24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

JAFO AINYOOSHEA KIDOLE SEKONDARI YA ILIBORU

Na JANETH MUSHI-ARUSHA


WAZIRI wa Tamisemi, Seleman Jafo, amesema haridhishwi na matokeo ya Shule ya Sekondari Iliboru ambayo ni ya vipaji maalumu.

 

Aidha, Jafo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, kuanzisha kampeni maalumu ya kuondoa sifuri mkoani Arusha kwa upande wa matokeo ya kidato cha nne na sita.

Waziri Jafo alitoa maagizo hayo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na walimu wa shule hiyo alipoitembelea na kukagua ukarabati wa madarasa, mabweni na maabara katika shule hiyo iliyojengwa mwaka 1970.

“Siridhishwi na matokeo yenu kwa sababu mwaka jana mlikuwa wa 12 kati ya shule 449 za Serikali katika matokeo ya kidato cha sita na mlikuwa wa pili kati ya shule 28 mkoani hapa. Nimeambiwa katika matokeo ya kidato cha nne mlikuwa wa 42 kati ya shule 3452 kitaifa.

“Iliboru ni miongoni mwa shule kongwe zinazokarabatiwa na Serikali ili kuboresha mazingira na ufaulu katika shule hizo.

“Kwa hiyo, ndiyo maana nasema siridhishwi na matokeo haya, nataka shule hii iwe kinara kwani ni aibu shule ya vipaji maalumu kuwa na matokeo haya.

“Najua Shule ya Kisimiri Juu imewavuruga na imewapita baada ya kuwa kinara katika mkoa wenu. Nawapongeza kwa kuwa mnaongoza kwa shule za Serikali, lakini nataka muongoze kwa shule zote.

“Nataka Iliboru iwe kinara, nafahamu uwezo huo mnao, tunataka hizi shule kongwe ziwe bora kwani walimu mkijipanga vizuri, hakuna kitakachoharibika kwani nasikia hata katika matokeo ya kidato cha sita, mmeondoa daraja la nne na la mwisho,” alisema Jafo.

Naye Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Evaline Moshi, alisema shule hiyo yenye wanafunzi 890 na walimu 76, inakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.

Pia, Moshi alitaja mikakati ya shule ili kuongeza ufaulu kuwa ni kufundisha madarasa ya mafunzo rekebishi nyakati za jioni, kusimamia na kuratibu taaluma na nidhamu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles