23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mtaalamu aeleza matumizi holela ya dawa yanavyosababisha vifo

AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

MRATIBU usugu wa vimelea dhidi ya antibiotiki, Dk. Siana Mapunjo, amesema matumizi ya dawa za antibiotiki kiholela ni hatari kutokana na kusababisha vimelea vinavyosababisha usugu wa dawa.

Hata hivyo ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Chakula Duniani (FAO) zinasema takribani watu 700,000 kila mwaka wanapoteza maisha duniani kote kutokana na usugu wa dawa.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika maadhimisho ya Wiki ya Matumizi ya Antibiotiki iliyoanza jana, Dk. Mapunjo alisema ni bora sasa watu wakazingatia matumizi bora ya dawa ili kuepukana na usugu wa dawa.

“Tafiti zinaonyesha kuwa nchi zinazoendelea zipo hatarini zaidi kuenea kwa usugu wa dawa, hivyo kwa sasa hii ni agenda ya dunia kwani usugu wa dawa ni vimelea vinavyosambaa. Mwaka 2015 FAO ilitoa wito kwa kila taifa kupambana na usugu wa dawa.

“Matumizi ya dawa holela ni hatari kwani unapotumia dawa hovyo unaweza kupata vimelea hivyo, mfano kuna mtu anatumia dozi halafu anaacha ikiwa nusu, hali hii inapelekea wadudu wasiishe, hivyo wanaobaki wanakuwa sugu hawatibiki kwa dawa.

“Na pia kuna wale ambao wao wanatumia dawa bila maelekezo ya wataalamu hii inaweza kusababisha usugu pia.

“Ni vema sasa watu wakaacha desturi ya kutumia dawa hovyo kwani sio kila ugonjwa unahitaji matumizi ya antibiotiki, hivyo kuna haja ya kuepuka matumizi ya antibiotiki ya mara kwa mara,” alieleza Dk. Mapunjo.

Alisema kuwa watu ambao wanatumia dawa nyingi wako hatarini kupata usugu wa dawa, kwani matumizi ya mara kwa mara ya antibiotiki yanaweza kusababisha kushuka kwa kinga.

“Unavyokunywa dawa nyingi ndivyo unavyokuwa hatarini, unaweza kupata ‘fangas’ kwa sababu ya kinga kushuka, madhara kwenye figo, tatizo hili la usugu wa dawa watafiti wanasema tahadhari isipochukuliwa itaua watu wengi kuliko hata kansa.

“Hivyo kwa sasa tunachokihamasisha kwa watu ni matumizi ya dawa na uhifadhi mzuri kwani hii ndio njia pekee ya kupambana na tatizo la usugu wa dawa,” alibainisha.

Kwa upande wake, Daktari wa Mifugo Mkuu, Sero Luwongo, alisema kuwa asilimia 75 ya magonjwa yanayoathiri binadamu yanatokana na wanyama hasa wanyama wa porini.

“Utafiti unaonyesha ifikapo 2030 tutakuwa na magonjwa 10 yanayotokana na wanyama, sasa hivi yako sita ambayo ni malale, kimeta, mafua ya ndege, kichaa cha mbwa, homa ya bonde la ufa na ugonjwa wa kutupa mimba kwa wanyama.

“Kutokana na utafiti huo, ni bora sasa watu wakazingatia matumizi ya dawa kwa wanyama, wapewe dawa kulingana na maelezo ya wataalamu na watu wayazingatie hayo maelezo,” alisema Dk. Luwongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles