23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Jaji Warioba awapigia chapuo wanawake majimboni

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amewapigia chapuo wanawake kupewa nafasi ya kugombea ubunge wa kuchaguliwa badala ya viti maalumu ambavyo amesema vinawafanya kuonekana kama daraja la pili.

Alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Jinsia lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

Tamasha hilo linalenga kuwaleta pamoja  wahanarakati wa haki za binadamu kutafakari na kusherehekea mafanikio, kubadilishana mawazo na uzoefu, kubaini changamoto.

 Jaji Warioba alisema kuwa anafikiri sasa umefika wakati taifa liamue kwa dhati kwamba katika utekelezaji wa mambo kutakuwa na 50 kwa 50 na kwamba ili kufikia hilo inabidi kuiangalia sheria ya uchaguzi ili iweke utaratibu ambao utahakikisha kwenye uchaguzi uwiano huo unafikiwa.

“Itafika mahali sasa hatutakwenda uwakilishi wa uwiano ili uwe na uhakika kwamba tangu uteuzi utapata 50/50, hilo tuanze kulifikiria maana tutakuwa tunazungumza hivi viti maalumu vinamfanya mbunge kama ‘second class’ (daraja la pili).

“Nadhani mpaka sasa hivi sheria yetu inasema kuwa Waziri Mkuu lazima uwe umechaguliwa. Kwa hiyo hawa wenye viti maalumu hawana sifa za kuwa Waziri Mkuu, kwanini? Mimi nadhani sasa kama taifa tuzungumze tuamue tuwe na utaratibu ambao utawahakikishia 50/50,”  alisema Jaji Warioba.

Alisema nguvu ya Watanzania iko kwenye umoja, mshikamano na uzalendo na taifa lina amani.

Jaji Warioba alisema ni muhimu kulinda umoja, mshikamano na uzalendo japo kuna dalili zinazoonyesha kuwapo majaribio ya kudhoofisha.

Hata hivyo Jaji Warioba alisema wanawake nchini wamesimama kidete katika kulinda umoja, mshikamano na uzalendo.

“Nilikwenda Bagamoyo nikakuta kuna semina ya wabunge wanawake wanaongozwa na mama Anna Abdallah na Suzan Lyimo, wanazungumza lugha moja, hawakugawanyika kwamba hawa CCM, hawa Chadema, hawa CUF, walikuwa wanazungumza mambo ya kitaifa, wanazungumza kwa pamoja,” alisema Jaji Warioba.

Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda, aliwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 badala ya kuishia kupiga kelele.

“Simameni kwenye uchaguzi, kelele zote kwenye uchaguzi tunafanya sisi, lakini tunawaachia wenyewe (wanaume) maandailizi, tena siyo Tanzania tu, kote ukiona wanawake wanashangilia uchaguzi utafikiri wao ndio wameshinda, utakuta wengine wamelala chini, inakuwaje kwenye kugombea,” alisema.

Mgeni rasmi katika tamasha hilo, Naibu wa Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Nugulile, aliwashawishi wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles