Jaji Chande awapa somo wanasheria chipukizi

0
2038

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

JAJI mstaafu wa Mahakama Kuu Tanzania, Mohamed Chande, amesema pamoja na kuwa na idadi kubwa ya mawakili nchini wapatao 6,750, bado watu wengi wa mikoani wamekuwa wakikosa uwakilishi wa mawakili wa kujitegemea, wengi wao wakitajwa kuzamia mijini pekee.

Amesema makadirio kwa Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 58, wakili mmoja anahudumia watu 82,857 wakati Afrika Kusini ambayo inalingana kwa kiasi kikubwa na idadi ya watu, wakili mmoja anahudumia watu 2,500.

Hayo aliyasema mwishoni mwa wiki Dar es Salaam wakati akitoa mhadhara kuhusu jukumu la wanasheria chipukizi kwa umma na mwelekeo wa sekta ya sheria nchini.

Jaji Chande alisema kuwa wanasheria na mawakili wanatakiwa kwenda kufanya kazi vijijini na kama maofisa wa mahakama wakasaidie katika utoaji haki na kuongeza kuwa asilimia 70 ya kesi nchini zipo mahakama za mwanzo, lakini wananchi wanajiwakilisha wenyewe.

Alisema wakiwa wanasheria vijana, wanapaswa kuhakikisha wanafikia wananchi waliopo vijijini ili kuwasaidia katika masuala yao ya kisheria na kusaidia mahakama katika utoaji haki kwa haraka zaidi kwani mawakili wengi wamekuwa wakiishia kufanya kazi mijini kuliko vijijini.

“Katika Mkoa wa Lindi kuna wakili mmoja huku mawakili nane wakiwa katika Mkoa wa Katavi, 20 mkoani Ruvuma, 29 Kigoma na 38 wapo mkoani Mara,” alisema Jaji Chande.

Alisema kuna baadhi ya mikoa takribani saba ya Tanzania Bara haina Mahakama Kuu kama vile Lindi, Katavi, Morogoro, Simiyu, Manyara, Pwani, Singida na Songwe huku wilaya 28 zikiwa hazina mahakama za wilaya kama vile Mkinga mkoani Tanga.

“Kutokuwepo kwa mahakama ni kikwazo kikubwa katika utoaji wa haki na masuala ya sheria, hususani kwa mawakili wachanga.

“Hivyo tutaendelea kuishauri Serikali kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya mahakama ili watu waweze kupata haki zao, natambua kuna mchakato wa mahakama wa kuhakikisha kila wilaya inakuwa na mahakama,” alisema.

Jaji Chande alisema ripoti ya dunia ya mwaka 2019 kuhusu utoaji haki inaonyesha watu milioni 230 wanaoishi katika mazingira mbalimbali wanakosa haki, huku watu bilioni 1.5 wanashindwa kutatua matatizo yanayowakabili yanayohusu haki na watu bilioni 4.5 wametengwa na fursa zitolewazo na sheria.

Alisema hali hiyo inaonyesha kutokuwepo kwa usawa au ufikishaji sawa wa haki kwa wote na ukosefu mkubwa wa uwakilishi wa kisheria.

Jaji Chande alisema katika miaka mitano iliyopita, zaidi ya asilimia 50 ya mawakili wamepokewa nchini kufanya kazi, hivyo anaamini wataendelea kubadilisha muundo na taasisi ya sheria.

Kwa upande wake, Balozi Juma Mwapachu alisema Serikali imefanya jitihada kubwa kuimarisha miundombinu ya mahakama, lakini bado watu wengi wana uhitaji wa kusaidiwa katika masuala ya utoaji haki.

“Wanasheria wachanga wanatakiwa kujua wanaisaidiaje jamii katika masuala ya sheria pamoja na kupigania haki za binadamu, uhuru wa kuongea na katiba,” alisema.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (TDHRC), Onesmo Olengurumwa, alisema ni wakati wa mawakili kuhakikisha wanakwenda vijijini kuwasaidia wananchi walio wengi ambao hawajui masuala ya sheria.

Alisema wanasheria wanapaswa kuwa na wito na uelewa mkubwa katika kuendesha kesi zenye masilahi kwa umma na zile za kimkakati zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here