28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yachukizwa mgongano DC, DED Malinyi

MWANDISHI WETU-MOROGORO

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amechukizwa na mgongano uliopo kati ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo (DED),  Mussa Mnyeti, hivyo kumwelekeza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza weledi wa utendaji kazi wao.

Agizo hilo alilitoa jana wakati akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Malinyi pamoja na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Toboa, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

“Ni aibu, Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli amewateua vijana wawe viongozi, lakini leo hadi wananchi wa kawaida wanajua mgongano wenu maofisini. Ni aibu Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi mnagombana, tena wakati mwingine mnagombania miradi, mmesahau kutekeleza majukumu yenu,” alisema Majaliwa.

Alisema  Serikali imewapa nafasi hiyo ili wakasimamie maendeleo ya wananchi na inapeleka fedha kuboresha maendeleo ya jamii kama kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara, lakini wao wanagombania miradi na mingine wanaichakachua.

Majaliwa alisema mbali na CAG na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza utendaji wa viongozi hao, pia ameuelekeza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakakague miradi ya ujenzi inayotekelezwa kwenye wilaya hiyo kama ubora wake unalingana na thamani halisi.

“Baada ya kupata majibu ya uchunguzi na kubaini kiini cha tatizo ndani ya wilaya hii hatua zitachukuliwa,” alisema.

Awali, Mbunge wa Malinyi, Dk. Haji Mponda (CCM),  alimweleza Waziri Mkuu kwamba kwenye wilaya hiyo kuna matatizo ya uhusiano kati ya Serikali na halmashauri jambo linalosababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo.

Mbunge huyo alisema kutoelewana kwa viongozi wa wilaya hiyo – DC na DED, kumesababisha mgawanyo mkubwa kuanzia katika Baraza la Madiwani hadi kwa wananchi mitaani, hivyo alimwomba Waziri Mkuu awasaidie katika kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema kuwepo kwa mabango mengi kwenye mikutano ya hadhara  ya viongozi wakuu, kunadhihirisha wazi kwamba watendaji wa halmashauri hawawatembelei  wananchi katika maeneo yao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

“Watendaji hamuendi kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekani wawe wanawasubiri viongozi wa juu na kuwasilisha kero zao kwa njia ya mabango, sasa jipangeni, haya mabango yote mtakuja kuyajibu kwa sababu katika mabango yao hakuna hoja hata moja inayomuhusu Waziri Mkuu, zote ni za ngazi ya halmashauri,” alisema.

Alisema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles