23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

JKCI: Tumeokoa Sh bilioni 89 kwa miaka minne

Mwandishi wetu-Dar es Salaam

SERIKALI imeokoa zaidi ya Sh bilioni 89 kwa wagonjwa 5.954 wenye matatizo ya moyo ambao walifanyiwa upasuaji wa kufungua na bila kufungua kifua katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kipindi cha miaka minne.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi wakati akielezea mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano kwa upande wa matibabu ya moyo katika kikao cha bodi ya wadhamani ya taasisi hiyo.

Profesa Janabi alisema kama wagonjwa hao waliofanyiwa upasuaji nchini wangetibiwa nje ya nchi, Serikali ingetumia zaidi ya Sh bilioni 178 kulipia gharama za matibabu hayo.

Alisema kwa wagonjwa hao kutibiwa hapa nchini, matibabu yao yamegharimu Sh bilioni 89 fedha ambazo zimelipwa kupitia bima zao za matibabu, misaada ya wafadhili mbalimbali wa nje, wagonjwa wenyewe kujilipia na Serikali kugharamia matibabu ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.

“Gharama ya mgonjwa mmoja aliyefanyiwa upasuaji nje ya nchi ni zaidi ya Sh milioni 30, lakini kwa mgonjwa mmoja kutibiwa hapa nchini gharama zake hazizidi Sh milioni 15.

“Kwa kutibiwa hapa nchini fedha anazolipa mgonjwa zinatumika kununua vifaa tunavyomuwekea katika moyo wake kama vile pacemaker, high power device, stent, device closure na valvu. Vifaa hivi tunaviagiza nje ya nchi kwani havipatikani hapa nchini,” alisema Profesa Janabi.

Alisema kwa kipindi cha miaka minne wameona wagonjwa 300,836 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na nchi jirani kama vile Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Ethiopia, Zambia, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Comoro.

 “Jambo la kufurahia ni kuwa tumeweza kuokoa maisha ya watu ambao tumewatibu, na hivi sasa wanaendelea na majukumu yao ya kazi za kila siku.

“Kwa kipindi cha miaka minne tulilaza wagonjwa 14,960 tumefanya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab kwa wagonjwa 4,207 na upasuaji wa kufungua kifua na kusimamisha moyo kwa wagonjwa 1,747,” alisema Profesa Janabi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI ambayo inamaliza muda wake, Profesa William Mahalu, aliupongeza uongozi wa taasisi hiyo pamoja na wafanyakazi kutokana na huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa kwa wagonjwa wanaowatibu.

Profesa Mahalu ambaye ni mmoja wa madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa kwanza hapa nchini, alisema anamaliza muda wake kama mwenyekiti wa bodi hiyo, huku ndoto yake ya kuona Tanzania inakuwa na hospitali ya  matibabu ya moyo ikiwa imetimia.

 “Ukiangalia idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi yetu imeongezeka kutoka 150 kwa mwaka 2016 hadi kufikia 300 kwa siku kwa mwaka 2019,” alisema Profesa Mahalu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles