26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

JPM aibua hoja uchaguzi Z’bar

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amewataka Wazanzibar kutorudia makosa yaliyojitokeza miaka ya nyuma, wakati wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Alisema miaka ya nyuma amani ilitetereka katika visiwa hivyo na kufikia hatua ya watu kuwekeana vinyesi katika maji, lakini sasa wako watu ambao hawalali kuhakikisha hali hiyo haijirudii tena.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa hoteli yenye hadhi ya nyota tano ya inayomilikiwa na Kampuni ya Bakhresa, Magufuli aliwataka wananchi wajitathmini mahali walikotoka, watambue waliko na wanakoelekea.

“Nchi yetu ikiwemo Zanzibar tumepitia katika mlolongo mkubwa, miaka ya nyuma amani ilitetereka katika kisiwa hiki. Ilifikia mahali watu wanaweka vinyesi mpaka kwenye maji ya kunywa, inawezekana wengine mmeshasahau, lakini hayo ndiyo maisha tuliyapitia.

“Katika hali ya namna hiyo, pasingeweza kufanyika uwekezaji kama huu. Inawezekana hata hoteli hii ingekuwa inanuka vinyesi, ninachowaomba Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla tuitunze amani yetu.

“Palipo na amani kila kitu kinawezekana, utapata watalii wengi watakaokuletea fedha, hivyo tuitunze amani, kamwe tusirudie katika enzi ambako amani ilishindwa kupatikana,” alisema Rais Magufuli.

Alisema licha ya hatua zilizopigwa kwa sasa, vibaraka na watu ambao hawapendi visiwa hivyo viwe na amani, bado wapo na akatahadharisha watu wote bila kujali itikadi zao kuitunza amani iliyopo.   

“Wale ambao wangependa nchi hii isiwe na amani wapo na vibaraka hawaishi. Wako watu ambao kazi yao ni kubeza tu hata ungembeba wapi, watu ambao hawana shukrani. 

“Na saa nyingine mnaweza kufanya uchaguzi mwingine akawa anazungumza nitaapishwa tu, msubiri nitakuja kuapishwa.

“Watanzania wa vyama vyote tunahitaji maendeleo, utulivu, tunahitaji kujenga uchumi wa nchi yetu. Kalisimamieni hili, uwe CUF, CCM, ACT… Maendeleo hayana chama, tukalizingatie hili katika mustakabali wa taifa letu,” alisema.

DHAMIRA YA MAPINDUZI

 Kuhusuhoteli hiyo, alimpongeza Mwenyekiti wa Kampuni za Bakhresa, Said Salim Bakhresa, kwa kujenga hoteli hiyo na kuwekeza katika sekta nyingine ndani na nje ya nchi.

“Tumezoea kufungua miradi ya watu waliotoka nchi zingine, leo unakuja kufungua mradi mkubwa wa Watanzania wenzako, ni raha sana,” alisema Magufuli.

Alisema ujenzi huo ni utekelezaji wa dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibari yanayotaka nchi ijikomboe kiuchumi na kumwomba Bakhresa awafundishe Watanzania wengi namna ya kuwekeza pamoja na kuleta wawekezaji wengine ambao ni waaminifu.

“Watanzania wote tuige mfano wa Bakhresa, hakuzaliwa tajiri, alizaliwa masikini, lakini aliamua kufanya kazi kwa bidii akawa mvulimivu na leo ni miongoni mwa matajiri wakubwa.

“Sisi si masikini, tukiamua tunaweza, nilikuwa Malawi, DRC, Kenya nikaambiwa kuna miradi yake, lakini nina uhakika hakuzaliwa hivi.

“Ninafahamu shughuli zake alizokuwa anazifanya kule Dar es Salaam, kazi aliyoweza kuifanya, mtu yeyote anaweza kuifanya tukiamua, wawekezaji si lazima watoke nje,” alisema Rais Magufuli.

WAWEKEZAJI HUJENGWA

Pia aliwataka viongozi wa Serikali zote mbili kutowakatisha tamaa wawekezaji wa ndani, hata kama wanaanza kidogo kidogo kwani wawekezaji hujengwa.

“Bakhresa alijengwa, ninafahamu wapo Watanzania wana fedha nyingi tu wanaogopa kuwekeza hapa, wanakwenda kuwekeza nje na wengine wanakwenda kuzificha nje. 

“Ukifa hizo fedha zitaliwa huko huko, wenye fedha wawekeze hapa, ukiwekeza hapa unajenga mazingira mazuri ya watu kufaidi uwekezaji wako. Hata kama fedha uliziiba, lakini zitasaidia Watanzania wengine,” alisema Magufuli.

Pia alitahadharisha hoteli hiyo isije kuwa lango la watu kufanya biashara mbaya, ikiwamo ya dawa za kulevya kwani itapoteza heshima yake.

“Vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kuongeza nguvu ili maeneo ya Tanzania yasiwe lango la biashara za ovyo kwani zinaharibu vijana na kuchelewesha maendeleo.

“Tutaendelea kulinda usalama wa wawekezaji na Watanzania wote na yeyote atakayejaribu kuchezea usalama wa Watanzania atakuwa amechezea mahali pabaya,” alisema Magufuli.

MAPINDUZI YATALINDWA  

Awali akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Mwanakwerekwe iliyopo Unguja, alisema atahakikisha Mapinduzi yanaendelea kudumu bila kuchezewa na mtu yeyote kwani ndiyo yameifanya Zanzibar iwe na amani.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli aliwahamasisha viongozi mbalimbali kuwachangia vijana waliokuwa wakitoa burudani na zaidi ya Sh milioni 50 zilichangwa zikiwa ni fedha taslimu na ahadi huku yeye mwenyewe akichangia Sh milioni 2.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,663FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles