24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Ripoti kuchunguza rushwa kwa trafiki yakamilika

PATRICIA KIMELEMETA NA CHRISTRINA GAULUHANGA

RIPOTI ya kamati maalumu iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kuchunguza rushwa kwa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani na ukiukwaji wa sheria imekamilika.

Akizungumza wakati wa kongamano la Kitaifa la Usalama Barabarani lililofanyika Dar es Salaam jana, Kangi alisema askari wa kikosi hicho wanapaswa kujitathmini na kusimamia sheria kabla uamuzi haujachukuliwa.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanapaswa kujiepusha na vitendo vya rushwa vitakavyoendelea kupoteza maisha ya watu.

“Kamati niliyoiunda kuchunguza vitendo vya ukikwaji wa sheria za usalama barabarani pamoja na rushwa imekamilika na kusubiri kuchukuliwa uamuzi, hivyo basi askari wa usalama barabarani wanapaswa kujitathmini kabla sijachukua uamuzi mgumu,” alisema Lugola.

Pia alisema askari wanaoishi kwa mazoea na kutotaka kubadilika siku zao zinahesabika.

Aliwataka wajumbe wa Baraza la Usalama Barabarani kufuatilia kwa umakini hoja zitakazotolewa na wadau ili waweze kuzifanyia kazi, hali inayoweza kusaidia kuboresha utendaji wa kazi za usalama pamoja na kupunguza ajali.

Kutokana na hali hiyo, alisema baraza hilo linapaswa kusimamia mpango mkakati wa nne ambao ni wa mwaka huu kuhakikisha unatekelezwa, ikiwa ni pamoja na kusimamia ukaguzi wa magari, mfumo wa ukaguzi ili kuweka msukumo wa mabadiliko ya sheria yanayolenga muundo wa baraza kuwa tendaji.

Naye Mwenyekiti Taifa wa Baraza la Usalama Barabarani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamad Masauni, alisema mwaka jana walizuia ugawaji wa stika za ukaguzi holela ili magari yaweze kukaguliwa kikamilifu, jambo lililosaidia kupunguza ajali.

“Mwaka huu napendekeza, fedha zitakazopatikana kwenye stika zitumike kununua magari ya kikosi cha usalama barabarani mikoani ili kuboresha utendaji kazi,” alisema Masauni.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Fortunatus Musilimu, alisema hadi sasa ajali zimepungua kutokana na ukaguzi wa mara kwa mara unaofanyika.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kulikuwa na ajali nyingi, lakini sasa hivi hali ni shwari, baadhi ya madereva wanatii sheria kutokana na elimu inayotolewa pamoja na kusimamia sheria.

“Mabadiliko ya sheria yakifanyika tutakuwa na matokeo chanya katika ukaguzi wa magari barabarani pamoja na askari wetu kuzingatia sheria,” alisema Musilimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,476FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles