22.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

JPM:SITETEI WAVAMIZI WA MAENEO

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli, amesema Serikali haiwezi kurudia kuwalipa watu ambao tayari walishalipwa fidia na hawezi kuwatetea kwa kuvunja sheria kwa kuvamia maeneo yasiyo yao.

Rais Dk. Magufuli, alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wananchi wa Mapinga wilayani Bagamoyo ambao walisimamisha msafara wake, wakati akienda kuzindua kituo cha Mafunzo Maalumu ya Kijeshi (Comprehensive Training Center CTC) kilichopo mkoani Pwani.

“Serikali haiwezi kurudia kuwalipa watu ambao tayari walishalipwa fidia na hawezi kuwatetea watu ambao wamevunja sheria kwa kuvamia maeneo yasiyokuwa yao.

“Serikali ina dhamira ya dhati ya kutekeleza mradi wa bandari na eneo la uwekezaji la Bagamoyo, watu wote waliolipwa fidia wakati hawakuwa na maeneo warejeshe fedha za Serikali.

“Waliolipwa fidia waondoke katika maeneo yaliyolipiwa na kwa wale ambao hawajalipwa fidia waendelee kutumia maeneo yao kwa shughuli zao mbalimbali,”alisema Rais Magufuli.

Awali katika madai yao, wananchi hao walimwomba Rais Dk. Magufuli awasaidie kulipwa fidia  kutokana na maeneo yao kuchukuliwa kwa ajili ya miradi, ukiwamo wa ujenzi wa kituo hicho cha mafunzo cha jeshi na kuvunjiwa nyumba zao katika eneo la Makurunge.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari  Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa, ilisema  kituo hicho kimejengwa kwa msaada kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China kwa gharama ya Shi bilioni 67.87.

Taarifa hiyo, ilisema kituo hicho kitatumika kutoa mafunzo ya kijeshi ya kisasa yatakayowawezesha askari kukabiliana na vitisho vya kisasa vya kiusalama.

Kabla ya kuzindua kituo hicho, Rais  Dk.Magufuli na Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke wameshuhudia makabidhiano ya kituo hicho kutoka Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China lililowakilishwa na Naibu Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Utawala ya Kamisheni Kuu ya Jeshi hilo, Jenerali Yang Jian kwenda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililowakilishwa na Meja Jenerali Yakub Hassan Mohamed.

Rais Dk. Magufuli, pia alishuhudia mazoezi ya kijeshi yaliyofanywa katika kituo hicho yakiwemo shambulizi la kutokea baharini (amphibian landing), makomandoo kukabiliana na magaidi na kupiga shabaha kwa kutumia miundombinu ya kisasa.

Akizungumza na maofisa,askari na wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio la makabidhiano ya kituo hicho, alilishukuru Jeshi la Ukombozi la Watu wa China  kwa kutoa msaada wa kujengwa kwa kituo hicho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo alisema miundo ya kituo hicho inakifanya kuwa kimataifa kilicho bora zaidi Afrika Mashariki na Kati kitakachoweza kutoa mafunzo ya kisasa kwa askari wengi.

Jenerali Mabeyo, alimwomba Rais Dk. Magufuli kusaidia ujenzi wa daraja la Mto Mpigi litakalokiunganisha  barabara ya kwenda Dar es Salaam.

Kutokana na hilo, Rais Magufuli alikubali ombi hilo la  Jenerali Mabeyo ya kupeleka maji, umeme na barabara katika eneo ambalo China imekubali kutoa msaada wa kujenga makao makuu ya JWTZ  mkoani Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,305FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles