23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

January: Tutawashawishi wadau watupe fedha za kusimamia mazingira

Na LULU MUSSA – DODOMA

SERIKALI imesema itaendelea na juhudi za kushawishi wadau wa maendeleo na jumuiya za kimataifa ili kupata fedha za kusimamia uratibu wa shughuli za mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2019/2020 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira. 

Alisema Tanzania ni mwanachama katika mifuko na mikataba mbalimbali duniani, hivyo kuna fursa za kunufaika na fedha zitolewazo na mifuko hiyo, akitoa mfano wa Mfuko wa Green Climate Fund.

Pia aliainisha mafanikio yaliyopatikana katika ofisi yake kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 kuwa ni pamoja na kufanya Mapitio ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 na mkakati wa utekelezaji wake, kuandaa rasimu ya Mpango wa Taifa wa Mazingira wa mwaka 2019-2023 na maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Viumbe Vamizi (Invasive Alien Species). 

Alisema katika kipindi cha mwaka 2018/2019, wamekamilisha rasimu ya mwisho ya Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini, baada ya kupata maoni ya wadau kabla ya kuwasilishwa bungeni kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

Alisema katika kuhakikisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira unazingatiwa, jumla ya miradi 1,254 ya maendeleo imefanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na Ukaguzi wa Mazingira pia, ili kuharakisha uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linatoa Kibali cha Awali cha Mazingira (Provisional Environmental Clearance) ili kuwawezesha wawekezaji kuendelea na maandalizi ya awali ya mradi. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Suleiman Sadick, aliupongeza uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa jitihada za kuhifadhi mazingira nchini. 

“Kamati inatambua jitihada za ofisi yenu katika kuhifadhi mazingira, sisi tunawaunga mkono,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,636FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles