23.2 C
Dar es Salaam
Friday, June 9, 2023

Contact us: [email protected]

JAPANI YATOA SULUHISHO LA FOLENI DAR

Mwandishi wetu


SHIRIKA la Maendeleo la Japan (Jica), limetoa suluhisho la msongamano wa magari jijini Dar es Saalaam kwa kupendekeza kujenga barabara nyingine tatu za juu (fly over), mtandao wa reli na miji ya pembezoni.

Mapendekezo hayo ya Jica ni matokeo ya utafiti uliofanywa na shirika hilo kwa kushirikiana na Wazira ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Ripoti ya utafiti huo imeonyesha kuwa ifikapo mwaka 2040, idadi ya watu katika Jiji la Dar es Salaam itafikia milioni 12 kutoka milioni sita ya sasa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuwasilisha matokeo ya ripoti hiyo, Mwakilishi wa Jica Tanzania, Toshio Nagasa alisema ili kukabiliana na msongamano katika kipindi hicho ni muhimu Serikali ikafikiria kujenga reli.

Alisema moja ya faida ya reli ni uwezo wake wa kusafirisha watu wengi kwa pamoja tofauti na usafiri wa magari.

Nagasa alisema kujengwa kwa reli kutasaidia kupunguza magari binafsi barabarani, jambo litakalorahisisha shughuli za kiuchumi.

Katika ripoti hiyo, mbali na barabara za juu zinazojengwa Taraza na Ubungo, nyingine zinapaswa kujengwe katika makutano ya barabara ya Morocco, Chang’ombe na Mwenge.

Utafiti huo umependekeza kujengwa kwa miji midogo katika maeneo ya pembezoni ili kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji.

Mbali na mipango iliyopendekezwa na Jaica, serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kumaliza msongamano Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na mradi wa mabasi yaendayo haraka kutoka katikati ya jiji kwenda Kimara na awamu ya pili inatarajia kutoa huduma kutoka mjini kati kwenda Mbagala.

Pia serikali inapanga kutanua barababara ya kutoka Ubungo mpaka Chalinze kuwa ya njia sita.

Jana, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Spora Liana alisema wataalamu wa Jica wameshauri miji midogo itakayojengwa iwekewe huduma zote za msingi ili watu wengi wasilazimike kufika mjini.

“Wametuletea utafiti wao nasi tumeupokea, jukumu linabaki kwetu serikali kuona ni nini tunafanya kufanikisha utekelezaji wake,” amesema.

Agosti 15, mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na aliye kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Ichiro Aisawa kabla kiongozi huyo hajatembelea miradi inayojengwa na kampuni za Japan, ukiwemo ujenzi wa barabara za juu (Flyover) wa Tazara na mradi wa kuzalishaji umeme kwa gesi wa Kinyerezi.

Aisawa alisema baada ya kuona changamoto ya foleni katika Jiji la Dar es Salaam, amebaini kuwa nchi yake bado inahitaji kuendelea kushirikiana na Tanzania kuboresha miundombinu ya jiji na kuahidi  kufikisha ujumbe huo kwa Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe.

Rais Magufuli alimshukuru Aisawa kwa kuja Tanzania na kumhakikisha kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa ambao Japan inautoa katika maendeleo na itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Japan katika masuala mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,351FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles