30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Jeremy Menez akatika sikio uwanjani

JEREMYPARIS, UFARANSA

MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya AC Milan ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Bordeaux ya nchini Ufaransa, Jeremy Menez, juzi  alikatika sikio uwanjani.

Ni siku mbili tangu mchezaji huyo ajiunge na klabu hiyo akitokea klabu ya AC Milan. Menez amepoteza kipande cha sikio lake la kulia baada ya kuanguka chini na kukanyagwa na mchezaji wa klabu ya Lorient, Didier Ndong.

Tukio hilo lilitokea wakati kiungo huyo wa klabu ya Lorient mwenye umri wa miaka 29, akijaribu kumruka mchezaji huyo wakati anaanguka, lakini bahati mbaya akamkanyaga kwenye sikio na kukatika.

Klabu ya Lorient imetoa pole kwa mchezaji huyo mpya pamoja na klabu ya Bordeaux kutokana na tukio hilo ambalo litamfanya mchezaji huyo kuwa nje ya uwanja kwa muda.

Hata hivyo, Ndong ameomba radhi kwa mchezaji huyo kutokana na kitendo ambacho amekifanya bila kukusudia.

“Naomba radhi kwa mchezaji mwenzangu Jeremy Menez na klabu ya Bordeaux, ni wazi kwamba ilikuwa ni sehemu ya mchezo na sikukusudia kufanya hivyo.

“Nitahakikisha ninakuwa pamoja na mchezaji huyo kwa kipindi chote cha kuuguza jeraha na ninaamini ataonekana tena uwanjani muda mfupi ujao katika Ligi hii ya Ufaransa,” alisema Ndong.

Menez, ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa klabu ya Paris Saint-Germain, amejiunga na klabu hiyo mwanzoni mwa wiki hii kwa mkataba wa miaka mitatu na huo ulikuwa ni mchezo wake wa kwanza tangu ajiunge.

Mchezaji huyo alitumia dakika 15 tangu kuingia kwake uwanjani, huku timu yake ikifanikiwa kushinda mabao 3-1. Nyota huyo anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa sikio hilo.

Ligi Kuu nchini Ufaransa inatarajia kuanza kutimu vumbi Agosti 12 mwaka huu, huku klabu ya Bordeaux ikianza kwa mchezo wa kwanza kwenye uwanja wa nyumbani.

Hata hivyo, Menez amelielezea tukio hilo na kudai kuwa atakuwa uwanjani muda mfupi ujao.

“Sidhani kama Didier Ndong alikuwa na lengo la kunichezea vibaya, ilikuwa ni bahati mbaya baada ya kuanguka na yeye akaja kunikanyaga wakati wa kuwania mpira, hivyo sina tatizo na yeye.

“Ninaamini hali yangu itakuwa vizuri muda mfupi ujao na nitarudi uwanjani kwa ajili ya kuipigania timu yangu, mashabiki wasiwe na wasi wasi juu ya hali hii kwa kuwa ni jambo la kawaida katika maisha ya soka.

“Kuna watu wengine wanavunjika mguu na wanakaa muda mrefu nje ya uwanja, lakini kwa upande wangu ninaamini nitakuwa nje kwa muda mfupi na nitarudi uwanjani,” alisema Menez.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles