23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Biashara kakakuona yashika kasi nchi za Asia

BAKARI KIMWANGA-ALIYEKUWA THAILAND

TAASISI mbalimbali za kimataifa zimekuwa na mkakati madhubuti wa kulinda rasilimali hasa wanyama akiwamo kakakuona ambaye kwa sasa yupo hatarini kutoweka.

Hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na usafirishaji haramu wa wanyamapori kutokana nchi za Afrika hasa zile za Afrika Magharibi zikiwamo Ghana na Nigeria, na kwa upande wa Afrika Mashariki Kenya ikitajwa kama sehemu ya uchochoro wa ukusanyaji wa wanyama hao na kuwasafirisha kwenda nchi za Asia.

Timu ya wanahabari watano kutoka nchini ilitembela nchini Thailand na kuzunguka kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo sehemu maalumu za wanyama waliokamatwa  kutoka nchi za Afrika, Idara ya Forodha Uwanja wa Ndege wa Suvarnabhumi na soko la bidhaa ya wanyamapori.

Wanahabri hao waliungana na wenzao wa nchini Thailand, ambapo kila upande uliweza kutembelea kwenye nchi za wenzake kwa lengo la kubadilishana uzoefu na taarifa kuhusu usafirishaji haramu wa wanyamapori, chini ya ufadhili wa USAID Protect Tanzania na USAID Wildlife Asia, kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).

Hata hivyo, nchi ya Ghana imelazimika kuingia katika mkakati wa kuangalia upya sheria zake za wanyamapori kutokana na biashara ya kakakuona ambayo imekithiri kwa kasi kubwa.

Hali hii imesababishwa na hofu ya kwamba nchi hiyo inatumiwa kuendesha biashara haramu.

Zaidi ya kilo 31,000 ya magamba ya kakakuona ilikamatwa duniani kote mwaka huu, hali hiyo inabainishwa na ripoti ya Shirika la Kimataifa la Ustawi wa Wanyama (IFAW).

Katika kipindi cha Mei na Juni mwaka huu, shehena mbili kubwa zilinaswa nchini Malaysia, ambapo pia kilo 700 zilipatikana zikiwa zimesafirishwa kupitia Ghana. Huku shehena nyingine kubwa zikikamatwa pia nchini Uganda, Camerron na Ivory Coast.

Mmoja wa maofisa wa juu wa IFAW, Mark Hofberg, anasema magamba mengi kutoka kwa mnyama huyo Afrika yameuzwa ili kufikia mahitaji yake katika Bara la Asia, ambako hutumiwa katika dawa za jadi.

Kakakuona anapatikana zaidi katika nchi za Afrika na Kusini Mashariki mwa Asia.

Aina mbili kati ya nane ya mnyama huyo wameorodheshwa kuwa hatarini, wakiwekwa katika orodha nyekundu ya aina ya wanyama walio hatarini.

 “Kuongezeka kwa kamatakamata ya mizigo hiyo kunaweza kuwa ishara kwamba mamlaka husika zinalichukulia suala hili kwa uzito, lakini nchi nyingi hazina sheria kali za kuadhibu wafanyabiashara haramu.

“Kwa biashara hii kupungua kwa kiasi kikubwa, kunahitajika adhabu na hukumu kali,” anasema Hofberg

Kakakuona ni mnyama aliyehifadhiwa nchini Ghana, ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Wanyamapori wa Ghana, Nana Kofi Adu-Nsiah, anasema sheria kali inahitajika.

Sheria zilizopo za ulinzi wa wanyamapori zilipitishwa katika miaka ya 1960 na tume hiyo inataka ziangaliwe upya ili kufikia viwango vya kimataifa.

Kutokana na ujangili huo mpya ambao sasa unashika kasi, watu watatu walikamatwa nchini Ghana kuhusiana na mizigo iliyonaswa Juni, mwaka huu, nchini Malaysia.

Viongozi wa Serikali wanaamini sheria mpya zitazuia nchi za Afrika Magharibi kutumiwa kuwa hatua ya usafiri kwa wanyama hao wanaosafirishwa lakini pia kuna wasiwasi pia juu ya uwindaji wa ndani wa kakakuona.

Wanyama hao ambao wana ukubwa wa sentimita 30 hadi 100 wanaweza kuuzwa kwa karibu dola za Marekani 45 au Euro 38. Na wale wanaowauza kwa kawaida huwa ni watu masikini.

UTAFITI

Watafiti wamegundua kuwa kakakuona anatumika kwa ajili ya chakula na magamba yake yanatumiwa kama viungo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na USAID Wildlife Asia, uliainisha sababu za kuwapo kwa biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori kama tembo, faru, kakakuona na tiger kunatokana na imani na tamaduni zao hasa kwa raia wa nchi za Thailand, China na Vietnam, ambapo pia inaelezwa kuwa asilimia 20 ya tembo wa Afrika wanadaiwa kuuawa na sehemu ya viungo vyao (pembe) husafirishwa kwa njia ya zisizo halali na kuingia kwenye nchi hizo.

“Mtu anatoa zawadi iliyotengenezwa kwa mazao ya wanyamapori kwa familia, marafiki, masuala ya kijamii na mitandao ya kibiashara kwa mazao ya wanyama wote wanne,” anaeleza mtaalamu wa mawasiliano na kubadilisha tabia wa USAID Wildlife Asia, Wenweena Tangsathianraphap.

Naye mfuatiliaji na mtaalamu wa uthamini na ufuatiliaji USAID Wildlife Asia, Pakprim Oranop, anaweka wazi suala hili na kusema kwamba bara hilo mtu kuvaa kidani au kitu chochote kilichotengenezwa kwa kiungo chochote cha mnyama ni ishara kwamba naye atakuwa jasiri kama mnyama aliyetokana na bidhaa hiyo au anajihakikishia ulinzi.

Hatya hivyo, pia wapo wenye imani kwamba inaongeza nguvu za kiume au uwezo wa mwanamume kutambulika kuwa rijali, na wengine wakitumia kama dawa ya kuwafanya kuwa imara kama mnyama husika.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na USAID Wildlife Asia, ya kwanini watu wanatumia bidhaa za wanyamapori, walibaini kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya imani na utamaduni kwa wanaotumia bidhaa za wanyamapori.

“Wengi waliamini kuwa anapotumia kitu chochote kilichotengenezwa kwa jino la tembo, pembe ya faru au tiger (chui) basi naye atakuwa na matendo ya kishujaa kama huyo mnyama, ndiyo maana wengi wameendelea kutumia,” anaeleza.

Katika utafiti wa walaji wa mwaka 2018, kati ya watu 10 waliohojiwa ambao ni wanunuaji na watumiaji kwa miezi 12 iliyopita, ulibainisha kuwa nchini China watumiaji wa bidhaa za tembo asilimia 4.01 ni vya tofauti, asilimia 3.86 waliamini katika imani za kiroho na asilimia 3.79 waliamini katika urembo.

Kwa upande wa kakakuona, asilimia 4.14 waliamini inaponya maradhi mbalimbali, 3.72 inaleta afya njema na maisha mazuri na asilimia 2.74 inaongeza nguvu za kiume.

HALI ILIVYO THAILAND

Asilimia 94 ya waliohojiwa nchin Thailand, wanasema wanatumia bidhaa za meno ya tembo kwa kuwa ni kitu cha tofauti na thamani kubwa, asilimia 88 wanasema inaleta matumaini na bahati, wakati asilimia 79 wanasema inawalinda dhidi ya adui na majanga.

Kutokana na hali hiyo, Mwakilishi wa Shirika la Kudhibiti Usafirishaji wa Wanyamapori Asia (Traffic), Monica Zavagli, anasema biashara ya mazao ya wanyamapori inahusisha watu wenye mtandao mkubwa na wenye fedha nyingi ambazo huzitumia kununua nyara hizo.

“Hii biashara ni kubwa ambayo inatumia zaidi ya Dola za Marekani bilioni tisa hadi 30 kwa mwaka, mtandao huu unatumia taasisi za kifedha kuhamisha fedha na benki zina uwezo wa kuchunguza kwamba fedha hizo zinatokana na nini kama zinahusisha ujangili,” anasema.

“Hata hivyo, nchi kama Tanzania imefanya vizuri kuwa na sheria kali, lakini jitihada zaidi zinahitajika katika kushirikisha taasisi za fedha, kwa kufuatilia mali na mienendo yao kama fedha hizo zinahusisha biashara hiyo itasaidia kumaliza mtandao huo,” anasema Monica.

Mkuu wa USAID Asia, Craig Karkpatrick, anasema ripoti ya polisi wa kimataifa imeonyesha kuwa biashara haramu ya mazao ya wanyamapori ipo na inafanyika kwa kiasi kikubwa.

HALI ILIVYO TANZANIA

Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya uchumi kwa Taifa ya mwaka 2017, inaonesha kwamba sekta ndogo  ya  wanyamapori  ilikusanya zaidi ya Sh milioni 29 ikilinganishwa na zaidi ya Sh milioni 38 mwaka 2016, sawa na upungufu wa asilimia 22.7.

Kati ya mapato hayo, mapato kwa sarafu ya ndani yalikuwa Sh 2,904,631,101.82 na  sarafu ya nje yalikuwa ni Dola za Marekani 11,940,029.80 ikilinganishwa na Sh  242,843,673,275 na Dola za Marekani 17,473,260 mwaka 2016.

Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kingwangalla, Serikali inaendelea na jitihada za kulinda rasilimali za wanyamapori dhidi  ya  ujangili na  uvunaji usio endelevu.

Katika kipindi hicho, anasema kulikuwa  na siku  za doria 262,770 zilizofanyika katika maeneo ya wazi na yaliyohifadhiwa ikilinganishwa na siku za doria 518,809  zilizofanyika mwaka 2016.

NYARA ZILIZOKAMATWA

Kutokana na doria hizo, nyara za Serikali za aina mbalimbali zilikamatwa ambazo ni  pamoja na meno ya tembo 296 yenye  jumla  ya  uzito  wa  kilo 929.8; nyamapori kilo  12,776;   meno mawili ya simba, kakakuona 644; ngozi  10  za chui na ngozi moja ya simba.

Anasema pia jumla ya silaha 5,309 zilizohusika katika ujangili zilikamatwa  zikiwamo SMG tisa, hunting rifles 14, shotgun 56, gobore 212,  bastola mbili na  nyaya za kutegea wanyama 5,016.

Huku watuhumiwa 3,889 wa makosa mbalimbali yakiwamo ujangili nao walikamatwa na kesi zao kuamuliwa na waliopatikana na hatia walilipa faini jumla ya Sh milioni 1.108 na wengine kufungwa jela miezi 12. Kesi 3,011 zilizobaki zilikuwa zinaendelea katika mahakama mbalimbali nchini.

MSIMAMO WA CITES

Katika mkutano wa wawakilishi wa nchi 183 wanachama wa mkataba wa kimataifa wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka (CITES), uliofanyika hivi karibuni Geneva, Uswisi kwa lengo la kuimarisha mikakati ya kulinda viumbe hao, wanatoka na mapendekezo 56 yenye lengo la kuimarisha na kulinda viumbe vya porini.

Katibu Mkuu wa CITES,  Ivonne Higuero, anasema tayari nchi hizo wanachama zimewasilisha mapendekezo 56 yenye lengo la kubadili na hatimaye kuimarisha kanuni za kulinda viumbe vya porini wakiwamo wanyama pamoja na maua, ambavyo vinauzwa kwenye soko la kimataifa.

“Mapendekezo mengi yanalenga kuhakikisha kuwa viumbe hivyo vilivyoko hatarini na ambavyo vinaendelea kuuzwa, vinasalia endelevu na hivyo mapendekezo yanataka vibali kutoka CITES ili kuruhusu biashara yao,” anasema Higuero.

Anasema mapendekezo mengine yanataka kupigwa marufuku kwa biashara za viumbe vilivyoko kwenye orodha I ilihali mengine yanataka kuwa viumbe ambavyo tayari idadi yao imekaa sawa vihamishwe kutoka orodha ya I kwenda orodha ya II ya mkataba wa CITES.

Anakumbusha kuwa kanuni zilizo wazi na zinazotekelezeka kwa kuzingatia sera thabiti ni muhimu katika kulinda utajiri wa asili na kufanikisha malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs),  ambayo yalipitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2015.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles