24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

TUME KUUNDWA KUCHUNGUZA GARI ZA POLISI BANDARINI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, ameagiza kuundwa tume kufanya ukaguzi wa kina baada ya kubainika magari matano kati ya 53 yaliyonunuliwa kwa ajili ya Jeshi la Polisi yana kasoro.

Pia ameagiza kupitiwa upya kwa mkataba wa ununuzi wa magari hayo ambao unaihusisha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Kampuni ya Ashok Leyland.

Alitoa agizo hilo jana baada ya kutembelea Chuo cha Polisi Kurasini yalikohifadhiwa magari hayo ambayo yanahusisha maroli 31 na magari madogo 22.

“Magari 53 yametengeneza masuala ambayo ni lazima majibu yake yapatikane. Ukaguzi wa ‘supplier’ unaonyesha baadhi yana hitilafu lakini haya ni magari mapya, hili linatosha kunipa shaka.

“Jambo hili hatuwezi kuliacha lipite hivi hivi, hivyo tunalazimika kufanya ukaguzi wa kina,” alisema Masauni.

Alisema tume hiyo itahusisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali ili kubaini ubora wa magari yote.

“Ikiwezekana Temesa (Wakala wa Ufundi) na NIT (Chuo cha Taifa cha Usafirishaji) ambao wana teknolojia za kisasa wahusishwe, si busara kutoa muda kisiasa lakini uchunguzi utafanyika haraka iwezekanavyo,” alisema Masauni.

Kwa mujibu wa Masauni, kasoro hizo zimebainika baada ya ukaguzi uliofanywa na msambazaji na kwamba huenda zikaongezeka zaidi pindi serikali itakapofanya uchunguzi wake.

Naibu Waziri huyo pia alihoji kwanini magari hayo bado yako chuoni hapo wakati jeshi lina changamoto ya usafiri katika maeneo mbalimbali nchini.

“Baada ya magari kufika yanatakiwa yakaguliwe tena na kwa sasa ‘supplier’ ndio amemaliza na sisi tutafanya tena ukaguzi,” alisema Kamishna wa Fedha, Mipango na Logistiki, Albart Nyamuhanga.

BANDARINI

Naibu Waziri huyo pia alitembelea bandarini ambako kuna magari 119 na kuagiza yatolewe haraka.

“Haya yaliyopo bandarini hakikisheni yanatolewa haraka. Hatutarajii Rais aje atoe maelekezo mengine…sisi tutakuwa hatuna faida,” alisema.

Kwa mujibu wa Masauni, hadi sasa yamenunuliwa magari 234 kati ya 777 yanayotakiwa kulingana na mkataba.

MSAMBAZAJI

Awali Msambazaji kutoka Kampuni ya Ashok Leyland, Ragho Donepudi, alisema walifanya ukaguzi katika magari 53 na kubaini matano yana itilafu.

Baadhi ya itilafu hizo ni za rejeta, pampu na gari lingine funguo ikiwekwa haitoki.

Licha ya mkataba kuelekeza kununuliwa magari mapya lakini miongoni mwa magari hayo liko ambalo tayari limetembea kilomita 1,000.

MKATABA

Kamishna wa Fedha, Mipango na Logistiki, Albart Nyamuhanga, alisema mkataba unahusisha ununuzi wa magari 777 na uliingiwa mwaka 2013.

Alisema gharama za magari yote ni Dola za Marekani 29,600,100 ambazo ni mkopo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles