29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

JK: Fungeni masoko ya pembe za ndovu

9-IMG_3156Na Mwandishi Maalumu, New York

 

RAIS  Jakaya Kikwete, ametoa changamoto kwa wabunge wa Bunge la Marekani kufunga masoko ya pembe za ndovu na faru duniani, kama njia ya kukomesha ujangili dhidi ya wanyamapori katika nchi za Afrika.

Rais Kikwete, amewataka wabunge hao kuzisaidia nchi za Afrika kifedha ili kukomesha ujangili huo, kwa sababu wabunge hao tayari wameitangazia dunia kuwa wanazo fedha za kutosha kwa ajili ya kukabiliana na ujangili.

Rais Kikwete alitoa changamoto hiyo juzi  usiku, wakati alipohutubia umoja wa wabunge wa Bunge la Marekani ambao wanalenga kulinda na kuhifadhi wanyamapori na uhifadhi duniani.

Mkutano huo pia ulilenga kujenga umoja wa kisiasa wa kukabiliana na ujangili na kutafuta majibu ya changamoto zinazokabili uhifadhi unaojulikana kama International Conservation Caucus Foundation (ICCF).

Akizungumza nao mjini New York, Marekani, ambapo alikuwa anafanya ziara ya kikazi, Rais Kikwete kama kweli wabunge wa Marekani wakiamua kutumia nguvu za taifa lao kubwa duniani kufunga masoko ya meno ya ndovu na pembe za faru, tatizo hilo litamalizika haraka.

ICCF inafanya kazi kwa karibu na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Zambia, Malawi, Gabon, Botswana, Msumbiji, Namibia, Congo-Brazaville na Afrika Kusini.

Miongoni mwa wageni waliokuwapo ni Peter Mutharika wa Malawi na Rais Ali Omar Bongo wa Gabon.

Katika hotuba yake, Rais Kikwete aliwaambia wabunge hao, kuwa nchi za Afrika pamoja na kufanya jitihada kubwa kukabiliana na kile alichokielezea kama “kiwango cha juu kabisa cha uendawazimu”  zina ukomo wa uwezo wa kifedha na nguvu katika kukomesha ujangili bila kusaidiwa na nchi kubwa kama Marekani.

“Nyie kama wabunge wa Marekani, mna uwezo mkubwa kama ilivyo nchi yenu. Fungeni masoko ya pembe za ndovu na faru. Wanunuzi mnawajua nyie wenyewe kuliko hata mimi. Wengi wenu mna fedha na nguvu nyingi kuliko sisi katika Afrika kumaliza tatizo hili.

“Sisi ni hadithi ya mkufu kukatikia pabovu. Timizeni wajibu wenu na kwa kweli ujumbe wangu mkubwa kwetu usiku wa leo (juzi), ni fungeni masoko haya na tatizo litaisha.

“Nimemsikia mama pale akisema ICCF ina kiasi cha dola bilioni 13.2 za kufanya kazi ya kukabiliana na ujangili duniani. Tunahitaji fedha hizi. Mnatamba mnazo fedha nyingi lakini sisi tulioko kwenye uwanja wa mapambano hatuzioni fedha hizo. Tupeni fedha tufanye kazi,” alisema.

Rais Kikwete alikuwa anazungumzia risala ya ICCF iliyokuwa imeeleza kuwa ICCF inazo fedha kiasi cha Dola za Marekani bilioni 13.2 za kukabiliana na changamoto za ujangili.

Rais Kikwete pia alitoa historia ya jinsi Tanzania imetoa kipeumbele kwa shughuli za hifadhi tokea uhuru mwaka 1961 na jinsi ambavyo imehangaika kukabiliana na ujangili katika miaka hiyo yote wakati mwingine kwa kulazimika kutumia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) kuendesha operesheni maalumu kuokoa wanyamapori.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles