwa kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, baada ya wagombea kukamilisha urejeshaji wa fomu na kuthibitishwa, tume imetoa muda wa siku moja kuwakilisha mapingamizi na kushughulikiwa.

Alisema kuanzia leo, wagombea ambao watakuwa hawana pingamizi watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuanza kampeni na kwa wale ambao watakuwa na pingamizi watakuwa tayari wameshashughulikiwa na majibu yao kutolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles